Wanachama wa Chama cha Wastaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOTRA) wamefanya mkutano mkuu wa mwaka na kujadili ya Mpango Mkakati wa BOTRA wa miaka mitatu, 2025 hadi 2027.
Mpango Mkakati huo unalenga kuongeza idadi ya wanachama, kuongeza motisha kwa wanachama, kuendeleza uanachama hai, kupanua uwezo wa chama kimawasiliano kwa ajili ya kuwafikia kwa wakati wananchama na watarajiwa, kukuza uelewa wa wadau wakuu kuhusu chama na mchango wake kwa walengwa na jamii kwa ujumla, kuongeza kipato kwa chama na kudumisha utawala bora.
Akifungua mkutano huo Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utumishi na Uendeshaji Bw. Kennedy Nyoni amewashauri wastafu ambao bado hawajajiunga na wale wafanyakazi watakaostaafu kujiunga katika chama hicho kwa lengo la kushirikiana na kusaidiana kwa kuwa wanafahamiana kwa muda mrefu.
Aidha, amesema kwa wanachama kuungana na kuwa kitu kimoja wanaweza kutoa mchango wao wa kitaaluma ambao unaweza kuiwezesha Benki Kuu ya Tanzania kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Awali akitoa taarifa kwa mgeni rasmi Mwenyekiti wa Chama hicho Bi. Grace Lubambe amesema kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya vitendea kazi kama samani za ofisi, kompyuta, mashine ya kutolea kopi, intaneti (WiFi) na mawasiliano ya simu za mezani jambo ambalo mgeni rasmi ameahidi kulifanyia kazi na kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyiakazi.