Asimulia alivyoiba pete ya ndoa ya mama yake kununua dawa za kulevya

Mwanza. “Nikiwa nasoma shule ya msingi, nilipata rafiki kumbe alikuwa msafirishaji wa dawa za kulevya, kwa sababu nilikuwa na tamaa ya fedha, alinipa chaneli kwamba na mimi nikijiunga naye kusafirisha, nitakuwa napata fedha. Ilifika mahali nikatakiwa niwe nameza dawa hizo na kuzisafirisha.”

Hiyo ni kauli ya Abdallah Naseeb (28), mkazi wa Nyegezi jijini Mwanza, shujaa wa kupinga matumizi ya dawa za kulevya anayefanya kazi ya utoaji wa elimu kwa waraibu wa hizo jijini humo.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano, Abdallah anasema baada ya kuanza kutumika kuzisafirisha dawa hizo mwaka 2007, alijikuta akishawishika kuanza kutumia dawa aina ya Heroine, jambo lililomfanya asitishe masomo akiwa kidato cha tatu mwaka 2013.

Anasema baada ya kusitisha masomo, aliendelea kusambaza dawa hizo na wakati mwingine alikuwa akimeza hadi kete 50 kwa ajili ya kuzisafirisha kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine, jambo lililomfanya abadilike tabia na kuanza kufanya kila namna isiyo halali kupata fedha.

“Kuna siku nilikutana na mtoto mdogo akiwa ameshika Sh10,000 nadhani alikuwa ameagizwa dukani. Akili yangu iliniambia ile hela naweza kuichukua, nilimfuata na kumpiga, kisha nikamnyang’anya. Baadaye niligundua yule mtoto alipata majeraha, niliumia sana,” anasema Abdallah.

Abdallah anasema baada ya kukumbwa na uraibu wa dawa hizo ‘arosto’ alilazimika kufanya vitu hatarishi, ikiwemo wizi wa mali za nyumbani kama simu na unyang’anyi wa kutumia silaha (visu, panga), ili apate fedha ya kununua dawa hizo.

Anasema uraibu huo ulimpeleka mbali zaidi na kufikia hatua ya kuiba pete ya dhahabu ya ndoa ya mama yake mzazi, Hidaya Ally na kwenda kuiuza Sh30,000 kwa sonara, kitendo anachosema anakijutia mpaka sasa.

 “Nilivyoichukua nilienda moja kwa moja kwa sonara bila kujua kuwa kuiba pete ile kutakuwa na athari gani. Huwa nawaza nitairudishaje pete ya mama yangu kwa sababu ilikuwa ni kumbukumbu pekee kwa mama baada ya kifo cha baba yangu (Nassib Salum) kwake,” anasema na kuongeza;

“Mwaka 2018 kaka yangu alifariki, siku moja nilikutana na mama barabarani akilia, akaniambia baada ya kifo cha kaka anaona kama ameshapoteza watoto wawili nikiwemo mimi, kauli hiyo iliniumiza sana, ukitazama ni kweli nilitoweka nyumbani nikawa sionekani,” anasema Abdallah.

Baada ya simulizi ya Abdallah, Mwananchi ilimtafuta mama yake, Hidaya Ally ili kujua anaichukuliaje hali ya mwanawe na namna alivyomuibia pete hiyo.

Hidaya anakiri kuwa ni kweli mwanawe huyo alimuibia pete yake ya ndoa, hata hivyo anashamsamehe kwa sababu hakuwa anatambua alichokuwa akikitenda, kwani alikuwa akisukumwa na matumizi ya dawa za kulevya.

“Siyo pete tu, akiwa mraibu, Abdallah aliniibia vitu vyangu vingi zikiwemo pesa na simu. Alikuwa akirudi nyumbani, sipati amani kabisa. Ila sasa sijui kitu gani kilimtokea hadi akaamua kuacha kuzitumia, lakini nadhani kifo cha kaka yake kilichangia aachane na matumizi ya dawa hizo,” anasema Hidaya.

Mama huyo ameiomba Serikali kuongeza nguvu katika kutokomeza uuzaji na usambazaji wa dawa za kulevya, ili kuwalinda vijana na kuwanusuru ambao tayari wamekuwa waraibu.

Hata hivyo, Abdallah anasema mwaka 2019 kuna watu alikutana nao, walikuwa wakitoa elimu ya Methadone, hivyo aliamua kujiunga nao.

Anasema baada ya kujiunga katika kliniki ya Methadone Septemba 13, 2019, alianza matibabu aliyoyapata kwa miaka mitatu na alimaliza Julai 25, 2023.

Anasema hapo naye akaanza kazi ya ubalozi wa hiari wa kutoa elimu kwa vijana waraibu wa dawa za kulevya mitaani na akawa anawaunganisha na kliniki ya kituo cha tiba saidizi ya Methadone kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT) kwa kushirikiana na Shirika la ICAP Tanzania.

Anasema tangu mwaka 2023, amefanikiwa kuwasaidia waraibu wa dawa hizo zaidi ya 50 jijini Mwanza kwa kuwaunganisha na kliniki ya MAT iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekoutoure.

Meneja wa MAT iliyoko Hospitali ya Sekoutoure jijini Mwanza, Dk Meshack Samwel anasema alimpokea Abdallah akiwa amedhoofu mwili kutokana na matumizi ya dawa hizo, huku akidokeza kuwa kijana huyo amebadilika tangu alipomaliza tiba ya Methadone katika kituo hicho.

“Tulimpokea Abdallah akiwa katika hali mbaya, tulipofanya ufuatiliaji tukabaini kwamba ilifikia hatua akawa anachukua mali za nyumbani akauze, ili apate fedha ya kununua Heroine. Sasa hivi anaendelea vizuri na ameshaweza kujitegemea na kuanzisha familia yake na amekuwa balozi wetu,” anasema Dk Samwel.

Dk Samwel ambaye ni daktari bingwa wa afya na magonjwa ya akili, anasema kliniki hiyo imeshatoa huduma kwa waraibu 780 katika kipindi cha miaka mitatu, akiwemo Abdallah huku 350 kati yao wakiendelea na matibabu.

Kaimu mkuu wa afya za kinga za VVU kutoka Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) nchini, Dk Nyagonde Nyagonde anasema kituo hicho kinashirikiana na Serikali kupitia Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kutoa msaada wa matibabu kwa waraibu ambao wamepata maambukizi ya VVU.

“Jitihada za kuwasaidia waraibu zinahitaji ushirikiano baina ya Serikali na wadau binafsi, ndiyo maana tunahakikisha hakuna upungufu wa dawa za Methadone na hata wale ambao wanakutwa na maambukizi ya VVU ama Homa ya Ini, wanatibiwa na kurejea katika utimamu wa mwili,” anasema Dk Nyagonde.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, takwimu za mwaka 2020 zinaonyesha ongezeko la waraibu wa dawa za kulevya na vilevi kutoka watu 169,269 hadi waraibu 854,134 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 78 (666,225) ya watumiaji wa dawa hizo wenye umri wa miaka kati ya 15 hadi 35.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau wamefanikisha uanzishwaji wa vituo 16 vya tiba ya Methadone nchini ambapo waraibu zaidi ya 16,460 wanaendelea na matibabu katika vituo hivyo, wakiwemo wanawake na wanaume. Pia watu 56 wanapatiwa huduma katika nyumba za huduma ya matibabu ya dawa za kulevya (Sobber house) nchini,” anasema Mtanda.

Related Posts

en English sw Swahili