Dabo hataki kurudia makosa msimu ujao

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amefunguka hataki kurudia makosa ya msimu uliopita katika michuano ya kimataifa na kusema ndio sababu iliyomfanya awaite mapema kambini mastaa wa timu hiyo ili kutengeneza muunganiko baada ya sajili mpya na kuiweka timu freshi kabla ya kuliamsha 2024-2025.

Msimu uliopita Azam licha ya kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga, ilitolewa mapema katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kutokana kikosi kukosa muunganiko wa mastaa waliosajiliwa kipindi hicho akiwamo Feisal Salum ‘Fei Toto’, Yannick Bangala na wengineo.

Kwa sasa klabu hiyo tayari imeshanasa wachezaji watano wapya ambao ni; Yoro Mamadou Diaby (Yeleen Olympique), Franck Tiesse (Stade Malien FC), Ever Meza (Leonnes FC), Jhonier Blanco (Aguilas Doradas), Adam Adam (Mashujaa FC) sambamba na kutema pia nyota watano waliokuwapo katika kikosi cha msimu uliopita.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dabo alisema licha ya kuwa bora msimu uliopita, bado wanahitaji kujenga timu imara zaidi ambayo wachezaji watakuwa tayari wamejenga muunganiko mzuri kutokana na maingizo mapya.

“Maandalizi ya msimu mpya yana faida kubwa mkiungana pamoja mapema kwani yanachangia wachezaji wapya kuingia kwenye mfumo haraka kabla ya michuano ya ushindani,” alisema Dabo na kuongeza;

“Mpango wetu ni kuingia mapema ili kujiweka sawa, tukipata nafasi ya kucheza mechi za kirafiki na kutengeneza uwiano sawa wa utimamu wa wachezaji bila kujali nani katumika sana au nani alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.”

Dabo pia alitaja michuano ya Ligi ya Mabingwa ambayo wanatarajia kuishiriki msimu ujao kuwa ni moja ya sababu ya wao kukutana pamoja mapema kwani wanatamani kuona wanafika hatua nzuri na sio kuondolewa hatua za awali.

“Tuna michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho (FA) na Mapinduzi hivyo tunahitaji kujiandaa vizuri ili kuweza kujiweka kwenye mazingira mazuri ya ushindani,” alisema Dabo na kuongeza;

“Ubora tuliouonyesha msimu uliopita tunatamani kuona tunaendelea tulipoishia tena kwa ubora zaidi kwani ongezeko la wachezaji wapya naamini litaongeza chachu ya mafanikio.”

Dabo alibainisha kufurahishwa na uongozi kufanya uamuzi wa kusajili washambuliaji wengine ili kuifanya timu yao kuwa bora kila eneo, huku akimtaja Fei Toto kuwa bado anamuona akitupia zaidi kutoka ana kuwa na jicho la kuona goli.

Azam inatarajiwa kuanza kujumuika pamoja kuanzia kesho Jumatatu tayari kujiweka sawa na msimu mpya kuanzia Julai 6 itakapoenda Zanzibar itakakokaa hadi Julai 13 na siku inayofuata itarudi Dar es Salaam ili kujiandaa na safari ya kwenda Morocco kwa kambi ya maandalizi ya msimu mpya.

Mara baada ya kurejea nchini mapema Agosti, Azam itakuwa na kibarua kwa ajili ya mechi za Ngao ya Jamii zitakazopigwa kati ya Agosti 8-11 ikishirikisha watetezi Simba, Yanga na Coastal Union.

Related Posts