Geita. Washtakiwa wanne wanaodaiwa kumuua Milembe Suleman (43) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali, wamejitetea wakieleza kutohusika na tukio hilo, wakiiomba mahakama iwaachie huru.
Wamewasilisha ombi hilo mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Kelvin Mhina walipotoa utetezi wenyewe mahakamani hapo.
Juzi, upande wa mashtaka ulifunga ushahidi ukiwa na mashahidi 29 na vielelezo 19.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Dayfath Maunga (30), Safari Lubingo (54), Genja Pastory na Musa Pastory (33) ambao kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua Milembe Suleman.
Milembe aliuawa usiku wa kuamkia Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani, usoni na mikononi.
Akitoa ushahidi katika kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023, mshtakiwa wa kwanza Dayfath Maunga aliieleza Mahakama alikua akiishi na Milembe Suleman kama mtu na mfanyakazi wake.
Akiongozwa na wakili wake, Liberatus John amedai alikuwa akiuza duka la vipodozi na kumsaidia Milembe kwenye biashara zake za kukopesha fedha kwa riba.
Amedai kwenye nyumba ya Milembe alikuwa akiishi na mama mzazi wa Milembe, msichana wa kazi za nyumbani, kijana wa usafi na mpenzi wa Milembe aliyemtaja kwa jina moja la Kidola aliyekuwa akifika mara kwa mara Usagara, mkoani Mwanza.
Kuhusu kuhusishwa na tuhuma za mapenzi ya jinsia moja, Maunga alidai hazina ukweli na hajawahi kufanya hivyo.
Amedai kusikitishwa na taarifa hizo kwa kuwa mapenzi ya jinsia moja siyo tu kosa kisheria lakini hata kwa dini yake ni dhambi.
Mshtakiwa huyo amedai hahusiki na kifo cha Milembe na hakuwa na sababu ya kufanya hivyo.
Katika ushahidi huo, amedai kabla ya kukamatwa hakuwa akiwafahamu washtakiwa wengine, akieleza kwa mara ya kwanza alikutana nao mahakamani hapo.
Amedai baada ya msiba aliendelea kuishi nyumbani kwa Milembe hadi Mei Mosi, 2023 alipokuwa kwenye kikao kujadili mali za marehemu ndipo askari polisi waliingia na kumkamata.
“Walikuja askari kwenye magari mawili waliposhuka waliniweka chini ya ulinzi pamoja na ndugu yake Musa Fundikira, wakafanya upekuzi kwenye chumba cha Milembe na chumba nilichokuwa nalala mimi kisha kutupeleka Kituo cha Polisi Nyamagana,” amedai.
Shahidi huyo alidai awali alielezwa amekamatwa kwa kuficha fedha za marehemu (Milembe), lakini akiwa kituo cha polisi yalibadilishwa mashtaka na kuelezwa anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya Milembe na baadaye alisafirishwa hadi Geita.
Amedai Mei 5, 2023 alitolewa mahabusu ya polisi Geita na kupelekwa Bwalo la Polisi alipowakuta askari wanne waliomhoji kuhusu mauaji ya Milembe.
Mshtakiwa huyo amedai akiwa huko aliwapa taarifa ya maisha yake na kukana kuhusika na kifo cha Milembe.
Mshtakiwa alidai hakuwahi kuhojiwa Kituo cha Polisi Nyamagana na hakuwahi kuwasiliana na watuhumiwa wengine kama ilivyotolewa ushahidi mahakamani kwa kuwa alikuwa hawafahamu.
Maunga aliiomba Mahakama imuangalie kwa kuwa hajahusika, kushiriki wala kupanga mauaji hayo. Pia yeye ni mama wa watoto wawili wanaomtegemea.
Mshtakiwa wa pili, akiongozwa na wakili Laurent Bugoti alipoulizwa kama anafahamiana na mshtakiwa wa kwanza amedai hamfahamu.
Pia amedai hajawahi kuwasiliana naye, akisema kama ushahidi wa simu upo basi ulipaswa kuwasilishwa mahakamani.
Kuhusu hoja ya kumtafuta Musa Pastory na Genja Pastory baada ya kupanga njama za kumuua Milembe, alidai hawafahamu na hajawahi kuwasiliana nao.
Amedai kama upande wa Jamhuri una ushahidi, ulipaswa kuwasilishwa mahakamani.
Mshtakiwa amedai hahusiki na tukio la mauji na kuiomba Mahakama imwachie huru.
Kwa upande wake, mshtakiwa wa tatu, Genja Pastory akiongozwa na wakili Elizabeth Msechu, ameieleza mahakama kabla ya kukamatwa alikuwa akijihusisha na shughuli za uvuvi Sengerema, mkoani Mwanza.
Amedai Mei 5, 2023 baada ya kukamatwa akiwa saluni hakuelezwa chochote hadi alipofikishwa Kituo cha Polisi Nyakalilo alipoelezwa anahusishwa na kesi ya wizi wa mtego uliotokea mwaloni.
Mei 6, 2023 amedai alitolewa mahabusu ya Polisi Nyakalilo na kupelekwa Kituo cha Polisi Sengerema na kuhusishwa na mauji ya Milembe aliyekuwa hamfahamu wala hajawahi kumuona.
Alidai akiwa kituoni hapo alihojiwa kuhusu jina, umri na kabila na baada ya hapo alilazimishwa kuhusu mauaji ya Milembe alipokataa alipigwa na mpini kisha kufungwa pingu na kubinywa sehemu za siri na bisibisi kitendo kilichosababisha azimie.
“Nilipoamka nilikuta mezani kuna karatasi na kalamu wakanilazimisha nisaini niliwaambia sijui kuandika wakaniambia niweke saini kwa kidole gumba,” alidai Genja.
Kuhusu kwenda kuonyesha lilipo jambia lililotumika kumuua Milembe alidai Mei 7, 2023 asubuhi alitolewa mahabusu ya polisi Geita na kuambiwa apande gari na kuzungushwa sehemu mbalimbali, mwisho walifika eneo lenye nyasi nyingi na polisi walimtaka ashuke kupekua kwenye nyasi na kukuta jambia.
Alidai polisi walimhoji kama analifahamu alieleza kutolifahamu ndipo alipoambiwa alibebe na kurudi nalo kituo cha polisi.
Mshtakiwa pia amekana kutambuliwa kwenye gwaride la utambuzi kwa kuwa hakuwahi kufanyiwa gwaride hilo akiwa mahabusu.
Mshtakiwa pia alikana kufahamiana na washtakiwa wenzake na kudai kuwaona mara ya kwanza walipofikishwa mahakamani.
Alidai tuhuma kuwa alipata jeraha mkononi siyo za kweli na kwamba hata ushahidi uliotolewa mahakamani kuwa alichukuliwa alama za vidole siyo wa kweli.
Alipoulizwa na wakili wa Jamhuri, Merito Ukongoji kama kuna sababu zozote zilizowafanya shahidi wa 9, 7, na 3 wa upande wa mashtaka kumtaja kuwa yeye ndiye aliyewapeleka polisi kuwaonyesha walikotupa simu za marehemu alidai hajui.
Kuhusu kama yeye siyo aliyewaonyesha polisi lilikokuwa jambia lililotumika kumuua Milembe, kwa nini polisi wamtaje yeye na siyo mwingine wakati kuna washtakiwa wengine alidai hajui.
Mshtakiwa Musa Pastory, akiongozwa na wakili Erick Lutehanga alidai hana undugu wowote na Genja Pastory wala Safari Lubingo na kuwa kwenye mahojiano na askari mpelelezi yeye alitoa taarifa za jina umri na sehemu anayoishi.
Alidai hakuwahi kuwasiliana na washtakiwa wengine kwa kuwa tangu simu yake ipotee Desemba 25, 2022 hakuwahi kumiliki tena simu.
Mshtakiwa alidai licha ya kutowasiliana na washtakiwa wenzake, alikuwa hawafahamu na hakuwahi kuwaona kabla.
Alidai hakuwahi kutoa maelezo polisi na wala hakuwahi kuwataja washtakiwa wengine popote kwa kuwa alikuwa hawafahamu.
Shahidi huyo wa utetezi alidai hajawahi kuhusika na mauaji ya Milembe. Ameiomba Mahakama imuachie huru.
Baada ya washtakiwa kukamilisha utetezi wao, Jaji alisema hukumu itatolewa Julai 19, 2024 baada ya Mahakama kupitia ushahidi na vielelezo vilivyotolewa na pande zote.