TETESI ZA USAJILI: Duke Abuya katika rada za Wagosi, simba…

WAGOSI wa Kaya wapo bize na maandalizi ya msimu ujao wa mashindano, hususani Kombe la Shirikisho Afrika na kwa sasa imeanza mazungumzo na kiungo mshambuliaji Mkenya, Duke Abuya anayekipiga Singida Black Stars (zamani Ihefu).

Nyota huyo inaelezwa huenda akaondoka kikosini humo baada ya mkataba aliokuwa nao Ihefu kumalizika, huku kukiwa hakuna mazungumzo mapya ya kumuongezea, japo timu ya Polisi Kenya aliyokuwa akiichezea kabla ya kuja nchini, inatajwa kutaka kumrejesha, huku uwepo wa kocha David Ouma ulitajwa chanzo cha kumvuta Coastal Union hasa kama mazungumzo baina yao yatamalizika freshi.

MABOSI wa Simba wako katika mazungumzo ya kuipata saini ya kiungo mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Jean Charles Ohoua. Nyota huyo anayekipiga Stella Adjame ya Ivory Coast, inaelezwa ndiye mrithi wa Clatous Chama anayedaiwa kwenda Yanga, huku msimu uliopita akiwa ni Mchezaji Bora (MVP) akifunga mabao 12 na kuasisti mabao mengine tisa.

KIUNGO mkabaji wa Simba Queens, Koku Kipanga ambaye anamaliza mkataba na klabu yake hiyo ya Msimbazi, anahusishwa na Ceasiaa Queens ya Iringa. 
Kwa sasa mchezaji huyo yuko huru baada ya kumaliza mkataba na Wekundu hao na kama mambo yatakwenda sawa atasaini mkataba na Ceasiaa.

TIMU ya Hearts of Oak imeanza kuisaka saini ya kiungo mshambuliaji wa Yanga, Augustine Okrah anayeelezwa anaondoka ndani ya kikosi hicho cha Jangwani. Nyota huyo wa zamani wa Simba alijiunga na Yanga Januari mwaka huu akitokea Bechem United inayotajwa inakabana koo na Oak ikitaka kumrejesha kikosini.

PAMBA Jiji inadaiwa imeanza mazungumzo beki wa kati wa Tusker ya Kenya, Michael Kibwage ili atue kikosini hapo kwa msimu ujao wa mashindano. Nyota huyo (26), anawindwa na timu hiyo iliyopanda daraja, huku klabu za Sofapaka, KCB Nairobi na AFC Leopards zote za Kenya nazo zikitajwa kumnyemelea.  

TIMU za Geita Gold, Pamba Jiji, KenGold na Fountain Gate FC zinaiwinda saini ya mshambuliaji, Andrew Raymond Chamungu aliyetamba Ligi ya Championship akiwa na FGA Talents. Nyota huyo yuko huru baada ya kumalizana na FGA Talents aliyoichezea msimu uliopita akiifungia mabao 10 na kuasisti matano katika michezo 25. 

UONGOZI wa Pamba unadaiwa unazungumza na mshambuliaji wa Tabora United, Eric Okutu aliyeonyesha nia ya kuondoka ndani ya timu hiyo. Mghana huyo aliyetua nchini akitokea Hearts of Lions FC ya Ghana, msimu uliopita alifunga mabao saba ya Ligi Kuu huku ikielezwa anataka kuondoka ili akaungane na Goran Kopunovic aliyewanoa nyuki. 

MAAFANDE wa Tanzania Prisons, wako hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa mshambuliaji wa Mbeya Kwanza, Oscar Mwajanga. Nyota huyo alikuwa na kiwango kizuri msimu uliopita katika Ligi ya Championship akimaliza na mabao 19, nyuma ya vinara, Edgar William (KenGold) na Boban Zirintusa wa Biashara Utd waliofunga 21 kila mmoja. 

Related Posts

en English sw Swahili