Machungu ya vivuko boti zikitumika, nane zakamatwa

Dar es Salaam. Makali ya upungufu wa vivuko kati ya Magogoni na Kivukoni yanaendelea kuwatesa wananchi ambao licha ya kuonywa na mamlaka, wameendelea kuvushwa na boti zinazohatarisha usalama wao. 

Taarifa ya Kikosi cha Polisi Wanamaji iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, inathibitisha adha wanayopitia wananchi hao kutokana na kutofanya kazi kwa vivuko vya Mv Magogoni na Mv Kigamboni ambavyo kwa sasa vipo kwenye matengenezo.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji, ACP Moshi Sokoro ilisema ufuatiliaji maalumu uliofanywa na Jeshi hilo kuanzia Mei hadi Juni, 2024 katika kudhibiti uhalifu ukanda wa Bahari ya Hindi uliwezesha kukamatwa ‘faiba’ boti nane zisizo na usajili wala majina zikijihusisha na usafirishaji wa abiria kwa njia hatarishi kati ya fukwe ya Kigamboni na soko la Samaki Feri.

Jeshi hilo pia limewaonya wamiliki wa boti na manahodha wanaobeba abiria kwa boti zisizo salama maeneo ya Kigamboni na Magogoni likisema halitasita kuchukua hatua kwa wote wanaojihusisha na uhalifu huo.

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), ulitangaza kukipeleka katika matengenezo makubwa kivuko cha Mv Kigamboni.

Mbali ya hicho kivuko cha Mv Magogoni kipo kwenye matengenezo makubwa Mombasa, Kenya tangu Februari mwaka jana.

Gazeti la Mwananchi hivi karibuni lilichapisha mfululizo wa ripoti maalumu kuhusu kucheleweshwa kwa matengenezo ya baadhi ya vivuko vinavyoendeshwa na wakala huo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kivuko cha Mv Kigamboni kilipaswa kupelekwa kwenye matengenezo makubwa mwanzoni mwa mwaka 2023, lakini kilipitiliza muda huo bila hilo kufanyika.

Juni 6, 2024 kupitia kitengo chake cha Masoko na Uhusiano, Temesa ilitangaza kusitisha huduma za kivuko hicho kuanzia Juni 7, ikieleza kinakwenda kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Hata hivyo, taarifa ya Temesa haikuweka wazi kwamba ni lini hasa kivuko hicho kitapelekwa kwenye matengenezo, wapi na lini kitarejea kuendelea na huduma.

Katika taarifa hiyo, Temesa iliweka wazi huduma za uvushaji abiria katika eneo la Magogoni-Kivukoni, zitaendelea kutolewa na Kivuko cha Mv Kazi na Sea Tax.

Kwa mujibu wa mkataba kati ya Temesa na Kampuni ya Azam Marine Ltd inayomiliki vivuko vya Sea Tax, vinapaswa kufanya kazi kwa saa nane.

Wenye magari walitakiwa kutumia njia mbadala kupitia Daraja la Mwalimu Nyerere ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na Mv Kigamboni kutokuwepo.

“Shughuli za uvushaji katika eneo hilo, zitaendelea kutolewa kama kawaida kwa kutumia kivuko cha Mv Kazi na Sea Tax,” ilieleza taarifa hiyo.

Licha ya kuendelea kufanya kazi, kivuko cha Mv Kazi kina uwezo mdogo wa kubeba abiria 800 na magari madogo 12 pekee, hivyo kushindwa kuhudumia mahitaji makubwa ya wananchi yaliyopo ambayo ni takriban abiria 60,000 kwa siku.

Ingawa haikueleza wazi, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra),  ilitangaza ruti mpya za daladala kutoka Kigamboni kwenda katikati ya jiji ikihusisha Kigamboni – Stesheni, Kigamboni – Mnazi Mmoja na Kigamboni Muhimbili.

Latra katika tangazo la ruti hizo lililotolewa Juni 21, 2024 kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram wa mamlaka hiyo ilieleza daladala zinazotakiwa kuingia barabarani katika ruti hizo ni 20 kwa kila njia, huku vigezo vikiwa kuwa na uwezo wa kubeba abiria kuanzia 25.

Ruti hizo zilitangazwa zikiwa zimepita wiki mbili tangu Temesa kukisimamisha kazi kivuko cha Mv Kigamboni.

Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Latra, Salum Pazi, aliliamboa Mwananchi kuwa uamuzi huo hauna uhusiano na kuharibika kwa vivuko isipokuwa kumekuwepo na ongezeko la mahitaji ya wananchi la usafiri katika njia hizo.

“Kazi yetu ni kuwafanya wananchi kupata huduma ya usafiri kwa wepesi na katika njia hizo hakukuwa na daladala jambo lililofanya bajaji kutumia kama fursa wakati wakijua wao ni usafiri wa kukodi na sio kutoa huduma kama wanavyofanya sasa

“Hivyo mbali ya kuwasogezea huduma wananchi lakini pia tunataka kuondoa tabia ya bajaji kujigeuza daladala kusafirisha watu kama ndio usafiri wa umma, huku ikiwatoza bei kubwa wananchi,” alisema Pazi.

Related Posts