Waathirika wa mafuriko Bukoba wapewa msaada

Bukoba. Kaya 49 zenye watu 147 zilizoathirika na mafuriko katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, wamekumbukwa na Serikali kwa kupatiwa msaada wa vifaa na chakula.

Kaya hizo ziliathiriwa na mvua iliyonyesha Mei 10, 2024 na kuleta  maafa katika Halmashauri ya manispaa ya Bukoba na kusababisha binti mmoja aliyetambulika kwa jina la Leah (19) kupoteza maisha.

Mafuriko hayo yaliziathiri kaya 49 zenye watu 147 kwa kukosa makazi na chakula katika Mtaa wa Kyaya, Kata Kahororo, wilayani hapa.

Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Idara ya Menejimenti ya Maafa imetoa pole kwa waathirika wa maafa hayo kwa kuwapatia vifaa vya kutumia na chakula cha kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Akizungumza na Mwananchi Digital  leo Ijumaa Juni 28, 2024, Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Joacob Nkerwa amethibitisha kupokea vifaa hivyo vya msaada wa kibinaadamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kuwasaidia waathirika hao.

Nkerwa amesema wamepokea blanketi 147, mikeka 98, ndoo 98 za lita 14, madumu ya maji 98, sahani 147 na vikombe 147 kutoka ghala la Dodoma.

Kwa upande wa chakula, amesema wamepokea pia tani 5.292 za mahindi kutoka Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA) kwa ajili ya waathirika 147 kwa kipindi cha miezi mitatu.

Vitu hivyo ambavyo havikutajwa thamani yake, vitagawiwa kwa kaya 18 zenye watu 93 ambao wamehifadhiwa kwa muda kwenye kambi ya Kituo cha Afya cha Kashai, kambi ya Shule ya Msingi Nyamkazi iliyohifadhi kaya 31 zenye watu 54.

Mkazi wa Buturage, manispaa ya Bukoba, Hassan Leonard ambaye pamoja na familia yake ya watu sita wamehifadhiwa kwenye kambi ya Shule ya Msingi Nyamkazi, amesema viongozi kuanzia ngazi ya mtaa hadi kitaifa, wanawatembelea mara kwa mara kuwajulia hali.

Mkazi wa Mtaa wa Kyaya, kata Kahororo, Benatha Anthony ameishukuru Serikali kwa msaada ambao wamekuwa wakiwasaidia mara kwa mara wa chakula na vifaa.

Benitha amesema wanapitia wakati mgumu maana hadi sasa hawajajipanga ipasavyo kupata viwanja vya kutengeneza familia zao kutokana na kutokuwa na kipato cha aina yoyote.

Mkuu wa wilaya Bukoba, Erasto Sima amewataka watu wote ambao wapo kwenye kambi mbalimbali walizotengewa na manispaa kwa ajili ya kujihifadhi kwa muda, kuanza kuhama maeneo hayo kwa kutafuta makazi mapya.

“Haya siyo makazi ya kudumu tafuteni sehemu ya kuishi, acheni kulazimisha kuishi kwenye maji, mji wetu wa Bukoba siyo mdogo, tafuteni viwanja sehemu nyingine mkaishi,” amesema Sima.

Related Posts