Xavi: Msihofu, kina Mkude, Bocco wapya wanakuja!

KATIKA safari ya kutafuta mafanikio kuna nyakati nyingi binadamu hupitia na kukumbana nazo kati ya zile za furaha na huzuni.

Hakuna wakati mbaya kama kukata tamaa. Haijalishi umejaribu mara ngapi, umeshinda mangapi, cha msingi ni kuendelea kupambana na kujifunza zaidi na zaidi.

Mfano mzuri ni kocha wa timu ya vijana ya Simba, Mohamed Mrishona Mohamed ‘Xavi’ ambaye anaelezea tukio lililowahi kumtokea akiwa mchezaji na kumkatisha tamaa ya kuacha kabisa soka.

“Nakumbuka Ligi ya Mapinduzi, timu ya taifa ya Jang’ombe tulicheza na Yanga zaidi ya miaka minane nyuma, niligongana bahati mbaya na mchezaji wa timu pinzani nikaumizwa tumbo.

“Nilipopelekwa hospitalini nikafanyiwa upasuaji wa tumbo, nikaambiwa chango zimechanika, hivyo nikashauriwa na madaktari nipumzike kwa mwaka mmoja nikasema siwezi kuendelea kucheza.”

Anasema ndipo ile kauli ya kukata tamaa mwiko ikamjia akilini mwake na kufanya uamuzi wa kusomea ukocha ili kuendelea kubaki kwenye soka.

“Mpira wa miguu upo kwenye damu, sikukata tamaa nikaamka na kusema naweza kusomea ukocha na hadi sasa nipo Simba nafundisha vijana wa U-17 na U-20 lakini pia ni kocha wa vijana wa timu za taifa, Bara na visiwani.”

Anasema mabadiliko kwa vijana hayakuwa ya siku moja kwani klabu hiyo ilianzisha mradi wa kutafuta vijana kwa ajili ya kuwakuza na kuleta ushindani.

“Kwanza niseme wakati sisi tunaingia Simba ni kweli hatukuikuta timu ikiwa vizuri kwani ulikuwa ndio mchakato wa mwanzo,” anasema na kuongeza:

“Baada ya hapo tukaanza kuwagawa vijana kulingana na umri, U-17 na U-20 kwa sababu sasa hivi mpira ni sayansi unaweza kumpa mazoezi mchezaji halafu kakudanganya umri ukamsababishia matatizo.

“Ni kweli hatukuanza vizuri, tulipopata nafasi ya dirisha dogo tukatengeneza timu, tukawafanya wachezaji wetu kuzoeana na tukashukuru timu imefika nusu fainali ambayo tumeendelea na tunaamini msimu ujao tutavuka hatua hiyo.”

Anasema kama klabu itaendelea na mradi huo basi watakuja vijana wengi zaidi aina ya kina John Bocco na Jonas Mkude ambao waling’aa Simba.

“Kipindi kile Simba ilipandisha wachezaji kadhaa kama Mkude, Said Ndemla, Abdallah Seseme na unaona matunda yake wamelipa na wote hawa bado wanaendelea kucheza Ligi Kuu hivyo kama mpango ukiendelea tutakuja kuwa na timu yenye ushindani,” anasema.

MAUA KWA RWEYEMAMU, MATOLA

Anasema huwezi kutaja mabadiliko ya timu hiyo ukawaacha viongozi wawili ambao wana mchango mkubwa kwenye soka la vijana Simba.

“Niwasifu sana viongozi wangu, Patrick Rweyemamu na Selemani Matola wana macho ya kuona vipaji vya vijana na tunawaona mazoezini kweli wamefanya kazi.

“Ni watu ambao wamekuwa kwenye timu za vijana kwa muda mrefu, mategemo yangu tufike mbali zaidi unaweza kuona timu bado mpya lakini imefika nusu fainali.”

Anasema kipindi hiki cha likizo anafundisha mazoezi binafsi kwa wachezaji wote, wanaocheza soka la wanawake, Ligi Kuu na vijana.

“Na hizi programu nawapa kulingana na matakwa ya mchezaji mwenyewe, mfano kipindi hiki cha mapumziko mchezaji anapewa ripoti na kocha wake mazoezi ya aina gani hivyo naisoma na kuwapatia,” anasema na kuongeza:

“Mfano wanakuja kina Simon Msuva, Opah Clement, Aisha Masaka, Ibrahim Bacca kuwapa sapoti vijana. Vijana wanakuja kusema, kocha mimi nina shida hii na uzuri huu hivyo namtengeneza kulingana na yeye alivyo.”

Anataja faida za mazoezi binafsi kuwa; “Ninaowafundisha mimi nimewatazama kwenye mechi zao, nimeona udhaifu ninaoufanyia kazi na baada ya hapa nitawaangalia tena kama wamebadilika, ili waendane na soka la kisasa kwasababu wanahitaji kujifunza zaidi.”

Mbali na kufundisha soka, Xavi pia ni kocha wa mazoezi ya mwili yaani fitness coach, fani ambayo alishauriwa kuisomea na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Oscar Mirambo.

“Mirambo huwa anatuambia mara nyingi tunapokutana, ukipata muda somea vitu vingine mfano inaweza kutokea siku kocha wa makipa kapata dharura unashika nafasi yake na mambo yanakwenda,” anasema na kuongeza:

“Kuwa na ufiti ndio silaha kubwa ya kuwa na timu nzuri yaani kama wachezaji wako fiti kocha anapata mteremko tu wa kupanga mambo yake.”

Sio kwa wachezaji wa Bongo tu, Mrishona anapata tenda ya kufundisha hadi wachezaji wa kigeni akimtaja kiungo wa zamani wa Yanga, Chico Ushindi.

“Kuna mawakala wananitafuta kuna wachezaji hawa wanataka niwafundishe, pia tunatarajia mwezi huu kupata wachezaji watatu kutoka AS Vita,” anasema na kuongeza:

“Pia niwape pongezi wachezaji wa Kitanzania, naweza kusema wao ni mabalozi wakubwa wa kunitafutia wachezaji wengine wanapokwenda kwenye klabu za nje na hata za ndani.”

Kuna wachezaji mbalimbali anaowafundisha mazoezi binafsi pindi wanapopata mapumziko ama Ligi Kuu inapomalizika na anawataja kama Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (aliyemaliza makataba na FC Lupopo ya Congo), Crispin Ngushi (Coastal Union), Ibrahim Bacca (Yanga), Nassoro Hamduni (Geita Gold) kwa kuwataja kwa uchache.

Kwa upande wa wanawake yupo Opah (Besiktas ya Uturuki), Diana Msewa (Amed SK ya Uturuki),Sheldah Boniface (Simba Queens), Clara Luvanga (Al Nassr ya Saudia) na Enekia Lunyamila (Eastern Flames – Saudi Arabia).

“Wengine kina Feisal (Salum) ambao wanakaa mbali inakuwa ngumu kufika kila siku lakini nawapa maelekezo na wakipata muda wanajumuika na wenzao.”

Related Posts