Vifuu vya nazi kutengeneza mkaa

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha mkakati wa miaka 10 wa  matumizi ya nishati safi ya kupikia unatekelezwa kwa ufanisi wajasiriamali wamekuja na ubunifu utengenezaji wa mkaa mbadala kwa vifuu vya nazi.

Mkakati wa matumizi ya nishati safi ulizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Mei 8 mwaka huu, ukilenga kuepuka athari za matumizi ya kuni na mkaa.

Akizungumza na Mwananchi leo Juni 29, 2024  Mkurugenzi wa kampuni ya KP, Deogratius Kapalata, amesema ili kutunza mazingira na kuepukana na matumizi ya nishati chafu alitumia ujuzi aliopata kutoka Japan.

“Tunatakiwa kutumia ujuzi ambao tunapata kutoka kwa wengine, baada ya kupata ujuzi nchini Japan nilikuja na ubunifu wa kutengeneza mafuta ya nazi ambayo yalinipa ujuzi mwingine wa kutengeneza mkaa mbadala,”amesema Kapalata.

Amesema mkaa huo unasaidia kutunza mazingira kwa kutokata kuni na kuweza kuhifadhi mazingira hivyo amekuwa akitumia wapandaji minazi katika eneo la Mbezi Msakuzi na kupata mafanikio ya kusambaza tani tano hadi saba za mkaa huo kwa mwezi.

Amesema ubunifu huo umesaidia kuajiri vijana zaidi ya 11, ambao wanashughulika kwenye utengenezaji wa mkaa na wengine kwenye mafuta.

Akielezea unafuu wa mkaa huo, Witness Faustine amesema mkaa huo una uwezo wa kukaa saa nne bila kuzimika na unatumika kupikia vyakula mbalimbali kama unavyotumika katika mkaa mwingine.

Pia, amesema gharama za mkaa huo ni nafuu ambapo wanauza kwa kilo ambazo zinaanzia kilo moja kwa Sh 1,500 hadi kilo 10 ambayo ni Sh 11,000.

“Ubunifu huu umesaidia jamii kwa kiasi kikubwa kwa kuwa wananchi wameanza kuelewa umuhimu wa kutunza mazingira na hivyo kuwa kivutio katika ameneo mbalimbali ikiwemo eneo la Mbezi Luis,”amesema Witness.

Utengenezaji wa mkaa huo utasaidia usafishaji wa masoko ambayo yanauza nazi kwa kukusanya sehemu moja na kupeleka kwenye viwanda kwa ajili ya matumizi husika.

Related Posts