Mzee wa miaka 78 aliyefungwa kwa ubakaji, kuambukiza HIV aachiwa huru

Iringa. Mahakama Kuu ya Tanzania, imemwachia huru mzee wa miaka 78 ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa madai ya kumbaka mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 na kumwambukiza virusi vya Ukimwi (HIV) kati ya 2022 na 2023.

Mbali na Mahakama ya Wilaya ya Iringa kumuhukumu vifungo viwili vya maisha Oktoba 20, 2023, Mahakama ilikuwa pia imemwamuru kumlipa mtoto huyo, fidia ya Sh30 milioni, kulipa faini ya Sh5 milioni na kuchapwa viboko 11.

Mzee huyo alikuwa ametiwa hatiani kwa makosa matatu, moja la kubaka mtoto mwenye umri chini ya miaka 18, kumwambukiza virusi vya Ukimwi (HIV) kwa makusudi na kosa la tatu likiwa ni kufanya jaribio la kumbaka mtoto huyo.

Hukumu ya kubatilisha na kufutwa adhabu hizo, imetolewa Juni 28, 2024 na Jaji Eliamin Laltaika wa Mahakama Kuu kanda ya Iringa, akisema upande wa Jamhuri haukuweza kuthibitisha kesi hiyo kwa viwango vinavyokubalika kisheria.

Kubatilisha kwa hukumu hiyo na hatimaye kuachiwa huru kwa mzee huyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kimaadili, kulitokana na rufaa aliyoikata Mahakama Kuu kanda ya Iringa, akiegemea sababu tano kupinga hukumu hiyo.

Miongoni mwa hoja hizo ni, Hakimu aliyemhukumu alikosea kisheria kumtia hatiani na kumpa adhabu hizo kwa kuegemea ushahidi dhaifu wa mwathirika (mtoto), aliyeshindwa kutaja tarehe halisi ambazo mshitakiwa alimbaka.

Hoja nyingine ni Hakimu alikosea kwa kushindwa kumpa nafasi ya kuipinga fomu namba 3 ya Polisi (PF3) na alikosema kisheria kumtia hatiani kwa kuegemea maelezo yake ya onyo, bila kujali kuwa ilirekodiwa pasipo kufuata sheria.

Mbali na hoja hizo, alijenga hoja Hakimu aliyemwadhibu, alikosea kisheria kwa kumtia hatiani na kumuhukumu kwa kupokea vielelezo ambavyo havikuainisha mipaka kipi ni cha ubakaji na kipi kilikuwa ni kwa ajili ya kosa la kujaribu kubaka.

Hoja ya tano ni kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha shitaka dhidi yake pasipo kuacha mashaka na kwa viwango vinavyokubalika kisheria, hivyo akaiomba mahakama ibatilishe kutiwa kwake hatiani na kufuta adhabu aliyopewa.

Jamhuri ilivyojitahidi kumng’ang’ania

Akijibu hoja za rufaa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), wakili wa Serikali, Muzzna Mfinanga alipinga hoja ya mleta rufaa kuwa mwathirika (mtoto) alishindwa kueleza ni tarehe gani na mwezi gani alimtendea makosa hayo.

Alieleza hati ya mashitaka ilionyesha makosa yaliyokuwa yakimkabili yalitendeka tarehe mbalimbali kati ya mwaka 2022 na 2023, hivyo tarehe hazijulikani bali ni miaka hiyo na tukio la kwanza la kubakwa lilikuwa 2022 akiwa darasa la nne.

Wakili huyo alieleza kulingana na mwenendo wa kesi, tukio la pili na la tatu la ubakaji linaelezwa vizuri katika ukurasa wa 11 na 12 wa mwenendo na kwamba kulingana na umri wa mtoto, haikuwa rahisi kukumbuka mwezi na tarehe.

Kuhusu kutopewa nafasi ya kupinga PF3 wakati ikitolewa kortini kama kielelezo, wakili huyo alikiri katika mwenendo uliochapwa kulikuwa na makosa ya kiuandishi, lakini nakala halisi inaonyesha alipewa nafasi hiyo na Mahakama.

Katika hoja ya tatu inayohusu maelezo yake ya onyo aliyoyaandika polisi, wakili huyo alisema wakati ilipokuwa inataka kutolewa kama kielelezo, mrufani alikaribishwa kuipinga, lakini alisema hakuwa na pingamizi lolote juu yake.

Kuhusiana na hoja kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha kesi hiyo, wakili huyo alisema mashitaka yote matatu yalithibitishwa pasipo kuacha mashaka kwani Jamhuri ilichotakiwa kufanya ni kuthibitisha vitu vitatu.

Jambo la kwanza kwa mujibu wa wakili huyo, ni kuthibitisha uwepo wa tendo la kumwingilia mtoto huyo, utambulisho wa mshukiwa au mtuhumiwa wa tendo hilo na umri wa mtoto, ambapo mama mzazi wa mtoto alithibitisha umri wake.

Hoja ya maambukizi ya HIV

Kuhusiana na kosa la pili la kumwambukiza kwa makusudi HIV, wakili Mfinanga alisema upande wa mashitaka ulichohitaji ni kuthibitisha dhamira ya kuambukiza HIV, kitendo halisi cha kuambukiza na utambuzi wa mshukiwa wa tendo hilo.

Alirejea katika ukurasa wa 49 wa mwenendo wa shauri hilo, ambapo mzee huyo alikiri mwenyewe kuwa yeye ni mwathirika na alikuwa akitumia dawa.

Wakili Mfinanga alisema kitendo cha kubaka kilichofanywa na mrufani (mzee huyo), kama kilivyoelezewa na mtoto mwenyewe, kilithibitisha uambukizaji huo na vipimo vilivyofanyika baina yao vilithibitisha hilo.

Katika vipimo hivyo, mama wa mtoto alipimwa na hakuwa na maambukizi.

Kuhusu kosa la jaribio la kubaka, wakili Mfinanga alijenga hoja kwa kugemea mwenendo wa shauri katika ukurasa wa 8 na 9 ambapo mwathirika ambaye ni shahidi mzuri katika kesi za aina hiyo, ikionyesha jaribio lilikuwa tarehe 21.8.2023.

Mzee alivyopangua hoja za DPP

Akiwasilisha majibu ya nyongeza kwa hoja zilizowasilishwa kortini na DPP, mzee huyo aliyejiwakilisha mwenyewe kortini katika rufaa hiyo, alisema yeye hawezi kuzungumza kama wakili wa DPP kwa kuwa yeye sio mzungumzaji mzuri.

Alieleza kwa tarehe ambazo zitatajwa kuwa alijaribu kubaka, tayari alikuwa amekamatwa na yuko mahabusu na mahakama haikujisumbua kutafuta ukweli wa tuhuma hizo na hakupewa nafasi yoyote ya kuipinga PF3.

Mrufani huyo alisema mwenendo uliandikwa kimakosa kuwa alikubali PF3 hiyo ipokelewe kama kielelezo na ushahidi wake haukurekodiwa popote, hivyo aliamua kukata rufaa kwa kuwa hakutendewa haki na hakutenda kosa.

Alidai alisukumwa katika mazingira ambayo upande wa mashitaka ulijichukulia faida (advantage) kwa vile yeye hajui kusoma wala kuandika.

Alipotakiwa na mahakama aeleze mtiririko wa kabla na baada ya matukio hayo, alieleza yeye alikuwa mkazi wa Idodi na hakuwa na uhusiano na mtoto na aliishi hapo kijijini kwa miaka mitatu alipokwenda kutafuta kazi za kilimo.

“Aliishi nyumbani kwa rafiki yake akiwa hana familia na akiwa na umri wa miaka 78. Kabla ya kuondoka Mauninga, alisema alipima afya na kuendelea kupokea huduma Idodi,”alisema Jaji akinukuu utetezi wa mzee huyo.

Alieleza Mahakama familia ya mtoto huyo walikuwa ni wanakijiji wenzake lakini wakiishi mitaa tofauti na walifahamiana na awali hakuna mtu yeyote aliyemuuliza kuhusu yeye kuwa na maambukizi hayo ya HIV.

Hata hivyo, alisema daktari aliyemfahamu yeye kama mteja wake ndio aliyeeleza hayo baada ya kufahamu anatuhumiwa kwa kosa la ubakaji na  siku iliyofuata, walichukuliwa sampuli mtoto na yeye bila ridhaa yake.

Sababu za Jaji kumwachia huru

Katika hukumu yake kuhusiana na rufaa hiyo, Jaji Laltaika alisema baada ya kupitia kwa umakini kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo katika mahakama ya wilaya ya Iringa, mrufani alishitakiwa kujaribu kubaka na kubaka kwa mtu huyo mmoja.

“Hii haiendani vyema na sanaa na ufundi wa kuandaa mashitaka ya jinai. Wakili wa Serikali alijaribu kutetea lakini nafikiri anaweza kushauriwa kurejea utamaduni (wa namna ya kuandika hati ya mashitaka),”alieleza Jaji Laltaika katika hukumu hiyo.

“Vyovyote itakavyokuwa, kushindwa kuonyesha tarehe za kosa lilipotendeka na kuishia tu kuonyesha kwamba ni kwa tarehe mbalimbali katika hati ya mashitaka kunaongeza chumvi kwenye kidonda,” alisema Jaji Laltaika na kuongeza;-

“Hati ya mashitaka ilionyesha kuwa kosa lilitendeka tarehe mbalimbali kati ya 2022 na 2023. Hata hivyo ushahidi wa mtoto haukuwa wazi (vague) na haukutoa kwa wazi ni lini. Hii inadhoofisha kesi ya upande wa mashitaka.”

Jaji akaendelea kueleza kuwa mrufani analalamika hakupewa nafasi ya kuipinga PF3 ambayo ni sehemu ya ushahidi muhimu, lakini wakili wa Serikali alieleza kuwa kulikuwa na makosa ya uchapaji lakini kwenye nakala halisi hili linaonekana.

“Wakili wa Serikali tena kwa heshima kubwa, alishindwa kutoa sababu zilizomfanya asiiondoe hiyo PF3 kutoka kwenye kumbukumbu za mahakama. Kwa hiyo mahakama inaiondoa PF3 hiyo kwenye rekodi za mahakama,”alisema Jaji.

Kuhusu maelezo ya onyo kuwa yalipokelewa na mahakama kinyume cha sheria, alisema maelezo ya mrufani kuwa alilazimishwa na hakupewa nafasi ya kueleza hadithi ya upande wake inafanya maelezo hayo yachukuliwe bila uhiari.

Jaji akasema umri wa miaka 78 alionao mzee huyo na kutokuwa na elimu, havikuzingatiwa kikamilifu na mahakama na vigezo hivyo vingeweza kumfanya asijue namna ya kupinga PF3 wala maelezo ya onyo.

Halikadhalika Jaji alisema mrufani alidai alipimwa HIV bila ridhaa yake na hivyo kuibua uhalali na maadili ya taratibu hizo za kitabibu na kueleza kuwa ushahidi unaonyesha wazi ofisa tabibu alitumia vibaya nafasi yake kufichua hali  ya kiafya ya mrufani bila ridhaa.

Jaji alisema kitendo cha upande wa mashitaka kutumia ushahidi wa aina hiyo kinakiuka haki ya mrufani (mshtakiwa) kuhusu haki ya faragha, hivyo pamoja na uchambuzi kwa ujumla wake, aliona Jamhuri haikuthibitisha kesi hiyo.

Related Posts