KLABU ya KMC imekamilisha uhamisho wa aliyekuwa beki wa kati wa KVZ ya Zanzibar, Salum Athuman ‘Stopper’ baada ya nyota huyo aliyekuwa pia anawindwa na Simba kuamua kujiunga na miamba hiyo ya Kinondoni kwa mkataba wa miaka miwili.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimeliambia Mwanaspoti kwamba, beki huyo tayari amekamilisha uhamisho wake na wakati wowote kuanzia sasa atatambulishwa katika kikosi hicho baada ya viongozi kukamilisha kila kitu ikiwemo kukubaliana maslahi binafsi.
“Ni kweli amekamilisha uhamisho wake na KVZ tayari wamemtakia kila heri katika changamoto yake mpya. Ni mchezaji mzuri ambaye naamini kwa uwezo alionao atakuwa msaada mkubwa kwenye kikosi hicho,” alisema mmoja wa marafiki wa mchezaji huyo.
Hata hivyo, kocha mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin alisema hawezi kuelezea juu ya nyota wanaowataka kwa sababu lolote linaweza kutokea isipokuwa watafanya uhamisho wa wachezaji wazuri kutokana na upungufu uliojitokeza kwa msimu uliopita.
“Ni mapema sana ndugu yangu kuzungumzia hilo ila tutafanya usajili kutokana na upungufu uliojitokeza, naamini utakuwa ni wenye tija kwa sababu tumefanyia tathimini ya kikosi kizima na kugundua tunatakiwa kuongeza nguvu maeneo gani,” alisema.
Stopper ambaye ni zao la timu ya vijana ya Simba amekuwa na kiwango bora akiwa na KVZ huku ikielezwa kwamba mwanzoni mabosi wa Msimbazi walimfuatilia wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na ile ya Muungano iliyofanyika mwaka huu huko Zanzibar.
Nyota huyo amewahi kupita katika timu za Fountain Gate inayokipiga katika Ligi ya Championship kama sehemu ya makuzi katika safari yake ya ubora na baadaye alijiunga na JKT Tanzania, Mbeya Kwanza kisha kutimkia Zanzibar alikoonyesha kiwango bora kilichoivutia KMC.
Uhamisho huo unakuwa ni wa pili kwa KMC katika dirisha hili la usajili tangu lilipofunguliwa Juni 15, mwaka huu, baada ya kumtangaza aliyekuwa beki wa kulia wa Mtibwa Sugar, Nickson Mosha aliyejiunga na timu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu.