Hii hapa hatari ya mzazi kubagua watoto

Dar es Salaam. Upo usemi wa wahenga usemao; “uchungu wa mwana aujuaye mzazi.”

Lakini pia hawakuishia hapo, wakaongeza mwingine usemao; “Hakuna mapenzi ya dhati zaidi ya yale yatokayo kwa mzazi.”

Licha ya kauli hizo za mababu zetu kuiasa jamii, bado mambo ni tofauti.

Wapo baadhi ya wazazi hawana upendo na wengine wana ubaguzi wa waziwazi kutoka kwa watoto wao.

Hiyo inatokana na tabia ya baadhi ya wazazi kuonyesha upendeleo kwa mtoto mmoja au baadhi ya watoto kuliko wengine, na wakati mwingine hata kuonyesha chuki ya wazi kwa mtoto au watoto hao.

Jambo hili linaweza kuwaacha watoto wanaobaguliwa wakiwa na upweke na simanzi moyoni.

Hali hii inaweza kuwasababishia watoto hao msongo wa mawazo na hata migogoro ya kifamilia.

Baadhi ya watu wanaopitia hali hiyo ni pamoja na Patrick Peter, mkazi wa Kimara, jijini Dar es Salaam.

Anasema ana huzuni kutokana na tabia ya mama yake kuonyesha upendeleo zaidi kwa mdogo wao wa mwisho ambaye ni wa kiume, licha ya kuwa wote wamefikia hatua ya kujitegemea kimaisha.

“Katika familia yetu tumezaliwa watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume ambaye ni wa mwisho, hata hivyo mama amekuwa akionyesha waziwazi kumpenda zaidi mdogo wetu na wakati mwingine kututamkia kuwa anatuchukia, jambo hili huwa linaniumiza sana,” anasema.

Hata Zuwena Salum, mkazi wa Chanika, jijini Dar es Salaam, anasema amewahi kupitia hali kama hiyo kwa baba yake kutomuonyesha kumpenda, huku mara kadhaa akimtamkia kuwa anapomuona, anamkumbushia nyakati ngumu alizopitia alipokuwa anaishi na mama yake.

“Nimelelewa nikiona bayana baba akiwapenda zaidi watoto aliozaa na mama yangu wa kambo kuliko mimi hadi hivi sasa, japokuwa nimeanza kujitegemea, alikuwa akiwaletea zawadi na hata katika mahitaji ya msingi ya shule na nyumbani, kipaumbele kiliwekwa kwa watoto hao kuliko mimi, hali hiyo iliniumiza sana.”

Jenipher Mwaikenja, mzazi wa watoto wawili anasema ni kweli wapo baadhi ya wazazi wenye tabia ya kuwapendelea baadhi ya watoto wao kuliko wengine.

Hata hivyo, anasema hiyo wakati mwingine husababishwa na uwezo wa kifedha walionao na namna ambavyo anakuwa msaada katika familia.

“Pia wapo wazazi ambao wamekuwa wakiwapa vipaumbele na upendo zaidi baadhi ya watoto wao kutokana na kufanya vizuri shuleni kuliko mwingine, ana bidii katika kazi na hata kuendana na falsafa pamoja na miongozo ambayo wazazi wanaitoa,” anasema.

Juma Sukambi, baba wa watoto watano anasema hakuna mzazi asiyempenda mtoto wake, ila pengine mtoto hupatwa na wivu na kuona mwenzake anapendelewa zaidi kuliko yeye, pengine anapoona mwenzake anazawadiwa na kupongezwa mara kwa mara, labda pale anapofanya vizuri katika masomo yake.

“Hivyo anapoona mwenzake anapongezwa na mambo mazuri anayofanya kama vile kufanya vizuri katika masomo, nidhamu na utii kwa familia na jamii na mengineyo mazuri na asiyefanya hivyo anapoadhibiwa kwa lengo la kumfanya awe na tabia njema na kuwa bora kama mwenzake, huweza kuona kama hapendwi,” anasema mzazi huyo.

Wanasaikolojia waeleza sababu

Mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya uhusiano na malezi kutoka Psychomotive Internation, Charles Kalungu anasema kuna sababu mbalimbali za kisaikolojia zinazoweza kumfanya mzazi kupendelea zaidi mtoto au baadhi ya watoto na mojawapo ni namna alivyompata mtoto huyo.

“Unaweza kukuta ujauzito wa mtoto asiyemuonyesha mapenzi aliupata kwa kubakwa na mtu asiyempenda, hiyo inaweza ikawa sababu ya kuwa na hasira kwa mtoto huyo, hivyo kushindwa kumuonyesha upendo wa dhati,” anasema Kalungu.

Akasema sababu nyingine inawezekana pia ikasababishwa na namna alivyopata shida ya malezi na ukuaji wa mtoto husika.

“Unakuta mama amepata tabu sana kumlea mtoto na pengine bila hata msaada wa mtu yeyote katika kipindi chote cha malezi, hivyo mtoto huyo anapofanya jambo ambalo labda amekuwa akilifanya mara kwa mara na kutomsikiliza mzazi wake anapomuonya, hupandwa na hasira kupindukia,” anasema.

Pia, jambo kama hili linaweza kusababishwa na visasi baada ya wazazi kuachana, kutokana na maumivu anayopitia akiunganisha na changamoto nyingine za kimaisha anaweza kujikuta anatengeneza chuki kwa mtoto husika.

Kwa upande wake mwanasaikolojia, Prisca Sao anasema hali ya mzazi kumpendelea au kuonyesha upendo zaidi kwa mtoto fulani huweza kusababishwa na mtoto huyo kuwa na jinsi ambayo mzazi au wazazi husika walikuwa wakiitamani kupata kwa muda mrefu.

“Mfano wazazi walikuwa wanapata watoto wa kiume tu, kisha wakapata wa kike, baadhi yao huonyesha upendo kwake,” anasema Sao.

Pia, anaongezea kuwa wakati mwingine mzazi huongeza zaidi umakini na upendo kwa mtoto fulani kutokana na changamoto za kiafya alizonazo.

Hata hivyo, Kalungu anasema tabia ya mzazi kuonyesha upendo zaidi kwa mtoto wake mmoja kuliko mwingine huweza kupelekea mtoto au watoto kupunguza upendo na huruma kwa wazazi wao au hata watu wengine katika jamii.

“Tunatarajia mtoto anapofanikiwa kimaisha atakuwa msaada kwa wazazi wake, lakini kutokana na kukosa upendo kutoka kwa wazazi husika alipokuwa mdogo huweza kumpelekea kushindwa kuwasaidia wazazi wake pale wanapohitaji msaada, jambo ambalo limekuwa kikishuhudiwa mara kadhaa katika jamii,” anasema.

Pamoja na kupunguza huruma kwa wazazi, Kalungu anaeleza kuwa tabia hiyo huweza kuwafanya wazalishe chuki na utengano kwa watoto.

“Endapo mzazi anampendelea mtoto mmoja au wawili wakati wengi wao wakionekana hawafai, ndipo watoto wale wanaochukiwa huamua kujitenga na wapendwao,” anasema.

Vilevile mwanasaikolojia Sao anaongeza kuwa watoto walioathirika na tabia hiyo mara nyingi hupunguza kujiamini na hata kushindwa kutengeneza mahusiano ya muda mrefu.

Related Posts