Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaamimekiri kuwashikilia watu 17 wanaotuhumiwa kuwafanyia mitihani wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Mbali na watuhumiwa hao, limethibitisha kuwashikilia wanafunzi saba wanaodaiwa kuwa ndiyo waliokuwa wakifanyiwa mitihani hiyo, huku wengine 10 wakiendelea kusakwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Juni 28, 2024 na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Elifas Bisanda watuhumiwa walikamatwa kuanzia Juni 18, 2024 katika vituo vya Ilala na Kinondoni wakiwa na vitambulisho vya kughushi na tiketi ya ukumbi wa mitihani.
Akizungumza na Mwananchi, leo Juni 29, 2024 Kaimu Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, SACP Foka Dinya amesema watuhumiwa 17 wako chini ya ulinzi katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni.
“Wale waliokuwa wanafanyiwa kwa sababu walikuwa nje ya kituo cha mitihani tumewakamata saba na wengine 10 waliobakia jitihada za kuwatafuta zinaendelea ili wakamilike kulingana na idadi ya waliokuwa wanawafanyia mitihani,” amesema Kaimu Kamanda Dinya.
Amesema watuhumiwa hao 17 walighushi vitambulisho kuwawezesha kuingia kwenye chumba cha mtihani, akieleza vilikuwa na majina ya watahiniwa halisi.
“Mhadhiri mmoja alishtukia mfumo huo wa udanganyifu kufanyika ndipo walipoanza kufuatilia kwa sababu kuna picha za watahiniwa baada ya kuwachunguza hawa 17 walionekana si watahiniwa halisi, baada ya hapo walivijulisha vyombo vya dola na tukawakamata watuhumiwa hao,” amesema.
Kaimu Kamanda Dinya amesema baada ya kuwahoji watuhumiwa wamedai waliingia makubalino na wanafunzi kuwafanyia mitihani kila ‘Paper’ kwa gharama ya kati ya Sh30,000 hadi Sh50,000.
Alipoulizwa iwapo watuhumiwa wamepewa dhamana, Kaimu Kamanda Dinya amesema:
“Kuhusu dhamana siwezi kulizungumzia sana isipokuwa dhamana ni haki ya mtuhumiwa lakini kwa kuwa kuna Mkuu wa Upelelezi na anaendelea na uchunguzi akikamilisha kazi yake, dhamana itakuwa wazi kwa kuwa ni haki yao.”
Amesema nafasi ya dhamana itakuwa wazi hadi wajiridhishe kile wanachokitafuta kutoka kwa watuhumiwa hao kama vimepatikana kulingana na wanavyohitaji.
Profesa Bisanda jana Juni 28 alisema chuo hicho kilianza mitihani Juni 3 hadi 24, na wanafunzi 10,417 waliandika mitihani katika vituo 53, ambavyo vimesambaa nchi nzima.
“Katika kipindi cha wiki tatu za mitihani, kwa umakini wa mifumo yetu, wasimamizi wa mitihani waliwakamata mamluki wapatao 17, hususani katika vituo vya Ilala na Kinondoni, Dar es Salaam. Matukio mengi yalibainika kuanzia Juni 18,” alisema Profesa huyo.
Alisema kitendo cha watu hao kughushi vitambulisho vya chuo na tiketi ya ukumbi wa mitihani ni vitendo vya jinai, hivyo sheria ichukue mkondo wake.
Alisema waliokamatwa siyo wa chuo hicho, bali ni kutoka vyuo vingine na wengine ni wafanyakazi katika fani walizosomea.
Profesa Bisanda alisema chuo kina sheria na kanuni za mitihani ambazo zitatumika kuwashughulikia.
“Mamlaka za chuo zitawahoji wahusika na wakikutwa na hatia, basi wataadhibiwa kulingana na kanuni,” amesema.
Kwa waliofikishwa Polisi, amesema hataridhika kuambiwa wanaendelea na upelelezi, kwani maofisa wa Usalama wa Taifa walishuhudia matukio hayo hivyo hayahitaji upelelezi zaidi.
Alisema taarifa ataifikisha makao makuu ya Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi na Ofisi ya Rais kwa ajili ya ufuatiliaji.
Ili kukomesha vitendo vya namna hiyo, Profesa Bisanda alisema OUT ipo kwenye maandalizi ya kuwasajili wanafunzi wote kwa alama za vidole, na kumhakiki kila mtahiniwa kwa mashine maalumu za utambuzi wa alama za vidole katika vituo vyote vya mitihani.
Profesa Bisanda alisema OUT kimejijengea sifa kimataifa, kwa kuwa na mfumo madhubuti wa usalama wa mitihani.