Tanzania yaiuzia Zambia mahindi tani 650,000

Dar es Salaam. Kutokana na ukame unaoikumba nchi ya Zambia, nchi hiyo imeingia makubaliano na Tanzania kununua tani 650,000 za mahindi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi milioni saba wa taifa hilo.

Mkataba huo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi nane na utaiingizia Tanzania dola milioni 250 sawa na Sh650 bilioni.

Mahindi hayo yatakayosafirishwa kwenda Zambia yatatolewa katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ambapo kwa kituo cha Songwe mahindi tani 55,000, Makambako tani 75,000, Sumbawanga tani 250,000 na Songea tani 270,000.

Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NFRA Dk Andrew Komba pamoja na Mratibu wa Maafa kitaifa  nchini Zambia Dk Gabriel Pollen, wakishuhudiwa na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Kilimo Zambia Reuben Phiri.

Waziri Bashe akizungumzia mkataba huo leo Juni 29,2024, ameitaka NFRA kuutekeleza kwa wakati na kuhakikisha Zambia haikosi mahindi, akisisitiza makubaliano hayo hayaifungi sekta binafsi kuiuzia Zambia mahindi bali wanapaswa kufuata utaratibu.

“Wafanyabiashara wote wafuate utaratibu ili kupeleka mahindi yenye ubora Zambia na nihakikishie Serikali ya Zambia kuwa mahindi yetu ni salama na hayahusiani na mbegu zilizobadilishwa vinasaba (GMO)”amesema.

Bashe amesema mkataba huo Serikali itausimamia kikamilifu kukabiliana na urasimu wakati wa usafirishaji akibainisha kuwa hiyo ni biashara kubwa.

Katika hatua nyingine Bashe ameitaka NFRA kuanza kufungua masoko ya kununua mahindi  kuanzia Julai 10 kwani Serikali haitaki mkulima kupata hasara .

Naye Waziri wa Kilimo Zambia,  Reuben Phiri amesema mahindi hayo yatakwenda kuwasaidia wananchi milioni saba walioathiriwa na ukame ambao umeikumba nchi hiyo .

“Zambia imekumbwa na majanga mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa Uviko-19, kipindupindu na sasa ukame ambao si tu umeathiri binadamu bali hata wanyama na hata vyanzo vya maji. Mkataba huu kwetu utakwenda kuimarisha ushirikiano baina yetu ambao uliasisiwa na viongozi wa mataifa yetu,”amesema.

Kwa upande wake , Dk Pollen amesema kutokana na ukame zaidi ya hekari milioni moja za mazao ziliathirika na mabadiliko hayo ya hali ya tabianchi na hivyo Serikali ya Zambia imechukua hatua ya kuwasaidia wananchi wake kukabiliana na ukame kwa kiwapatia chakula.

Naye Dk Komba wa NFRA amesema usambazaji wa mahindi hayo nchini Zambia, utazingatia viwango vyote vya kiafya.

“Mahindi yanakayopelekwa Zambia ni salama na yamekidhi viwango vyote vinavyohitajika na mataifa haya mawili, tumeshirikisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS), tumejipanga kuhakikisha mkataba huu unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa,”amesema.

Pia kwenye mkutano huo,Waziri wa Fedha Dk Mwigulu amesema mwelekeo wa Tanzania kwenye kilimo ni kutotegemea mvua badala yake kulima kilimo cha kisasa kupata hifadhi kubwa ya chakula kuwalisha wananchi wake na hata mataifa ya Afrika Mashariki.

Utekelezaji wa mkataba huo ni kufuatia ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Zambia,  ambapo viongozi wa nchi hizo mbili walijadili kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo.

Related Posts