Wabunge wahoji ugawaji wa maeneo ya utawala

Dodoma. Wakati baadhi ya wabunge wakihoji kuhusiana na ugawaji wa maeneo ya utawala, Serikali imesema kwa sasa kipaumbele kimewekwa katika uboreshaji wa miundombinu kwenye maeneo hayo.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange ameyasema hayo leo Ijumaa Juni 28, 2024 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara.

Waitara amesema mwaka 2023, Serikali ilitoa maelekezo katika majimbo yao na watu walipendekeza kata, vijiji na mitaa na mamlaka ya miji ili yagawanywe.

“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, je katika maeneo tuliyopendekeza nini kauli ya Serikali kuelekea uchaguzi mwaka 2024,” amehoji Waitara.

Akijibu swali hilo, Dk Dugange amesema maeneo ambayo halmashauri imependekeza kupata maeneo mapya ya utawala, Serikali itaendelea kufanya kazi mahali inapoonekana inawezekana.

“Lakini hata kama haitapata idhini ya mpango kwa mwaka huu ambao tunaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa bado uchaguzi wa serikali za mitaa unaweza kufanyika kwa kufuata mipaka ileile ya siku za nyuma wakati utaratibu wa kuyagawa unaendelea,” amesema.

Amesema Serikali imepokea maombi hayo na inaendelea kuyafanyia kazi lakini haitaathiri uchaguzi wa serikali za mitaa wala ujao.

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Mlalo(CCM), Rashid Shangazi amesema mwaka 2016, wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti Waziri Mkuu alitoa tamko la kusitisha mamlaka mpya za utawala.

“Ni kwa jinsi gani tangazo hilo lifike mwisho sasa ili mamlaka mpya za utawala ziweze kutangazwa,” amehoji.

Pia, Shangazi amesema zipo kata zimegawanywa lakini hakuna ulinganifu kwa baadi ya majimbo kuwa na kata 20 na nyingine 8 hiyo haileti ulingalifu.

Amehoji kuwa Serikali haioni ni wakati sasa wakufanya mapitio ya mgawanyo huo.

Akijibu maswali hayo, Dk Dugange amesema Serikali inaendelea kupokea mapendekezo ya kugawa maeneo lakini kipaumbele wameweka katika kukamilisha miundombinu katika maeneo ya utawala.

“Kwa hiyo bado kuna upungufu mkubwa wa miundombinu, ofisi za wakuu wa wilaya, wakurugenzi, maofisa watendaji wa kata na vijiji bado tuna upungufu mkubwa miundombinu hiyo,”amesema.

Amesema baada ya hapo Serikali itapitia mapendekezo yaliyoletwa kwa ajili ya kubadilisha mipaka.

Dk Dugange amesema kuwa ni kweli kumekuwa na maeneo ya makubwa na madogo na kuwa Serikali iko tayari kupokea maoni ya wadau ili ione uwezekano wa kuyafanyia kazi.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Makambako (CCM), Deo Sanga amehoji ni lini Serikali itaigawa Kata ya Kivavi, Makambako.

Akijibu swali hilo, Dk Dugange amesema Serikali imekuwa ikizingatia suala la uanzishaji wa kata kwa mujibu wa kifungu cha 16 (1) – (3) cha Sheria za Serikali za Mitaa, Sura 288, ili kuchochea ukuaji wa shughuli za maendeleo.

Amesema katika mfumo wa mamlaka za serikali za mitaa, hadi sasa kuna kata 3,956 katika halmashauri 184.

Amesema utaratibu wa kugawa na kuanzisha kata uko kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 288 ambapo vikao huanzia ngazi ya vijiji baraza la madiwani, DCC na RCC kisha kuwasilisha Tamisemi.

Amesema ni vema hatua hizo zifuatwe.

Related Posts