Lori la Kenya, shangingi la mbunge lililobeba Waethiopia kutaifishwa?

Moshi. Wakati raia watano wa Ethiopia waliokamatwa Juni 19,2024 wakisafirishwa uvunguni mwa lori la kusafirisha gesi wakifikishwa kortini na kukiri makosa yao, hatima ya lori hilo na ‘shangingi’ linalodaiwa ni mali ya mbunge itajulikana wiki ijayo.

Lori hilo aina ya Mercedes Benz lenye usajili wa Kenya kwa namba KCV 571Y lilikamatwa katika mji wa Tarakea uliopo mpakani mwa Tanzania na Kenya, wakati gari Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T888 BTY, lilikamatwa Juni 4,2024 likiwa na raia saba wa Ethiopia.

Hata hivyo, hadi sasa dereva wa gari hilo Toyota Land Cruiser ambalo nyaraka za umiliki zinasoma jina linalofanana na Mbunge anayetokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), hajapatikana na mmiliki wake anadaiwa kuwa nje ya nchi.

Kulingana na kifungu cha 46(1) cha sheria ya Uhamiaji sura ya 54 kama ilivyorejewa mwaka 2016, kimetamka makosa mbalimbali yanayoweza kutendwa na mtu ikiwamo kusafirisha na kuwahifadhi wahamiaji haramu.

Kifungu hicho kinatoa adhabu kwa mtu anayepatikana na hatia ya makosa hayo kuwa ni faini isiyopungua Sh20 milioni au kwenda kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.

Kulingana na kifungu kidogo cha (2) ni kuwa mbali na adhabu hiyo, mahakama kwa utashi wake yenyewe au maombi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), inaweza kuamuru kutaifishwa kwa chochote kile kilichotumika.

Hii kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (2)(a), inaweza kuamuru kutaifishwa kwa pesa na mali zilizopatikana kwa kuwaingiza kiharamu wahamiaji haramu na 2(b) chochote kile iwe nyumba au gari iliyofanikisha biashara hiyo haramu.

Kwa kuwa washtakiwa katika kesi zote mbili wamekiri makosa yao, katika hatua ya kutoa hukumu yake, Hakimu anaweza kutoa amri ya kutaifishwa kwa magari hayo mawili, kama kutakuwa hakuna kipingamizi cha kisheria kutoka kwa wamiliki.

Usikilizwaji wa awali (PH) kwa kesi zote mbili umepangwa kufanyika wiki ijayo.

Akizungumza na gazeti hili Juni 5,2024, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Fakih Nyakunga alisema kwa mujibu wa sheria za nchi gari likibainika kutumika kusafirisha wahamiaji haramu hutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.

Jana Juni 28, 2024, raia watano waliokamatwa chini ya uvungu wa lori la kusafirisha gesi nao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi mbele ya Hakimu Mkazi, Herieth Mhenga, ambao nao walikiri kosa waliloshitakiwa nalo.

Waliofikishwa kortini ni Admasu Bakala (18), Dagife Dasta (18), Abayna Safa (19), Emanuel Tegese (18) na Mesgana Trfo (18) ambaye ni mwanafunzi, ingawa haikutajwa wa ngazi gani ya elimu.

Akiwasomea kosa hilo, wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Issack Mangunu, amedai kuwa Juni 19,2024 huko Tarakea wilayani Rombo, washtakiwa waliingia nchini kinyume cha sheria kwa kutumia lori hilo la gesi.

Washtakiwa walikiri makosa yao ambapo mahakama imepanga Julai 2,2024 kuwa siku ya kuwasomea maelezo ya kosa lao, kuyakubali au kuyakataa na pale ambapo watayakubali kama yalivyo, basi mahakama itawapa adhabu wanayostahili.

Raia saba wa Ethiopia waliokamatwa katika ‘shangingi’ hilo, wao walifikishwa mahakama ya Wilaya ya Moshi mbele ya Hakimu Mkazi, Rehema Olambo na kusomewa mashitaka mawili ya kuwapo nchini bila uhalali ambayo waliyakiri.

Wahamiaji hao walifikishwa kortini Juni 14, 2024 na kusomewa mashitaka mawili na mwendesha mashitaka, wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Issack Mangunu, ambapo walikiri kutenda makosa hayo ya jinai.

Washtakiwa hao ni Tensa Matwis, Abi Arose, Buruk Helobo, Arigudo Aromo, Sisy Abera, Mirhetu Sulore na Sharifan Betiso na usikilizwaji wa awali umepangwa kuwa Julai 2,2024, ambapo mahakama inaweza kutoa hukumu dhidi yao.

Katika shitaka la kwanza, ilidaiwa kuwa Juni 4, 2024 huko Njiapanda katika wilaya ya Moshi, washtakiwa hao wakiwa raia wa Ethiopia, waliingia nchini kinyume cha sheria wakitumia gari lenye namba za usajili T888 aina ya Toyota Land Cruiser.

Katika kosa la pili, ilidaiwa kuwa siku hiyohiyo katika eneo hilohilo, washitakiwa walikutwa kinyume cha sheria wakiwa ndani ya ardhi ya Tanzania bila kuwa na hati halali za kusafiria au nyaraka yoyote ya kisheria inayowaruhusu kukaa nchini.

Related Posts