Trump alivyomtoa mchezoni Biden kwenye mdahalo

Dar es Salaam. Kabla ya Alhamisi jioni, Wamarekani wengi walikuwa wameelezea wasiwasi wao kuhusu umri wa Rais wao, Joe Biden na ubora wa afya yake kwenye majukumu yake ya kiofisi.

Biden aliingia kwenye mdahalo baina yake na Donald Trump akiwa na matarajio ya chini, na akateleza. Alikuwa mnyonge. Alikuwa anazungumza bila mpangilio na hana uwazi.

Hata hivyo, katikati ya mjadala, upande wa kampeni ya Biden uliwajulisha waandishi wa habari kwamba kiongozi huyo alikuwa anakabiliwa na mafua jaribio la kuelezea sauti yake iliyokuwa kavu. Hilo linaweza kuwa kweli, lakini pia lilionekana kama kisingizio tu na si sababu halisi.

Kwa dakika 90, Biden alionekana kuwa katika hali yenye shaka, baadhi ya majibu yake hayakuwa na maana. Baada ya kupoteza mwelekeo wa mawazo, alitoa jibu kwa swali moja kwa kusema, “Hatimaye tulishinda Medicare”, akiwa anarejea mpango wa Serikali wa huduma za afya kwa wazee.

Mkurugenzi wa zamani wa mawasiliano wa Biden, Kate Bedingfield, alionekana kwenye kituo cha runinga cha CNN mara baada ya mdahalo, na alikuwa wazi: “Hakuna namna nyingine ya kusema, haukuwa mdahalo mzuri kwa Biden.”

Kate alisema suala kubwa la Biden lilikuwa kuwathibitishia Wamarekani kwamba alikuwa na nguvu na uvumilivu, lakini hakufanikiwa kufanya hivyo.

Mdahalo ulipoendelea, kama bondia aliyebanwa kwenye kamba, Biden alianza kutoa mashambulizi makubwa dhidi ya mpinzani wake kwa jaribio la kubadilisha mwenendo wa mdahalo. Baadhi ya mashambulizi hayo yalifanikiwa kumchokoza Trump hadi akatoa majibu ya hasira.

Kwamba mada za mwanzo zilizoulizwa na waendesha mdahalo wa CNN zilihusu masuala muhimu kwa wapiga kura kama uchumi na uhamiaji ambapo kura za maoni zinaonyesha Wamarekani wanamwamini Donald Trump zaidi.

“Kwa kweli sijui alichosema mwishoni mwa sentensi hiyo, na sidhani kama yeye pia anajua,” Trump alitania baada ya jibu lingine kutoka kwa Biden.

Trump alivyojibu kwa weledi

Rais huyo wa zamani alionyesha kiwango fulani cha umahiri na nidhamu. Alifanikiwa kuepuka aina ya maudhi na ukali yaliyoathiri mdahalo wake wa kwanza mwaka 2020 na alimrejesha rais kwenye mjadala, huku akishambulia rekodi ya Biden kila ilipowezekana.

Mara kwa mara alitoa madai ambayo hayakuwa na ukweli pamoja na uwongo wa wazi, lakini Biden hakuweza kumkabili sana juu ya madai yake hayo.

Mada ilipobadilika na ikahusu utoaji mimba, kwa mfano, Biden alihamisha mara kwa mara umakini kwa kile alichosema ni misimamo mikali ya chama cha Democrat. Alidai, kimakosa kwamba wanachama wa chama hicho wanaunga mkono utoaji mimba hata baada ya watoto kuzaliwa.

Utoaji mimba ni suala ambalo limeonekana kuwa udhaifu kwa Trump na wanachama wake wa Republican kwa ujumla tangu kubatilishwa kwa Roe v Wade (hukumu maarufu ya Mahakama Kuu ya Marekani iliyotolewa mwaka 1973. Hukumu hiyo ilithibitisha haki ya mwanamke kupata huduma ya utoaji mimba.) ambayo ilikuwa inalinda haki ya kikatiba ya utoaji mimba kulikofanywa na Mahakama ya Juu mwaka 2022.

Kwa kifupi, Roe v. Wade ilibainisha kuwa Katiba ya Marekani inatoa haki ya faragha ambayo inajumuisha haki ya mwanamke kufanya maamuzi juu ya afya yake ya uzazi, ikiwa ni pamoja na uamuzi wa kutoa mimba. Hukumu hii ilisababisha mabadiliko makubwa katika sera ya utoaji mimba nchini humo.

Lakini, mashambulizi ya Biden katika eneo hili ambalo angeweza kupata pointi hayakuzaa matunda.

Kamala Harris akiri Biden alibanwa

Muda mfupi baada ya mdahalo huo, Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris alikiri kwamba rais alikuwa na ‘mwanzo mzito’ lakini alimaliza mdahalo kwa nguvu na uthabiti.

Hata hivyo, maneno ya Kamala yalikuwa ni ya matumaini, lakini ukweli ni kuwa Biden alijirekebisha kadri mdahalo ulivyokuwa ukiendelea.

Katika kukumbuka masuala, Biden aligusia hukumu ya Trump juu ya mashitaka yaliyotokana na madai ya uhusiano wa kimapenzi na nyota wa filamu za ponografia, Stormy Daniels, na kusema rais huyo wa zamani alikuwa na ‘maadili ya paka wa mtaani’.

“Sikuwahi kufanya mapenzi na nyota wa filamu za ponografia,” Trump alijibu kwa ukali.

Trump pia alionekana kukosa mwelekeo alipokuwa akijibu shambulio la Januari 6, 2021, kwenye Jengo la Capitol la Marekani.

Tarehe hiyo kulitokea tukio la uvamizi kwenye Jengo la Bunge la Marekani, maarufu kama Capitol Hill. Uvamizi huo ulifanywa na wafuasi wa Trump, wakati huo akiwa angali rais wa Marekani, baada ya hotuba yake karibu na Ikulu ya White House.

Uvamizi huo ulisababisha kusitishwa kwa kikao cha Bunge kilichokuwa kikithibitisha matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Marekani na kusababisha ghasia na uharibifu. Tukio hilo lililoacha kovu kwenye historia ya Marekani.

Awali, Trump alijaribu kukwepa swali kuhusu uwajibikaji wake kwa ghasia za Capitol, lakini safari hii Biden hakumwacha akwepe.

“Aliwahimiza wale watu kwenda Capitol Hill. Alikaa hapo kwa saa tatu huku wasaidizi wake wakimsihi afanye kitu,”. “Hakufanya lolote kabisa,”alisema Biden.

Trump pia alijaribu kukwepa alipoulizwa kama atakubali matokeo ya uchaguzi wa 2024.

Huu ulikuwa mdahalo wa mapema zaidi katika historia ya kisiasa ya Marekani, kwa sababu timu ya Biden ilitaka iwe hivyo. Sababu moja ni kwamba walitaka kumvurugia Trump katika msimu wa kampeni, wakiwa na matumaini kuwa wapiga kura wa Marekani watakumbuka hali ya machafuko ya wakati wa urais wake.

Lakini, watu wengi watazungumzia utendaji wa Biden baada ya mjadala huu kuliko wa Trump.

Sababu nyingine timu ya Biden ilitaka mdahalo huo ili kumpa mgombea wao muda zaidi wa kujirekebisha kutokana na utendaji dhaifu.

Related Posts