MASTAA wa Simba wanaanza kujumuika pamoja kuanzia kesho Jumatatu, lakini utamu zaidi ni dili la mrithi wa beki wa kati aliyetimkia FAR Rabat ya Morocco, Henock Inonga limefikia pazuri baada ya menejimenti ya mchezaji huyo kutua Dar es Salaam ili kukutana na Mohamed ‘Mo’ Dewji kumaliza kazi.
Simba inampigia hesabu Nathan Fasika Idumba anayechezea kwa mkopo Varelenga ya Norway akitokea Cape Town City ya Afrika Kusini na tayari manejimenti inayomsimamia imeshatua mjini ili kuzungumza na Mo Dewji kuwekana mambo sawa, baada ya awali mmoja wa vigogo wa Simba aliyewafuata DR Congo kuchemsha kupata muafaka.
Inaelezwa awali, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alipewa kazi ya kushughulikia dili la mchezaji huyo mwenye asili ya DR Congo, lakini safari zake za nchini humo na baadaye Afrika Kusini ilikwama na manejimenti ya mchezaji huyo imeona isiwe tabu ije Dar es Salaam kujua moja.
Chanzo cha kuaminika kutoka kambi ya mchezaji huyo, inasema Meneja wa Idumba ametua baada ya kupigiwa simu na Mo Dewji ili kuwekana sawa na inaelezwa walitarajiwa kuonana jana kabla ya dili kufikia mwishoni kwa beki huyo wa kati kuja kuchukua nafasi ya Inonga.
“Mohamed Dewji ndiye aliyemuita meneja huyo wa Idumba ili waje kuzungumza na tayari wameshatua na wikiendi hii (jana) wataonana kuwekana sawa. Mchezaji anataka kuichezea Simba, lakini kuna mambo hayakupata muafaka walipozungumza na Try Again,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti mmoja wa watu wa karibu na menejimenti ya mchezaji huyo alipoulizwa juu ya ujio wao hapa mjini, alisema wamekatazwa kuzungumza lolote kwa sasa hadi watakapomalizana na Simba, lakini chanzo chetu kingine kutoka Simba kinasema;
“Wanachopambana sasa ni mchezaji huyo kwenda Simba kwani ni miongoni mwa timu bora zinazoshiriki michuano ya kimataifa na kwa namna wanavyoendelea kuzungumza huenda wakamalizana vyema. Uamuzi wa mwisho utapatikana baada ya meneja kuonana na bosi mkubwa kwani kwake ndio kuna majibu ndio maana walimuita ili wazungumze.”
Kwa sasa beki huyo mwenye umri wa miaka 25 yupo Uarabuni baada ya kutoka Afrika Kusini akisubiria dili hilo kama litafanikiwa ili aibukie kambini Misri.