Rais Nyusi mgeni rasmi ufunguzi maonyesho ya Sabasaba

Dar es Salaam. Ushirikiano katika sekta za habari, afya na elimu ni miongoni mwa mambo watakayojadili Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Msumbiji, Felipe Nyusi.

Wakuu hao wa nchi, wanatarajiwa kukutana Julai 2, 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam kwa mazungumzo maalumu, baada ya Rais Nyusi kuwasili nchini kesho Jumatatu, kwa ziara ya kitaifa ya siku nne.

Sambamba na mazungumzo kuhusu ushirikiano katika sekta hiyo, ujio wa Rais Nyusi pia unalenga kuja kuwaaga Watanzania anapohitimisha miaka 10 ya uongozi wake nchini Msumbiji.

Hatua yake ya kuwaaga Watanzania inathibitisha uimara wa ushirikiano kati ya nchi hizo, ulioasisiwa tangu enzi za ukombozi.

Akizungumzia ziara hiyo leo Jumapili, Juni 30, 2024, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Afrika Mashariki, January Makamba amesema kesho Jumatatu kiongozi huyo atapokelewa nchini.

Mapokezi rasmi, amesema yatafanyika Julai 2, 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam yakifuatiwa na mazungumzo ya faragha baina ya viongozi hao wawili, kisha mazungumzo rasmi yatakayohusisha viongozi mbalimbali.

Mazungumzo hayo kwa mujibu wa Makamba, yatafuatiwa na kusainiwa kwa mikataba ya ushirikiano katika sekta za ulinzi na usalama, elimu, nishati, habari na  uchumi.

Kwa mujibu wa Makamba, Jumatano Julai 3, 2024 mkuu huyo wa nchi ya Msumbiji atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba.

Maonyesho hayo yameshaanza tangu Juni 28 na yatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2024 katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.

“Baada ya siku hiyo atakwenda visiwani Zanzibar kwa ziara binafsi kisha atarejea nchini Msumbiji Julai 4, 2024 ikiwa ni mwisho wa ziara yake,” amesema.

Sambamba na matukio hayo, ujio wa Rais Nyusi nchini unalenga pia kuwaaga Watanzania kwa kuwa anakaribia kumaliza muhula wake wa pili wa urais katika nchi hiyo.

Rais Nyusi ameiongoza Msumbiji kwa miaka 10 hadi sasa na Oktoba 2024 taifa hilo linatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu wa kumpata Rais mpya.

Maeneo ya mipaka ya nchi hizo, kwa mujibu wa Waziri Makamba kwa muda mrefu yanakabiliwa na changamoto za kiusalama na ziara hiyo inatarajiwa kusaidia kwenye eneo hilo.

Related Posts