Mapya ya Dk Nawanda na tuhuma za ulawiti mwanafunzi wa chuo

Dar es Salaam. Ukimya wa taarifa za mwenendo wa tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (RC), Dk Yahaya Nawanda umewashtua wadau wa sheria, wakitaka upelelezi uharakishwe ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani.

Msisitizo wa wataalamu hao wa taaluma ya sheria, unatokana na kile walichofafanua kuwa ni mahakama pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuamua iwapo mtuhumiwa ana hatia au vinginevyo.

Mzizi wa hoja za wadau hao ni ukimya uliotawala katika mwenendo wa ushughulikiwaji wa tuhuma za Dk Nawanda tangu Jeshi la Polisi lilipotangaza kumkamata Juni 13, 2024.

Dk Nawanda anatuhumiwa kumlawiti mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) mkoani Mwanza.

Katikati ya taarifa hizo zilizoibua mijadala mitandaoni, Juni 11, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan alitengua uteuzi wake wa ukuu wa mkoa na nafasi yake kurithiwa na Kenani Kihongosi.

Taarifa ya Juni 13,2024 ndiyo ilikuwa ya mwisho kwa Jeshi la Polisi kuitoa kwa umma, baada ya hapo hakuna mwendelezo wa taarifa yoyote na hata walipotafutwa mara kadhaa na Mwananchi ilikuwa vigumu kuzungumzia.

Mara ya mwisho Mwananchi ilizungumza na Msemaji wa jeshi hilo, David Misime Juni 20, 2024 kutaka kujua iwapo mtuhumiwa huyo anaendelea kushikiliwa mahabusu au yupo nje kwa dhamana, alijibu kwa ufupi, “Subirini.”

Hata hivyo, Mwananchi ina taarifa za uhakika kuwa Dk Nawanda yupo nje kwa dhamana na bado hajapelekwa mahakamani hadi sasa.

Hatua hiyo imewatia wasiwasi wadau hao, wakidhani kunaweza kutokea masuala ya kesi kumalizwa kifamilia.

Msingi wa hofu za wadau hao ni kuwepo kwa tabia za kesi zinazohusisha ulawiti ama ubakaji kumalizwa kifamilia, kama ilivyowahi kuelezwa katika ripoti ya utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na watoto (UNICEF) mwaka 2017.

Utafiti huo unabainisha kesi nyingi za ukatili wa kingono dhidi ya watoto humalizwa katika mazingira ya nyumbani.

Nayo Ripoti ya Haki za Binadamu kwa Mwaka 2022 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mapema mwaka 2023 ilitaja “utamaduni wa kusameheana” na “kuficha aibu ya familia” kama moja ya sababu zinazochochea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto Tanzania.

Hata hivyo, tathmini ya LHRC, ilibinisha kati ya kesi 100 za ulawiti na ubakaji zinazoripotiwa polisi, ni 15 pekee ndiyo hufikishwa mahakamani.

Ingawa hatua ya mtuhumiwa huyo kuwa nje kwa dhamana ni haki yake, kulipaswa kutolewa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa kesi yake kama inavyoelezwa na Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe.

Amesema kama yupo nje ilipaswa kueleza kila hatua inayofikiwa kuhusu tuhuma zake.

Kwanini ni muhimu taarifa hizo kutolewa, Massawe amesema kwa sababu mtuhumiwa ni mtu maarufu na alikuwa kiongozi mkubwa serikalini, hivyo jamii inastahili kuarifiwa hatua zote.

“Ujue mkuu wa mkoa ni mwakilishi wa Rais katika ngazi ya mkoa, ni kiongozi mkubwa na mwenendo wa kesi anayotuhumiwa nayo ulipaswa kutolewa taarifa kila hatua,” amesisitiza.

Pamoja na mtazamo wake huo, Massawe amependekeza kuharakishwa kwa upelelezi, ili kama mtuhumiwa ana hatia afikishwe mahakamani kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.

Kwa upande wake, mtaalamu wa masuala ya sheria, Frank Chundu ameelekeza hoja yake katika changamoto za upelelezi, akisema ni hatua ambayo kwa Tanzania haina kikomo, hivyo kusababisha mamlaka zinazohusika zisione haja ya kuharakisha.

Utaratibu huo, amesema unasababisha kutotendwa haki akifafanua katika baadhi kesi watuhumiwa wanawekwa mahabusu muda mrefu.

“Kwenye hili, jamii inahitaji kujua kinachoendelea, bado Polisi hawaoni kama wana wajibu wa kufanya uchunguzi na upelelezi haraka,” amesema.

Kwa mujibu wa wakili huyo, kesi hiyo inafuatiliwa na jamii ili kujua iwapo haki inatendeka kwa makundi yote, yaani wananchi na hata viongozi.

“Polisi kama kawaida yao kwenye mambo yanayowahitaji wafanye uchunguzi wamekuwa wazito kuchukua hatua na hiyo si kesi moja ni nyingi,” amesema.

Kwa kadri upelelezi unavyochelewa, ameeleza ndivyo makali ya kesi yanavyopungua.

Hata hivyo, amesema ingawa sheria haijaweka ukomo wa upelelezi, Jeshi la Polisi linawajibika kufanya uchunguzi kwa wakati kama msingi wa utendaji haki.

“Mahakama ndiyo inayopaswa kuamua kwamba ametenda au hajatenda, hakuna sababu ya Polisi kuendelea kukaa na mtuhumiwa au aendelee kuripoti kwao kama kawaida. Watu wameathirika wanataka kuona haki ikitendeka,” amesema.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema kwa sababu taarifa ya awali ilihusisha tuhuma zilizokuwa wazi na mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kuamua ama za kweli au vinginevyo.

Kwa sababu hiyo, Ole Ngurumwa ametaka kesi ifikishwe mahakamani, ili ijulikane kama tuhuma dhidi ya Dk Nawanda ni za kweli au hapana.

“Kitendo cha kutaka kumalizia kesi bila kwenda mahakamani ni kuvunja utaratibu wa utawala wa sheria,” amesema.

Mtaalamu mwingine wa masuala ya sheria, Hekima Mwasipu amesema kukosekana ukomo wa muda wa upelelezi katika makosa ya jinai, kusifanye Polisi washindwe kutimiza wajibu wao wa kukamilisha uchunguzi.

Kwa sababu jeshi hilo kwa sasa lina vifaa vya kisayansi, ametaka upelelezi ufanywe haraka, ili kuhitimisha jambo hilo.

Hata hivyo, wakili huyo ameonyesha mashaka katika kuchelewa kwa upelelezi huo, kwa kile alichoeleza inawezekanaje uchelewe ilhali aliyefanyiwa yupo.

“Hata Rais Samia Suluhu Hassan wakati anapokea ripoti ya Tume ya Haki Jinai alieleza suala la upelelezi limekuwa changamoto, nafikiri ni wakati wa kufanyia kazi mapendekezo ya ripoti ili kutatua hizi kasoro zilizopo wazi,” amesema.

Kwa mujibu wa Wakili Mwasipu, inashangaza kesi zilizopo wazi zinachukua muda mrefu kama zile ambazo ushahidi wake umejificha.

“Hapa tunakuwa hatutendi haki kwa wale ambao wanakuwa wametendewa hayo makosa,” amesema wakili huyo.

Mwanaharakati wa haki za binadamu, Dk Ananilea Nkya amesema kwa kadri Polisi wanavyochelewa kumpeleka mahakamani wanasababisha umma uamini sheria zimetungwa kwa ajili ya wananchi mafukara na si viongozi.

“Polisi wanavyoendelea kuchelewesha kumpeleka mahakamani umma unachikilia kwamba Sheria zimetungwa kwa ajili ya wananchi mafukara na siyo viongozi,” amesema.

Amesisitiza sheria inapaswa kuchukua mkondo wake maana kosa lililofanywa ni jinai.

“Kosa la jinai ni kosa dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo polisi wanatakiwa kumfikisha mahakamani haraka iwezekanavyo,” amesisitiza.

Related Posts