Dar es Salaam. Viongozi wa dini, wananchi na mtaalamu wa saikolojia wamekuwa na maoni tofauti kufuatia kushuka kwa idadi ya ndoa zilizosajiliwa, huku talaka zikiongezeka.
Baadhi wanasema ndoa zinazofungwa ni nyingi lakini hazisajiliwi rasmi, wakati wengine wanadai watu wamekuwa na hofu ya kuoa kutokana na wimbi la talaka na kuona ndoa ni ngumu.
Baadhi wanasema ndoa zinazofungwa ni nyingi, lakini hazisajiliwi, wengine wanadai watu wamekuwa na hofu ya kuoa kwa sababu ya wimbi la talaka na kuona ndoa ni ngumu.
Kauli hizo zimetolewa ikiwa ni baada ya kitabu cha hali ya Uchumi wa Taifa 2014, kilichotolewa na Wizara ya Fedha kuonyesha ndoa zilizosajiliwa zilipungua kwa asilimia 10.89 mwaka 2023, huku talaka zilizosajiliwa zikiongezeka kwa asilimia 93.7 kutoka zilizokuwapo mwaka 2022.
Kitabu hicho kinaonesha kuwa mwaka 2023 ndoa zilizosajiliwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (Rita) zilikuwa 45,455, ikiwa zimeshuka kutoka 51,011 mwaka 2022, huku talaka zikifika 866 kutoka 447 mtawaliwa.
Hata hivyo, ndoa zilizosajiliwa mwaka 2022 zilikuwa ni ongezeko la asilimia 39.2 ikilinganishwa na zilizosajiliwa mwaka 2021 zilizokuwa 36,645, wakati ambao talaka zilikuwa pungufu kutoka 512.
“Ndoa ni hiari, mwanamke na mwanamume wanaoana ili kuishi pamoja, hivyo kupanda au kushuka kunatokana na utayari wa watu kwa wakati huo, hivyo si lazima ndoa ziendelee kuongezeka,” amesema Patricia Mpuya, Meneja wa usajili Rita.
Amesema hali hiyo hufanya baadhi yao kuwa tayari kuishi pamoja na hawaoni sababu ya kufunga ndoa.
Lakini kwa mujibu wa Mpuya, hali hiyo ni tofauti na ya talaka wanazosajili wakati tayari uamuzi umeshafikiwa na wawili walioamua kuvunja ndoa yao, ama mahakamani au kwa viongozi wa dini na ustawi wa jamii.
Suala la kupungua kwa ndoa zilizosajiliwa, lilipingwa na Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo ambaye amesema huenda watu hawasajili ndoa zao, lakini si kwamba hawaoani.
“Wapo watu wengi wanafunga ndoa misikitini, kanisani, kuendana na imani zao, kwa sisi Waislamu, hasa wakati wa Ramadhan wanaume wengi wanaoa kwa sababu wanataka iftar na daku halali, labda tuseme mwamko wa wao kwenda kuzisajili ndiyo mdogo,” amesema Kitogo na kuongeza;
“Kwa talaka naweza kukubali kuwa zinaongezeka na hii ni kutokana na tamaa na kutokuwapo kwa maelewano ndani ya familia, kuachana ndiyo inakuwa uamuzi wa mwisho, ila kuoa watu wanaoa,” amesema.
Amesema miongoni mwa sababu za uwepo wa talaka hizo ni tamaa ya mali pale mmoja wa wanandoa anapoona ana mafanikio kidogo, anatamani umiliki wa peke yake.
Hapo ndipo uamuzi wa kutaka amiliki kitu chake huingia na kujikuta ndoa ikisambaratika.
“Hapo sasa ndiyo linapokuja tatizo, watu wamejenga Mbagala wanataka watengane wagawane wanauza nyumba, hiyo fedha watajenga wapi, tamaa za kibinadamu, kutokuelewana kwenye mahusiano ni tatizo,” amesema Kitogo.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge – Ngara, Severine Niwemugizi amesema mara nyingi ndoa inaanza na familia iliyo imara na thabiti wakati ambao uthabiti wa ndoa unahitaji matayarisho.
Amesema matayarisho hayo yatawasaidia watu kujua sifa za ndoa iliyokuwa bora na wajibu wao, huku akifafanua kuwa kutokuonekana kwa maana na umuhimu wa ndoa, ndiyo unaofanya idadi kushuka.
“Kwa bahati mbaya ulegevu wa familia umevamiwa na vitu vingi ninavyoweza kuita ni nguvu za shetani.
“Hali hii inafanya maana na umuhimu wa ndoa kupungua, watu wanataka uhuru usiokuwa na mipaka, hawataki kujifunga, ni mtindo ulioanzia huko nje unakuja hadi hapa nchini, mtu anataka kurukaruka bila kuzuiwa,” amesema Askofu Niwemugizi.
Kwa bahati mbaya walioingia katika ndoa bila kujua maana yake, ndio hao ambao wanaishia kupeana talaka. “Kabla ya kila kitu mtu anapaswa kujua ndoa si suala binafsi, ndiyo maana wanaojua ukiingia kutoka ni kazi linafanya wengine kushindwa kuingia,” amesema Askofu Niwemugizi.
Mwanasaikojia Charles Kalungu amesema matukio yanayotokea ndani ya ndoa na kushuhudiwa na baadhi ya vijana ambao bado hawajaoa na kuolewa ni miongoni mwa sababu kuu inayofanya vijana wengi kujivuta kuingia katika kundi hilo.
Amesema matukio hayo wanapokutana nayo maeneo mbalimbali huwafanya kukosa amani, kuwa wenye hofu, woga na kudhani kuwa watakapokamilisha taratibu yatatokea wanayoyaona.
“Mbali na hili, pia zipo sababu nyingine ambazo zinaweza kuwafanya watu waogope kuingia kwenye ndoa, ikiwemo uchumi, maandalizi ya ndoa yenyewe pia ni vyema kuangalia upande gani ambao unafunga ndoa sana kati ya Wakristo na Waislamu,” amesema.
Wakati Kalungu akisema hayo, kwa Mwanasaikolojia John Ambrose ni tofauti, yeye anabainisha kuwa kutokuwapo kwa mawasiliano mazuri ni miongoni mwa njia ambazo zinakwamisha mahusiano mengi, kwani ni ngumu mtu kutatua matatatizo ikiwa hawezi kusikiliza.
“Mawasiliano haya siyo tu kupokea simu na kuongea, lakini hatuweki utimamu, usikivu wetu katika mazungumzo kama mke na mume au mtu na mwenzi wake, ukiwa mtu unayejua namna nzuri ya kuwasiliana unakuwa na subira, unamuelewa mtu na unamstahi,” amesema Ambrose.
Alitolea mfano wa baadhi ya ndoa kama zile ambazo mmoja ni mlevi, akilewa anamgombeza mwenzake lakini hawaachani miaka yote.
“Hawaachani kwa sababu wanaelewana, anaweza kuongea maneno mengi, lakini mwenzake anasema ni pombe, zikiisha atakaa vizuri kwa sababu wanajuana, japokuwa wakati mwingine changamoto ndogo ndogo zinatengeneza tatizo kubwa linaloonekana, kwa sababu hakukuwa na mawasiliano mazuri ya mwenzake anataka nini kifanyike,” amesema Ambrose.
Hata hivyo, amesema miongoni mwa vitu vinavyoweza kufanya uhusiano kutokwenda hatua nyingine ni uchumi, afya, malezi, makuzi, kushindwa kuheshimu hisia za watu na hata uaminifu.
Jackson Lolenzo, ambaye ni mmoja wa vijana waliozungumza na Mwananchi kuhusu suala hilo, amesema huenda lina ukweli ndani yake, huku akisema kuwepo kwa taarifa za ndoa ambazo hazifanyi vizuri katika mitandao ya kijamii na baadhi ya anayoyashuhudia ni kikwazo.
“Ukiacha kutokuwa na mtu anayefaa kuwa mke, kipato changu kutostahimili kuendesha familia, taarifa za mitandaoni na ninayoyaona yananiogopesha kuoa. Kuna rafiki yangu anatembea na mke wa mtu anayehudumiwa na mumewe kila kitu, lakini bado anatoka nje ya ndoa! Napata wapi nguvu,” amesema Lolenzo.
Amesema mauaji ndani ya ndoa, mke kamuua mume, mume naye kamuua mke nalo ni miongoni mwa sababu zinazomfanya kuendelea kufikiria mara mbili uamuzi wake kama ataoa au la.
Licha ya kuwa tayari ni baba wa mtoto mmoja, anasema bado analazimika kuangalia kama anayo sababu ya msingi ya kumuoa aliyezaa naye, kwa kile alichoeleza kuna baadhi ya vitu anavikosa.
“Ulisikia taarifa ya yule mchezaji aliyekuwa analea watoto watatu kumbe wote si wake, naogopa kupewa watoto wasiokuwa wangu ndani ya ndoa, naogopa,” amesema Lolenzo.
Kwa nini haoni kama mwanamke aliyezaa naye anafaa kuwa mke, amesema wivu uliopitiliza hadi katika sehemu ambazo hakupaswa kuzionea wivu na uongeaji uliopitiliza ni miongoni mwa vitu vinavyomkera.
“Najua siwezi kumpata mwanamke aliyekamilika, lakini angalau awe na mawili au matatu. Mwanamke niliyezaa naye ana mdomo sana, mimba yenyewe sikutarajia, ana wivu usiokuwa na manufaa, mimi nina marafiki wa kike wakati mwingine nawasiliana nao, lakini akiona ana kelele, ni ngumu,” amesema Lolenzo.
Hata hivyo, mtazamo wa Lolenzo ni tofauti na wa Digna Chundu, ambaye anaeleza kuwa katika ulimwengu wa sasa, baadhi ya wanaume wanashindwa kujua namna ya kusimama kama wanaume.
Anasema hilo amelishuhudia katika makuzi yake na mama alisimama kama kichwa cha familia katika kutoa huduma zote za familia licha ya kuwa ameolewa na mwanaume ambaye ana kipato.
“Baadhi ni wabinafsi, kipato anacho lakini hata kuhudumia watoto wake inakuwa ngumu, hali kama hii nimekuwa nikiishuhudia, inanifanya nione naweza kumudu gharama za maisha kama alivyokuwa mama miaka yote,” amesema Digna.
Maneno yake yalitofautiana na Lucia Chande, ambaye anasema mwanamume ndiye mwenye uamuzi wa mwisho linapokuja suala la ndoa.
“Mimi ni muolewaji, siwezi kumlazimisha anioe, yeye ndiye anajua anataka nini na wakati gani, anahitaji mwanamke wa aina gani, mtu akikuambia uchumi wake haumruhusu kuoa, utamlazimisha?” alihoji huku akiongeza:
“Wakati mwingine sisi pia ndio tunaweka ugumu wa kutaka vitu vikubwa ambavyo wenzetu hawawezi kumudu, mwisho wa siku hata kama alikuwa na mpango wa kuoa mwaka huu, inabidi aendelee kutunza kwa ajili ya mwakani,” amesema.
Askofu Niwemugizi akilizungumzia hilo amesema ili kuondokana na hilo, ni vema kukawa na matayarisho kwa vijana kabla ya kuingia ndani ya ndoa, hilo linaweza kufanyika kupitia mifano ya wazazi wao wanaowalea.
“Maandiko yanasema ndoa na iheshimiwe na watu wote, hivyo ni vema watu walio kwenye ndoa wajifunze kuitunza na kuiheshimu ili watu wengine wajifunze kutoka kwao na watoto wanaowalea wakiingia watajua maana ya ndoa na kuona si kitu cha kuingia na kutoka,” amesema.
Katika hili, Kalungu anashauri vijana watiwe moyo pia kuwasaidia watu kuondokana na ile dhana kuwa ili mtu uoe lazima uwe na kipato kizuri.
“Kuna watu wana vipato vizuri lakini ndoa zimewashinda, sasa wanajiuliza sisi tusiokuwa na vipato tutaishije humo ndani,” amesema Kalungu.