Chadema yakosoa bajeti ya Serikali kujikita katika matumizi ya kawaida

Dar es Salaam. Kutokuwepo kwa uwiano wa fedha za maendeleo na matumizi ya kawaida katika bajeti ya kila mwaka wa fedha ni moja ya sababu zilizotajwa kama kikwazo cha maendeleo ya kiuchumi nchini.

Kwa mujibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika bajeti za miaka takribani mitatu ya fedha, sehemu kubwa ya fedha zimetengwa kwa matumizi ya kawaida kuliko matumizi ya maendeleo.

Kauli ya Chadema, imetolewa zikiwa zimepita siku mbili tangu wabunge wapige kura kupitisha bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/25 ya Sh49.34 trilioni.

Katika bajeti hiyo, Sh35.59 trilioni ambazo ni zaidi ya asilimia 70 zimepangwa kutumika kwa matumizi ya kawaida, huku Sh15.75 trilioni zimepangwa kutumika kwa maendeleo.

Chadema kupitia Bunge lake la Wananchi imesema ni vigumu kufikia maendeleo kama bajeti inayotengwa kwa ajili ya eneo hilo ni ndogo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumamosi, Juni 29, 2024, mbunge wa zamani aliyetokana na chama hicho, Suzan Lyimo akiongoza kikao cha uchambuzi wa bajeti ya Serikali amesema maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania yanakwazwa na mipango ya kibajeti iliyojikita katika matumizi ya kawaida badala ya maendeleo.

“Ili nchi ifanikiwe bajeti ya maendeleo inapaswa ama ilingane na fedha za matumizi ya kawaida au ya maendeleo izidi bajeti za matumizi mengine,” amesema.

Amechambua bajeti za miaka mitatu iliyopita akisema, mwaka wa fedha 2023/24 matumizi ya kawaida yalikuwa Sh30.31 trilioni, huku ya maendeleo yakiwa Sh14.08 trilioni.

Amesema katika bajeti ya mwaka 2021/22 asilimia 62 yalikuwa matumizi ya kawaida na asilimia 38 ndiyo ya maendeleo.

Mwanasiasa huyo amesema katika bajeti ya mwaka 2022/23 asilimia 66 ilitengwa kwa matumizi ya kawaida na asilimia 34 kwa ajili ya maendeleo.

Katika uchambuzi huo, Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Catherine Ruge amependekeza bajeti itakayotengwa iakisi maisha ya wananchi.

Amesema ni vyema kuwapo mfumo wa utawala unaoshirikisha wananchi, hasa kwenye maeneo ya bajeti.

“Mfumo wa bajeti uwe unajibu maswali kwa ufanisi yanayowahusu wananchi na uchumi wao na muhimu kuwapo mfumo wa ugatuzi wa kiuchumi unaoendana na ugatuzi wa madaraka,” amesema.

Amesema Serikali imekuwa na matumizi mabaya, akihoji inawezekanaje inanunua magari ya Sh850 bilioni ilhali mwaka jana ilinunua ya zaidi ya Sh500 bilioni.

Askofu Maxmillian Kadutu amegusia ongezeko la mikopo akisema inachochea mzigo wa ugumu wa maisha kwa wananchi.

Ongezeko la deni hilo kutoka Sh60 trilioni hadi Sh91 trilioni mwaka huu, amesema ni kubwa zaidi kuwahi kutokea tangu awamu zote za Serikali.

“Pengine wananchi hawataelewa namna wanavyolipa, lakini kimsingi wanalipa kupitia kodi na tozo zinazowekwa. Kwa mtindo huu, hali ya maisha ya wananchi itaendelea kuwa ngumu,” amesema.

Kwa upande wa Devotha Minja amekazia suala la fedha nyingi kutengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida akisema ni changamoto kwa maeneo ya uchumi.

“Pamoja na bajeti hii kuangalia zaidi makusanyo ya kutumia nguvu na kumuumiza Mtanzania, Waziri (Dk Mwigulu Nchemba) juzi kasema ifike wakati mtu asipotoa risiti, faini iwe Sh15 milioni,” amesema.

Amesema mambo hayo ndiyo yanayofanya ufanyaji biashara nchini uwe changamoto.

Hata hivyo, Serikali imeondoa ukomo wa faini ya juu ya kosa la kutotoa risiti za kielektroniki (EFD) ya Sh15 milioni na badala yake kuweka Sh4 milioni.

Amependekeza kodi katika bidhaa zitozwe viwandani ili zikifika kwa mlaji zisitozwe ushuru wowote na kuwaumiza wananchi.

Kuhusu sukari, amependekeza viwanda vya bidhaa hiyo viwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara badala ya Wizara ya Kilimo.

Pendekezo lake lingine ni bajeti inayotengwa iendane na uhalisia na matumizi yasiyo ya lazima yapunguzwe.

Ameeleza hakuna sababu ya Rais kukopa zaidi ya Sh10 bilioni ilhali nchi ina rasilimali lukuki zinazopaswa kutumika.

Related Posts