MIONGONI mwa wachezaji wanaolijua lango vizuri kwa upande wa soka la wanawake, Opah Clement yupo kwenye listi hiyo.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba Queens kwa sasa anaichezea klabu ya Besiktas inayoshiriki Ligi Kuu ya wanawake nchini Uturuki na ndio nahodha wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.
Hadi anaondoka nchini kujiunga na klabu ya Kayserispor ya Uturuki katika msimu wa 2021/2022 alikuwa amefunga mabao tisa, wakati msimu uliotangulia wa 2020/2021 alitisha sana akiweka kambani mabao 34 katika Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara akiwa na Simba.
Katika mahojiano yake na Mwanaspoti mapema wiki hii, Opah amezungumzia maisha yake ya soka tangu anaanza na nje ya soka anavyoendesha biashara zake.
Kama ulikuwa hufahamu basi Simba Queens ilimuona Opah kutokea Kigoma akikipiga kwenye klabu ya Kigoma Sisters.
“Nilijiunga na Simba katika dirisha dogo la mwaka 2018 wakati huo bado nilikuwa na majeraha na nikawaeleza kuwa daktari kaniambia nimebakiza mwezi mmoja wa kuuguza majeraha wakasema haina shida,” anasema Opah na kuongeza:
“Nilipopona haikuwa rahisi kupata namba kutokana na wachezaji waliokuwa wanacheza walikuwa wazuri, nikajipa moyo ninaweza nikaaminiwa na kucheza kikosi cha kwanza.”
Kabla ya kujiunga na Simba, Opah alipita katika klabu mbalimbali ikiwemo Mbasko ya mkoani Mbeya, Evergreen ya Dar es Salaam na Kigoma Sisters.
Anasema kwenye familia yao yeye si mtu wa kwanza kucheza soka kwani wote wamecheza kwa miaka tofauti.
“Baba yangu mzazi, kaka zangu wote walicheza soka lakini sio la ushindani wakicheza mkoani Mbeya na kuna mdogo wangu anayenifuata na yeye pia anacheza kwa hiyo ni familia ya soka.
“Ukiachana na hao mama yangu pia alikuwa mchezaji wa netiboli na mara nyingi nilipokuwa mdogo baba alikuwa ananibeba na kwenda uwanjani ndipo nikaanza kupenda.”
Supastaa huyo anasema nje ya soka ana biashara ya OPAH BURGER ambayo anauza baga na juisi, na pia yuko mbioni kufungua duka la kuuza simu.
“Soka bado halijanilipa kwa kiasi kikubwa, lakini kwa kidogo tulichokipata tunajitahidi kujiwekeza kwenye biashara mbalimbali,” anasema na kuongeza:
“Biashara ya kuuza simu tutachanga na mmoja wa watu wangu wa karibu.”
Timu anayoichezea straika huyo msimu huu imemaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ikikusanya pointi 59 kwenye michezo 30.
Machi mwaka jana, Opah aliuzwa na klabu yake ya Simba Queens kwenda Besiktas ya Uturuki kwa mkataba wa mwaka mmoja ambao umeisha hivi karibuni na hapa anaeleza hatma yake.
“Ni kweli mkataba wangu umeisha lakini kwa sasa siwezi kusema chochote juu ya kuongeza mkataba, kuondoka au kubaki nasubiri ruhusa ya wakala wangu,” anasema.
Anasema kuhusu wachezaji wa kike kujiweka kiume hana majibu lakini kwa upande wake anapenda mitindo ndio maana hupendelea kujiweka jinsia ya kike.
“Napenda mitindo na kupendeza pia kwangu mimi ni mwanamke na haitabadilisha kitu na kuhusu wachezaji wanaojiweka kiume sina komenti yoyote.”
UHUSIANO NA SANGA WA YANGA
Kama lilivyo jina lake, Opah Clement Sanga jina linaloendana na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga enzi za Yusuf Manji, Clement Sanga alipoulizwa kama wana uhusiano na hapa anajibu kwa ufupi huku akicheka.
“Hee! Jamani makubwa haya, mimi ni Simba sasa haya ya Yanga yanatoka wapi tena? Sina mzazi aliyewahi kufanya kazi huko Yanga.”