Dar es Salaam. Wakati wapiga kura 197 wakitarajia kufanya uamuzi wa kikatiba kumchagua mwenyekiti mpya wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Kamati ya uchaguzi huo imesema pingamizi alilowekewa mmoja wa wagombea wa nafasi ya mwenyekiti, Shabani Haji Itutu halijafuata kanuni za chama.
Itutu aliwekewa pingamizi na wanachama saba wa ADC, Ibrahim Pogora, Asha Milongea, Asha Mzee, Khadija Tambwe, Maisala Khamis, Doni Mnyamani na Halima Msumali wakidai ni mwanachama wa chama kingine cha upinzani.
Katibu wa kamati ya uchaguzi, Innocent Siriwa ameiambia Mwananchi Digital leo Ijumaa, Juni 28, 2024 kwamba wamepokea pingamizi hilo, lakini kwa mujibu wa kanuni za chama, kamati haitalifanyia kazi.
“Kwanza limekuja nje ya muda wa mapingamizi uliowekwa, lakini pia kanuni za chama zinaelekeza mtu anayetakiwa kumwekea pingamizi mgombea ni mgombea mwingine, sio wanachama,” amesema Siriwa.
Akizungumzia mchakato wa uchaguzi huo utakaofanyika kesho Jumamosi, Siriwa amesema mkutano mkuu utaanza saa 2:00 asubuhi na wanatarajia mchakato wote hadi kupata viongozi wapya wa ADC kukamilika saa 10:30 jioni kwenye hoteli ya Lamada, Ilala jijini Dar es Salaam.
“Wapiga kura ni 197 kutoka Bara na Zanzibar, wataanza kwa kumchagua mwenyekiti (nafasi hiyo inawaniwa na Itutu aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti na Doyo Hassan Doyo aliyewahi kuwa katibu mkuu), mshindi atakabidhiwa madaraka na mwenyekiti anayemaliza muda wake (Hamad Rashid).
“Atakapokabidhiwa, mwenyekiti mpya ndiye ataendelea na mchakato wa kuwapata makamu mwenyekiti wa Bara na Zanzibar,” amesema Siriwa.
Wanaowania nafasi hiyo upande wa Bara ni Scola Kahana na Hassan Mvungi na Zanzibar ni Fatma Salehe na Shara Amrani huku pia kesho utafanyika uchaguzi wa nafasi 19 za wajumbe Bodi ya uongozi taifa.
Kwa mujibu wa Siriwa, nafasi hizi wagombea wake watachukua na kurudisha fomu siku hiyohiyo ya uchaguzi (kesho), watapigiwa kura siku hiyo ukumbini na kati ya watakaochaguliwa, robo au nusu ya idadi hiyo wanapaswa kutoka Zanzibar.
Kabla ya uchaguzi huo kesho, leo Ijumaa kuanzia saa moja usiku, Bodi ya Taifa ya uongozi ya ADC itakuwa na mkutano mkuu maalumu kupitisha ajenda za mkutano huo mkuu wa uchaguzi.
“Mkutano mkuu unatambuliwa na Bodi ya taifa ya uongozi, ambayo ndiyo itapitisha ajenda za mkutano mkuu wa kesho,” amesema Siriwa.
Kampeni za uchaguzi wa chama hicho zitakoma leo saa 12 jioni ambapo zitafungwa tayari kwa uchaguzi huo kesho, huku wagombea wakisisitizwa kufuata kanuni na taratibu za chama ambazo zimeelekeza kufanya kampeni za kukijenga na kugusa maisha ya wananchi.