“Kupitia cheti hiki cha ubora vipimo vinavyofanyika hapa Mloganzila majibu yake yanafanana na majibu kutoka maabara yoyote duniani, kwahiyo hii inadhihirisha namna ambavyo wataalam wetu wanafanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Shirika la Afya Duniani pamoja na ile ya Wizara ya Afya” ameongeza Prof. Janabi
Prof. Janabi ameongeza kuwa kufuatia ithibati hiyo Maabara ya Mloganzila itakuwa kituo cha mafunzo na utafiti, inaweza kupokea na kupima sampuli kutoka sehemu mbalimbali na kutoa majibu sahihi kwa wakati, kuaminika kwa ubora wa vipimo na majibu kimataifa. Hivyo sampuli ya vimelea vitakavyopimwa katika maabara hiyo vinaweza kutumiwa na mamlaka au taasisi yoyote duniani.
Aidha, Prof. Janabi amewataka wataalam hao wa maabara kuendelea kuchapa kazi kwa weledi ili kulinda ubora uliopo na kuifanya maabara hiyo kuendelea kuaminika nje na ndani ya Tanzania.
Kwa upande wake Afisa Ubora wa Maabara MNH-Mloganzila Lanja Kahemela amesema ukaguzi uliofanywa na SADCAS umezingatia mwongozo mpya wa ubora kutoka ule wa zamani (ISO15189:2012 kwenda ISO15189:2022) ambapo unasisitiza kumfikia mgonjwa ikiwemo kuangalia usalama wake zaidi.
Itakumbukwa kuwa Maabara ya Muhimbili Mloganzila ni miongoni mwa maabara kubwa nchini ambayo inapima zaidi ya vipimo 1000 kulingana na idadi ya wateja wanaofika kupata huduma za uchunguzi na matibabu.