Watu 20,000 wapatiwa matibabu kambi madaktari bingwa Arusha

Arusha. Wananchi 20,000 wamehudumiwa katika kambi ya matibabu ya madaktari bingwa na wabobezi inayoendelea katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Akizungumza leo Ijumaa Juni 28, 2024, viwanjani hapo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema tangu kuanza kwa kambi hiyo Juni 24 hadi 27, 2024, wananchi 20,000 wamepatiwa vipimo, matibabu na dawa.

“Lengo letu siyo idadi ya watu wengi, lengo letu siyo kuutaka umaarufu, lengo letu ni wananchi wahudumiwe na wapate afya njema ili warejee katika maisha yao ya kupambania uchumi wa familia zao.

“Jumatatu hadi jana Alhamisi, wamehudumiwa watu wasiopungua 20,000, ni idadi kubwa ambayo walikuwa wanaishi majumbani wakiwa wamekata tamaa, hawana pesa ya kwenda kumuona daktari, kupata vipimo, kununua dawa, wamejikatia tamaa, wanamuomba Mungu wao na kwa mapenzi makubwa Mungu wao amesikia kilio chao,” ameongeza.

Makonda amesema kwa idadi hiyo, inaonyesha watu wenye uhitaji ni wengi na kuwa kwa sababu wameongeza madaktari na Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza dawa zitakazotumika katika kambi hiyo, hadi Jumapili Juni 30, 2024 ambayo ndiyo siku ya mwisho ya kambi hiyo, watu wengi watapata huduma hizo za afya.

Katika hatua nyingine, Makonda ametangaza ujio wa Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu na Mkurugenzi wa Tiba nchini ambao wataungana na wataalamu wengine kutoa huduma hizo.

Viwanjani hapo kwa sasa tangu kuanza kwa kambi hiyo, kumejaa mabanda maalumu yanayotumika kutoa huduma ambayo yamewekwa kuzunguka uwanja wote, huku kukiwa na madaktari na wataalamu wa afya zaidi ya 500 kutoka hospitali na Taasisi mbalimbali za afya nchini.

Baadhi ya wanufaika wa kambi hiyo wamesema kutokana na idadi ya wagonjwa kuongezeka kila siku, wanaomba shughuli hiyo iendelee kwa muda zaidi ili watu wenye mahitaji wapate huduma hiyo muhimu ya afya.

Mmoja wa wananchi hao, Sara Mtoba amesema alikuwa akisumbuliwa na viungo ikiwemo miguu, mgongo na kichwa ila kutokana na kutojiweza kiuchumi alishindwa kupata huduma za matibabu.

“Nimekuja hapa ni nzuri daktari amenisikiliza vizuri, nimepata ushauri, vipimo na matibabu, naamini dawa zitanisaidia niweze kupona na kurejea katika hali ya kawaida.

“Ukifika hapa kama utakuwa mvumilivu wa kuelekezwa na kusubiri matibabu, huduma ni nzuri. Lakini mimi naona siku saba hazitoshi, tunaomba atuongezee muda na madaktari maana mimi niliona Youtube ndiyo nikaja,” amesema.

Naye, Jackline Kennedy amesema wanashukuru kwa huduma hiyo kwani alikuwa na uvimbe katika bega la mkono wa kushoto ambalo limemsumbua kwa zaidi ya miaka miwili lakini kupitia kambi hiyo, ameweza kupatiwa vipimo na matibabu.

“Nashukuru kwa huduma hii kwani nimepitia changamoto hii kwa muda wa miaka miwili, na nimepewa rufaa hivyo nitaenda KCMC kwa matibabu zaidi,” amesema.

Dora Mollel amesema alikuwa akisumbuliwa na tatizo la nyonga pamoja na macho, hata hivyo alishindwa kuendelea kupata matibabu kutokana na kuwa na hali ngumu kiuchumi.

“Nina shida ya nyonga toka Desemba 2-23, nimeenda hospitali ya mbalimbali lakini sikufanikiwa kupona, sikuwa na uwezo wa kuendelea kwenda hosptali, mguu umekufa ganzi, nimekuja kwa kuchechemea hapa lakini nashukuru nimepatiwa vipimo na dawa, nasubiri matibabu zaidi.

“Tunashukuru kwa msaada huu, hatujawahi kupata, Makonda amekuja kwa wakati mwafaka, ametutetea ametupigania sisi wananchi wa hali ya chini ukiangalia huu umati watu wamekuja kwa kuwa ni wagonjwa lakini hawana uwezo wa kumudu matibabu,” ameongeza.

“Tunamshukuru ametutoa mahali, anatujali nimepimwa nimepewa dawa nimeenda kwenye mifupa nimepewa dawa, nilikuwa na shida kwenye jicho moja nimepimwa nimepewa miwani,” amesema.

Mapema leo asubuhi kabla ya kuendelea kwa matibabu hayo viongozi wa dini ambao ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel na Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Sheikh Shaban Juma, waliongoza sala na dua maalumu kwa ajili ya kambi hiyo.

Akizungumza baada ya sala hiyo, Sheikh Shaban amesema suala hilo linapaswa kuigwa na kila mwananchi hata kwa kumsaidia mhitaji mmoja wa afya na kuwa ni jambo lenye manufaa makubwa kwa wananchi.

“Kwa jambo hili ambalo mkuu wetu wa mkoa amebuni ni jambo lenye manufaa makubwa kwetu, tunamuombea Mungu ampe nguvu na ubunifu wa mambo mengine ambayo yana manufaa na maslahi kwetu sisi wananchi,” amesema.

“Hii tunaona ni chachu ama kichocheo cha kutafuta upendo kwa watu kwa sababu jambo hili ni jambo la heri na baraka na ambalo likitendwa watu wanakuwa na matumaini na serikali yao na utulivu tunaoukusidia utapatikana,” ameongeza.

Dk Mollel amesema viongozi wengine wanapaswa kuiga mfano huo wa Makonda, wa kuwa na moyo wa kusaidia wananchi wanaowaongoza.

“Makonda alianza na Wiki ya Haki na sasa anaendelea na Wiki ya Afya, na umati huu uliofika katika uwanja huu kupokea huduma unadhihirisha jinsi watanzania walivyo na mahitaji lakini fursa za kuyapata zinakosekana,” amesema.

“Tunatoa wito kwa viongozi wote wawe na moyo wa kusaidia, wawe tayari kuwasaidia wananchi huo ndiyo uongozi tunaoutegemea, kilichotokea hapa ni fursa kwa wananchi kupata fursa hii, tunamshukuru Mungu kwa Makonda aliyepata maono haya na kufanya kwa vitendo,” ameongeza Dk Mollel.

Related Posts