Dar es Salaam. Ripoti ya awali ya vipimo kutoka kwa madaktari wa Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam, imeonyesha Edgar Mwakabela maarufu kama Sativa, amepata mpasuko wa taya zilizosagika, huku baadhi ya mifupa ikionekana na mipasuko midogo.
Sativa anayejishughulisha na biashara ya miamala ya fedha na michezo ya kubahatisha, alichukuliwa vipimo usiku wa kuamkia leo Jumapili, Juni 30, 2024 katika hospitali hiyo, akitokea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikofikia awali, akitokea mikoa ya Dodoma na Katavi.
Mwakabela anayedaiwa kutoweka Juni 23 na kupatikana Juni 27 katika pori la Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha mwilini, alionekana katika video fupi iliyosambaa katika mitandaoni ya kijamii akiomba msaada wa kupelekwa hospitalini huku akivuja damu na kulalamika maumivu makali kutokana na kipigo alichokipata.
Hata hivyo, baada ya kupatikana Sativa alipekelewa Kituo cha Afya Mpimbwe, kisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kwa huduma za kwanza, huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyanyi akitangaza kuanza uchunguzi dhidi ya tukio hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Juni 30, 2024 mratibu wa matibabu ya Sativa, Martin Masese maarufu ‘MMM’ amesema wameelezwa na madaktari kuwa ndugu yao ameonekana kuwa na alama za michubuko ya panga katika mikono yake.
“Alikuwa anapigwa mabapa ya mapanga, sasa kuna moja lilimpata katika mikono yake, lakini tunashukuru timu za madaktari wote waliompa huduma ya kwanza hadi tulipofikia hapa.
“Hivi ni vipimo na matokeo ya awali, lakini atafanyiwa vipimo vingine vikubwa, ili kujua kila alipoumia au anaposikia maumivu, hatimaye apate matibabu ya uhakika. Tunamshukuru Mungu hali yake inaendelea kuimarika kila kukicha,” amesema Masese.
Masese amesema timu ya madaktari wa Aga Khan inafanya kazi ya kuhakikisha Sativa anapata ahueni na kurudi katika hali ya kawaida.
Kwa mujibu wa Masese, baada ya kufikishwa Muhimbili Sativa alifanyiwa vipimo na madaktari mbalimbali wakiwemo watalaamu wa meno, lakini baada ya mashauriano na ndugu pamoja na uongozi wa Muhimbili waliazimia kumhamishia Aga Khan.
Kuhusu gharama za matibabu, Masese amesema:”Ile michango au harambee tunayoifanya kupitia mitandao ya kijamii ndiyo inayowezesha matibabu ya Sativa, tunawashukuru Watanzania na wadau wanaoendelea kujitoa kuchangia, ili kufanikisha mchakato huu, naomba waendelea na moyo huu wasichoke.”
Juni 27, 2024 ndugu wa Sativa, Patrick Israel alisema katika harambee waliofanya walifanikiwa kupata zaidi ya Sh 10 milioni zilizochangwa na wadau mbalimbali, ili kufanikisha matibabu wa Mwakabela, akiwaomba Watanzania kujitoa zaidi katika mchakato huo.
Leo Jumapili, Israel ameliambia Mwananchi kuwa wanamshukuru Mungu kwa Sativa kufika salama Dar es Salaam, akisema hawezi kuzungumza kwa kirefu zaidi kuhusu mwenendo wa matibabu ya mgonjwa huyo hadi atakapokutana na ndugu zake katika vikao.