Morogoro. Mwili wa mtoto mchanga (Kichanga) umeokotwa leo juni 28, baada ya kutelekezwa daraja la Kasanga Msikitini, Barabara ya Kuu ya Morogoro Iringa Mtaa wa Mgaza Kata ya Mindu Manispaa ya Morogoro na mtu ambaye hakufahamika.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo juni 28, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mtaa wa Mgaza Spesioza Sylivestre amethibitisha kuokotwa kwa Mtoto huyo ambaye anakadiriwa na umri wa Siku moja ambaye alikuwa na jinsia ya kiume ambapo mpaka sasa aliyekitupa bado hajafahamika.
“Kwa ushirikiano wa wananchi la Polisi tumemuokota mtoto mchanga ambaye alikua ametupwa kwenye mtaa wangu, mtoto yule ametupwa kwenye ndoo na inavyoonekana ni mtoto wa siku moja, baada ya kufika na kuona mwili wa yule Mtoto mara moja nilitoa taarifa Polisi ambao walifika na kuchukua mwili wa huyo mtoto,” alisema.
“kwa kushirikiana na jeshi la polisi Bado tunaendelea na kutafuta ni nani ambaye ametupa kile kichanga ili aweze kuchukiwa hatua, lakini pia tunawaomba akina mama ambao wanatunza ujauzito na kuja kutupa watoto waache mara moja kwa maana tunaua nguvu kazi ya taifa,” ameonya.
Fatuma Mashaka mkazi wa mtaa wa Mgaza amesema Mwanamke ambaye alifanya tukio la kumtupa mtoto huyo amefanya kitendo cha kikatili ambacho hakivumiliki.
“Tendo la kumtupa huyu mtoto halivumiliki nanitendo la kinyama, mwanamke ukibeba mimba unatakiwa uzae na siyo kumtupa mtoto mtoni tena kwenye ndoo, baada ya kumuangalia alikutwa amefariki. Tunaziomba mamlaka zihakikishe aliyefanya tukio hili anakamatwa ili sheria ichukue mkondo wake,” amesema.
Teopista Alex amesema yeye alipata taarifa za mtoto huyo kutupwa kupitia kwa majirani zake ambapo alifika na kumuona mtoto huyo.
“Nilikuwa nafanya shughuli zangu nikaitwa, kuwa kuna mtoto ameonekana ametupwa daraja la Kasanga akiwa kwenye ndoo, nikafika na kuona mtoto ametupwa kwenye ndoo kwahivyo jamii inatakiwa ibadilike na vitendo hivi vya kikatili na mwanamke akizaa mtoto anatakiwa amlee akue na sio kumtupa,” amesema.
Mkazi wa Kasanga Fahad Ramadhan amesema hilo sio tukio la kwanza kutokea kwenye mtaa wao matukio kama hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara.
“Mwezi uliiopita kuna mwanamke mmoja alifariki eneo hili na leo tena ameokotwa Mtoto mchanga akiwa ametupwa kwenye eneo hili, pia kihistoria eneo hili kuna miili mingi ambayo iliwahi kuokotwa baada ya kutupwa hapa na huwa wanaofanya hawajulikani,” amesema.
“Tunaiomba Serikali iweke ulinzi na uangalizi maalumu eneo hili maana limekuwa likitumiwa na wahalifu kuleta miili baada ya uhalifu na kuitupa hapa na kiukweli hili halikubaliki kwakua watoto wadogo wanaoishi huu mtaa wanaona yanayoendelea hapa kwa kiasi kikubwa wanadhurika kisaikolojia,” amesema.