Katika makala yaliyopita tuliona umuhimu wa tabia ya uwajibikaji kwa mtoto. Bila uwajibikaji, tulisema, mtoto hataweza kufanya majukumu yake ipasavyo kwa sababu wakati wote atakuwa anangoja wengine wafanye kwa niaba yake.
Ili kujenga uwajibikaji, tulipendekeza mipaka iwe sehemu ya maisha ya mtoto. Mamlaka inamsaidia mtoto kuelewa kipi lazima yeye akifanye na kipi hawezi kukifanya kwa sababu kiko nje ya mipaka yake.
Aidha, tulidokeza pia kuwa watoto waliokuzwa bila kutambua mipaka yao katika maisha, mara nyingi hupata shida kuwajibika wanapokuwa watu wazima. Ni hivyo kwa sababu wamezoeshwa kutarajia watu wengine wafanye vitu ambavyo kwa kawaida walipaswa kuvifanya wao.
Makala haya yanaangazia mambo mengine matatu yanayojenga uwajibikaji kwa mtoto. Mambo haya ni kuweka utaratibu wa uwajibikaji, upendo na uhuru wa kuchagua. Kama tutakavyoona hivi punde, mambo haya hayafundishwi kwa maneno, bali kupitia maisha ya kila siku, ambayo matokeo yake humfanya mtoto ajisikie vibaya pale inapotokea hajawajibika.
Hakuna mtoto anaweza kuwajibika katika mazingira ambayo kuna mianya imeachwa anayoweza kuitumia kutegea. Ukiacha maisha yaende bila utaratibu hapo nyumbani utakuza watoto wasiojua wafanye nini kwa sababu haifahamiki nani hufanya nini na kwa wakati gani.
Ukitaka mtoto awajibike, unahitaji kuweka mfumo mzuri unaotambua nani amefanya nini na kwa ufanisi wa kiwango gani. Faida ya mfumo kama huu ni kukusaidia wewe mzazi kujua kiwango cha ushiriki wa kila mmoja kwa nafasi yake.
Ili hili liwezekane, shirikiana na mtoto kutengeneza sheria (taratibu) zinazoongoza maisha yake tangu anapoamka mpaka anapokwenda kulala usiku. Hapa nina maana ya kujenga desturi au mazoea ambayo kitu kisipofanyika inakuwa rahisi kufahamu.
Kwa mfano, ni muhimu saa ya kuamka na kulala kwa mtoto ijulikane. Mtoto afahamu kuwa nyumbani kwao, huwezi kulala mpaka saa moja, au ukawa macho mpaka usiku wa manane isipokuwa kwa nyakati maaluma. Kadhalika, lazima ifahamike, baada ya kuamka kila mmoja kupaswa kufanya nini.
Utaratibu kama huu wa kuhakikisha ratiba ya kila siku inafahamika una faida kuu mbili. Kwanza, unamsaidia mtoto kupambanua majukumu yanayomwangukia yeye binafsi. Unapokuwa na familia ambayo kila mtu anaweza kushika chochote anachotaka, ni rahisi baadhi ya watu kujificha na uvivu wao hautafahamika kirahisi.
Lakini pia, mgawanyo wa majukumu unasaidia kujua nani hajafanya wajibu wake na hivyo kuchukuliwa hatua za kumwajibisha. Huwezi kutoa adhabu kwa haki kama haikuwa inafahamikaa bayana nani anapaswa kufanya nini wakati gani.
Binadamu, kwa hulka yetu, hatupendi sheria kwa sababu zinaanika mapungufu yetu. Fikiria utaratibu unaosaidia kumbaini kirahisi mtu ambaye, kwa sababu moja au nyingine, hakufanya wajibu wake. Kwa anayekosea itakuwa vigumu kwake kuupenda.
Utakumbuka nilitangulia kusema kwamba, kwa kawaida, watoto hupenda kuwa tegemezi kwa watu wengine. Unapoweka utaratibu unaomlazimisha kupunguza utegemezi huo kwa watu wengine hapo nyumbani, hawezi kufurahia.
Katika mazingira kama haya, ipo haja ya kujenga mazingira ya upendo kwa watoto.
Upendo siyo kudekeza wala kufumbia macho mapungufu ya umpendaye. Upendo ni kumfanya mtoto awe na hakika kwamba wewe mzazi wake unamjali.
Kwa maneno mengine, kumpenda mtoto ni kumfanya ajue kwamba hata kama itatokea hamtaelewana, hiyo bado haipunguzi thamani aliyonayo kwako. Kwa hiyo namna rahisi zaidi ya kumfanya mtoto afuate utaratibu mliokubaliana ni kumhakikishia upendo wako kwake.
Pamoja na kuweka utaratibu wa uwajibikaji, ni muhimu kumsaidia mtoto kuongozwa na dhamira yake zaidi kuliko sheria. Mtoto anayeongozwa na sheria ni rahisi kuziasi siku atakapoondoka nyumbani.
Ndio maana wapo watoto hubadilika sana pindi wanapokwenda shule mbali na wazazi.
Watoto wa namna hii, mara nyingi, huwa wamelelewa kwenye mazingira yanayowabana kupindukia kiasi cha kuwafanya wajione kama wafungwa fulani wanaolazimika kufuata utaratibu wasiouamini. Inapotokea kuna upenyo wa kufanya watakavyo, tabia inageuka.
Haitoshi mtoto kuzifahamu sheria. Mruhusu mtoto kuwa na kiasi fulani cha uhuru wa maamuzi. Hii, hata hivyo, haimaanishi kumpa mtoto uhuru uliopindukia. Huwezi kuwa mzazi mwenye busara kama mwanao anaweza kujifanyia mambo vile atakavyo.
Pale ambapo usalama wa mtoto unakuwa hatarini, ni wazi utalazimika kubana kiasi fulani cha uhuru kwa faida yake.