HATIMAYE Simba Queens imekamilisha usajili wa viungo wawili wa Yanga raia wa Nigeria, Precious Christopher na Saiki Atinuke kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Wachezaji hao wawili wamecheza Yanga kwa misimu miwili wakisajiliwa Septemba 2022, Precious ambaye ni kiungo mshambuliaji na Saiki anayemudu kucheza kiungo mkabaji.
Viungo hao wako huru kwa sasa baada ya kumaliza mikataba na Yanga na inaelezwa tayari Simba wamemalizana nao.
Mmoja wa viongozi Simba (hakutaka jina litajwe) alisema wamekamilisha dili la wachezaji hao ambao ni matakwa ya kocha Mussa Mgosi.
“Kila kitu kimekamilika na jana wamesaini mkataba wa mwaka mmoja kwanza kama mambo yatakwenda tutawaongeza mwingine,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Tumewasajili kutokana na uzoefu wao kwenye michuano ya kimataifa na sisi msimu huu tutashiriki hivyo tunataka kufika mbali zaidi yaani fainali na kuchukua kombe.”
Kwenye mechi 18 za Ligi, Precious amefunga mabao matatu huku Saiki akifunga bao moja.
Ikumbukwe Simba inauhitaji kwenye eneo la kiungo mshambuliaji ambalo inaamini kumsajili Precious itakuwa imelamba dume kutokana na uwezo wake wa kuchezesha timu na kupiga pasi sahihi ilhali pia akitumia mguu wa kushoto.
Kwa upande wa Saiki litakuwa chaguo sahihi kwenda kusaidiana na Vivian Corazone ambaye inadaiwa lengo la Simba ni kuleta ushindani kwenye eneo hilo.