Uthubutu na ujasiri kwa vijana kubuni miradi yenye tija, kwa ajili ya uwekezaji wa ndani, imeelezwa ni jibu sahihi kwa kundi hilo kumaliza tatizo la ajira nchini na kuchochea maendeleo endelevu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema hayo kwenye hafla ya ufunguzi wa kituo kipya cha mafuta, kampuni ya BUTL, chini ya kijana mzalendo, aliyedhamiria kuwekeza sehemu mbalimbali hapa nchini, huku akipata uungwaji mkono kutoka benki ya KCB Tanzania.
“Hauwezi kuvutia wawekezaji kama huduma hakuna na huduma mojawapo ni hii ya kuhakikisha kuna mafuta ya kutosha kuendesha magari na mitambo mbalimbali, hii inatupa nguvu ya kuita wawezaji wengi zaidi kuja kuwekeza hapa Singida,” alisema.
Meneja Masoko wa KCB Bank, Cledo Michael alieleza namna benki hiyo inavyowawezesha watanzania kufanikisha malengo ikiwamo uwekezaji wenye tija kwa maendeleo ya taifa kupitia ufadhili wa miradi ya kimkakati.
“Benki ya KCB ni mdau muhimu wa kibiashara na tunawezesha watanzania kufanikisha ndoto na malengo yao kupitia ufadhili na huduma za malipo kidigitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma,” alisema.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa BUTL Oil, Steven Marwa alieleza nia ya kampuni hiyo katika kuendeleza uwekezaji na kufungua fursa za ajira kwa watanzania wengi zaidi kupitia ajira mbalimbali.
Kituo cha mafuta BUTL kinaelezwa kuwa cha kwanza kwa ukubwa mkoani Singida, kutokana na uwezo wa kuhudumia magari manane kwa mara moja, huku kikiwa na uwezo wa kuhifadhi akiba ya mafuta ya petrol lita 66,800 na diseli lita 71,200.
1. Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego akishiriki tukio la uzinduzi wa kituo cha mafuta cha kampuni ya BUTL Oil kilichopo Singida mjini.Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya BUTL Oil, Steven Marwa. Kituo hicho kipya kitasaidia katika kuchochea Uchumi pamoja na kutoa ajira kwa vijana mkoani humo.
1. Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego akisalimiana na Meneja Masoko wa Benki ya KCB Tanzania, Cledo Michael wakati akiwasili kuzindua kituo kipya cha mafuta cha BUTL Oil kilichopo mkoani Singida mjini.Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya BUTL Oil, Steven Marwa. Kituo hicho kipya kitasaidia katika kuchochea Uchumi pamoja na kutoa ajira kwa vijana mkoani humo.