Kaya 394,000 kuchomolewa orodha ya Tasaf

Iringa. Baada ya tathmini kuonyesha kaya 394,000 zimeweza kujimudu kiuchumi, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) unatarajia kuziondoa katika mpango huo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tasaf, Shadrack Mziray amesema Juni, 2024 utakuwa wa mwisho kwa kaya hizo kupokea fedha kutoka Tasaf, hivyo kuanza kujitegemea.

Akizungumza leo Juni 28, 2024 wakati wa ziara ya wadau wa maendeleo waliotembelea wanufaika wa Tasaf wilayani Kilolo, Mziray amesema wanufaika 900,000 nchi nzima ndio watakaobaki kwenye mpango huo.

“Lengo la Tasaf ni kuinua kipato cha mwananchi kutoka kwenye kipato cha chini, tathmini yetu imeonyesha zipo kaya ambazo tayari zimeweza kujitegemea,” amesema.

Amesema tafiti zinaonyesha asilimia 26 ya Watanzania ni masikini lakini asilimia nane wapo kwenye umasikini uliokithiri na hao ndio wanaotakiwa kuwepo kwenye mpango huo.

Amesema tangu kuanza kwa Tasaf II awamu ya pili, zaidi ya Sh1.3 trilioni zimetumika.

Mziray amesema mpaka Septemba 2025, fedha hizo zitafikia kati ya Sh1.8 trilioni mpaka Sh2 trilioni.

“Zaidi ya wadau wa maendeleo 13, wakiwamo Benki ya Dunia wanasaidia mpango huu na ndio hawa wamekuja kututembelea,” amesema Mziray.

Awali, baadhi ya wanufaika wa Tasaf kutoka Kijiji cha Ilindi, Kata ya Mahenge wilayani Kilolo walisema wapo tayari kuondoka baada ya hali zao kuimarika kiuchumi.

“Sikuwa hivi nilivyo, hata milo mitatu ilikuwa shida kumudu, nashukuru Mungu tangu mwaka 2015 nilipoanza kunufaika na Tasaf, nimejenga nyumba na nafuga bata na nguruwe. Nipo tayari kuondoka Tasaf,” amesema Emilia Kilave, mkazi wa Kijiji cha Ilole, wilayani Kilolo.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia (WB), Paulina Mloso aliwataka walengwa wa Tasaf kujifunza kuweka akiba na kuanzisha miradi ya kiuchumi ili wasibaki kwenye hali duni za maisha.

Ofisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Iringa, Saida Mgeni amesema kazi kubwa waliyonayo ni kuzipatia elimu kaya hizo ili fedha wanazopokea ziweze kuzalisha.

“Zipo kaya ambazo tayari zimefanikiwa na zipo tayari kuondoka kwenye mfuko huu kwa sababu zinaweza kujisimamia kiuchumi,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba amesema mafanikio ya Tasaf ni kuona kaya zilizokuwa kwenye umasikini uliokithiri zimepiga hatua kiuchumi.

Related Posts