Kocha mpya Simba mambo freshi ni suala la muda tu

HUKO Msimbazi mambo ni moto, kwani baada ya kuanza kutambulisha vifaa vipya ikianza na Lameck Lawi kutoka Coastal Union, kwa sasa inajiandaa kumtangaza kocha mpya na mashine nyingine mpya zitakazoingia kambini kuanzia kesho Jumatatu.

Simba inataka kutambulisha benchi la ufundi ili kuanza kambi ikiwa kamili kwa ajili ya msimu ujao, huku Msauzi, Steve Khompela akitajwa.

Simba iliyomaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu msimu uliomalizika hivi karibuni na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika, mbali na Lawi pia ilitangaza kuwaongezea mikataba, Mzamiru Yasin, Israel Mwenda na Kibu Denis, huku ikiwapa ‘Thank You’ nyota sita wa kikosi hicho akiwamo Saido Ntibazonkiza, Luis Miquissone, John Bocco, Kennedy Juma, Shabaan Chilunda na Henock Inonga aliyeuzwa.

Baada ya zoezi hilo inaelezwa jambo linalofuata ni kutangazwa watu wa benchi la ufundi kabla ya timu kukutana kesho Jumatatu kujiandaa na safari ya kwenda kambi ya pre season huko Misri.

Moja ya vigogo wa Simba aliliambia Mwanaspoti, wamemalizana na wachezaji watatu, huku wengine wawili wakiwa hatua za mwisho ila wamegeukia kwa makocha ambapo Msauzi Steve Khompela bado anapewa nafasi kubwa ya kutambulishwa.

“Ndio tumeanza, usitarajie tutasimama bila kumaliza. Taratibu za kutambulisha wachezaji wapya zitaendelea, lakini wakati huo huo tutendelea kutoa Thank You kwa tutakaoachana nao,” alisema moja ya viongozi wa Simba na kuongeza;

“Lawi ni utambulisho wa kimkakati na nikuambie tu huo ni mwanzo, mambo makubwa yanakuja kwani tutatambulisha bechi la ufundi lenye mabadiliko pamoja na wachezaji wengine wanaokuja kurejesha heshima yetu.”

Kigogo huyo alipoulizwa uwezekano wa Khompela kuwa kocha mpya wa Simba kwa msimu ujao alijibu;

“Nimeona mmemuandika. Ila kwa kuwa tuna vyanzo vyetu vya kutoa taarifa zetu rasmi basi msubiri mtaona huko,” alijibu.

Mwanaspoti linajua Simba na Khompela wamefikia pazuri katika mazungumzo, lakini kocha huyo alipewa masharti ambayo kama atayatimiza ni wazi atawanoa wakali hao wa Msimbazi msimu ujao.

Miongoni mwa masharti aliyopewa Khompela ni kutozungumza na chombo chochote cha habari, juu ya ujio wake hadi pale atakapotambulishwa, pia alitakiwa apendekeze watu wawili hadi watatu, atakaofanya nao kazi kwa karibu akiwemo kocha wa makipa na wa viungo.

Simba iliachana na Mhispania Dani Cadena aliyekuwa akiwanoa makipa, pia haina kocha wa viungo tangu kuondoka kwa Mualgeria Kamal Boudjenane.

Mabadiliko mengine ya benchi ni upande wa meneja, kwani haina mpango wa kuendelea na Mkenya Mikael Igendia na sasa inatajwa huenda Patrick Rweyemamu akarejeshwa katika nafasi hiyo aliyoitumikia kwa muda mrefu.

Ukiachana na mabadiliko ya benchi la ufundi, lililokuwa chini ya Juma Mgunda aliyemaliza mkataba, Simba ipo mbioni kumtambulisha kiungo Joshua Mutale kutokea Power Dynamos ya Zambia,  ikielezwa imemalizana na mshambuliaji Mganda, Steven Mukwala kutoka Asante Kotoko ya Ghana.

Related Posts