Usajili mpya…Gamondi atoa neno Yanga SC

WAKATI mabosi wa Yanga wakiendelea na mchakato wa kuboresha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano, kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amechekelea na kutoa neno kwa mambo yanavyokwenda klabuni hadi sasa katika ishu za usajili mpya.

Yanga ambayo inafanya mambo yake kimya kimya na kesho Jumatatu itaanza kuweka hadharani wachezaji ilioachana nao na wale inaowasajili kwa ajili ya msimu mpya na kocha Gamondi amekiri mambo yanaenda sawa na kuzidi kumpa mzuka kabla ya kwenda kambini kujiandaa na vita mpya ya 2024-2025.

Akizungumza na Mwanaspoti Gamondi amesema siku za mapumziko zimefikia tamati, lakini ndani yake alikuwa anajipanga na hesabu za msimu mpya sambamba na kufuatilia ripoti ya maboresho kwenye usajili wa dirisha kubwa.

Gamondi alisema hadi sasa kwa ripoti anayoipata amefurahishwa na namna viongozi wake wanavyoendelea kufanyia kazi ripoti yake.

Ingawa hakutaka kutaja majina, Gamondi alisema mastaa ambao amejulishwa wameshamalizana na timu hiyo wataiongezea nguvu kubwa timu yao.

“Tuko katika siku za mwisho za mapumziko, unajua unapumzika lakini pia kuna ratiba chache za msimu ujao inabidi ziendelee, hata zile ratiba binafsi,” alisema Gamondi aliyeiwezesha Yanga kutetea mataji mawili kati ya matatu iliyokuwa inayashikilia.

“Nafurahia ripoti ambayo naipata kwa viongozi wangu, nadhani wachezaji watakaongezeka ni watu wenye viwango vikubwa tunatarajia makubwa watakapounganika na hawa watakaobaki, “ aliongeza Gamondi.

Aidha, Gamondi ambaye ameirudisha Yanga kucheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika alisema mastaa hao wanatarajiwa kufanya makubwa ndani ya kikosi chao.

Kocha huyo raia wa Argentina alisema anaamini msimu ujao utakuwa mgumu ambapo watahitaji kujituma kwa kiwango kikubwa kwa kuwa kila timu itajipanga kuzuia kiwango chao.

“Naona taarifa nyingi huko, ukweli ni kwamba kila timu inajipanga kuhakikisha inakuwa tofauti, hizo pia ni hesabu zetu, msisahau Ligi itakuwa ngumu sana, tunatakiwa kuwa na nguvu kubwa kuliko msimu uliokwisha.

Yanga inatajwa kumalizana na mastaa wanne kipa Abubakar Khomeny, beki Chadrack Boka, kiungo Clatous Chama na mshambuliaji Prince Dube, huku ikitajwa kuwawinda washambuliaji wengine Jonathan Sowah na George Mpole sambamba na kiungo Adolf Mutasingwa.

hatimaye  sakata la mshambuliaji Prince Dube limemalizika rasmi baada ya klabu ya Azam kuthibitisha kwamba imemuachia Mzimbabwe huyo na sasa safari ya kwenda Yanga imebarikiwa.

Mwanaspoti tuliwajulisha mapema wiki hii kwamba Dube dili lake la kutua Yanga limekamilika baada ya kulipwa fedha alizokuwa akitakiwa kuilipa Azam klabu aliyokuwa akiichezea tangu mwaka 2020 lakini akaanzisha mgomo wa ghafla mwishoni mwa mwaka jana na kuzua sintofahamu.

Taarifa iliyotolewa na Azam juzi usiku ni kwamba klabu hiyo imeridhia maombi ya Dube kuvunja mkataba wake aliyowasilisha kwa uongozi wa klabu hiyo Machi 2024.

Azam imeweka wazi, kwamba mshambuliaji huyo ametimiza matakwa ya kimkataba kama ambavyo imeanishwa kwenye vipengele vinavyoruhusu upande mmoja kuvunja mkataba.

Inaelezwa kuwa Dube ameilipa Azam FC zaidi ya Sh 540 milioni ili kuvunja mkataba wake huo na klabu hiyo iliyomleta nchini mwaka 2020 akitokea Zimbabwe. Awali klabu ilitaka ilipwe Dola 300,000 (zaidi ya Sh 700 milioni) ili imuachie, huku mchezaji akisisitiza angelipa pesa ya usajili wake yaani Dola 250,000.

Awali, uamuzi huo ulizusha wasiwasi baada ya Azam kuonyesha kwamba bado haijapokea malipo hayo kabla ya baadaye kuthibitisha kupokea.

Uamuzi huo wa Azam, utamfanya sasa Dube kusalia na njia nyeupe ya kwenda kujiunga na Yanga ambayo Mwanaspoti linafahamu kuwa ndio klabu anayotaka kuitumikia hapa nchini.

Dube tayari alishamalizana na Yanga akisaini mkataba wa miaka mitatu na mabingwa hao wa Tanzania ambao ataanza kuwatumikia.

Kwa misimu minne aliyoichezea Azam, Dube ameifungia jumla ya mabao 33 ya Ligi Kuu Bara, mbali na mengine ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), Kombe la Mapinduzi na michuano ya kimataifa.

Msimu wa kwanza nyota huyo wa zamani wa Highlanders ya Zimbabwe alifunga mabao 14, kisha akaumia na kukaa nje na aliporejea msimu wa 2021-2022 alifunga bao moja, wakati msimu wa tatu alifunga mabao 11 na uliomalizika hivi karibuni akiitumikia kwa nusu msimu alifunga saba.

Related Posts