KIPINDI cha mavuno kwa wachezaji na mawakala au mameneja wao ndio kinaendelea duniani kote kwa sasa baada ya msimu wa soka wa 2023/24 kumalizika, hivyo kuruhusu wachezaji waanze kuangalia wapi kuna majani ya kijani zaidi.
Lakini wapo wanaouguzia machungu ya kusaini mikataba kiholela baada ya kuhakikishiwa malipo mazuri ya bonasi ya kusaini (sign-on fee), mshahara mnono na bonasi nyingine za mechi na za mwisho wa msimu na hivyo kupuuza vipengele vingine vinavyohusu maisha yao ya baadaye.
Wapo ambao wameona konde zuri nje ya klabu walizopo sasa, lakini mikataba yao ina vipengele ama vya kununua mkataba (buyout clause) au vile vya masharti ya kuachiwa kuondoka (release clause).
Kwa kawaida kipengele kinachohusu masharti ya mchezaji kwenda timu nyingine (release clause), huhusisha pande zote mbili, yaani mchezaji na klabu kukubaliana ni kiasi cha chini cha fedha ambacho kitatakiwa na klabu inayommiliki ili iweze kumruhusu aanze mazungumzo na klabu inayomtaka.
Yaani kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesajiliwa Yanga kwa miaka mitatu na imetokea Azam FC inamtaka ndani ya muda huo, basi itaweka kiasi cha fedha ambacho mchezaji huyo amekubaliana na Yanga kwamba kikifikiwa (unaweza kutaja kuwa ni Sh200 milioni) klabu imruhusu kuanza mazungumzo na muajiri mtarajiwa.
Lakini kuna kipengele kingine cha kununua mkataba (buyout clause) na hii hufanyika sana Hispania. Chini ya kipengele hicho klabu huweka kiwango cha juu cha fedha kwa lengo la kuzuia klabu kumfuata mchezaji wake inayoona kuwa ni lulu. Klabu nyingine inayoona kuwa inaweza kufikia kiwango hicho, huwasiliana na mchezaji ambaye hulipa fedha zilizowekwa kama sharti la kuondoka na hivyo kuwa huru kwenda klabu inayomtaka.
Ligi kama za England, Ujerumani na Italia hazitumii kipengele hicho na badala yake zina release clause ambayo humpa uhuru mchezaji kushiriki kupanga ada ya kununuliwa na klabu inayomtaka na yenye uwepo wa kufanya malipo hayo.
Matukio ya Fei Toto na Prince Dube yaliibua mijadala kuhusu uhalali wa wachezaji hao kuamua kuondoka kwenye timu zao za Yanga na Azam, wakati msimu ukiendelea kwa madai kuwa hawataweza kuendelea kuchezea klabu hizo kwa sababu tofauti.
Lakini nia yao ya kuondoka ilikwamishwa na kipengele cha buyout clause, kununua mkataba, baada ya klabu hizo kuweka kiwango cha juu, huku kwa Fei akizuiwa na kanuni za uhamisho za Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) zinazotaka kuwa na sababu za kimpira za kuachana na klabu ndani ya mkataba.
Hata hivyo, bado kiwango alichowekewa Fei Toto kilikuwa kikubwa kulinganisha na muda wa mkataba wake, hali kadhalika kile kilichowekwa kwenye mkataba wa Dube.
Haijulikani nini kimo katika mikataba ya wachezaji wengine. Huenda kikawa kikubwa kuliko wawili hao.
Ni katika matukio kama haya, mamlaka husika huibuka na kutafuta dawa ya kupunguza tatizo linaloweza kuzuia mchezaji kwenda kuuza nguvu kazi yake kwingine alikoona kuna majani ya kijani zaidi au mazingira mazuri zaidi kimpira.
Ndio, kuna kanuni za Fifa zinazoongoza masuala hayo yote, lakini kama nchi ni lazima tuwe na miongozo yetu inayoendana na utamaduni na hali yetu ya kiuchumi. Kwa mchezaji mzuri ambaye anaona mazingira ya kuendelea kucheza Yanga si mazuri kulinganisha na mazingira ambayo anayaona Tabora United, itakuwa vigumu kwake kuruhusiwa kama ujio wake kwenye klabu ulilazimisha awekewe buyout clause kubwa.
Na mawazo yangu kuwa donge la Sh200 milioni ambalo anaweza kuwekewa mchezaji huyo kwenye mkataba wake litakuwa gumu sana kwa Tabora United kulimudu. Zaidi ya hayo litakuwa limemzuia mchezaji kwenda kuuza nguvu kazi yake sehemu anayoona ni bora kwake.
Kwa England, mchezaji ambaye anawekewa kikwazo kikubwa kwenye mkataba wake, huweza kwenda mahakamani kushtaki kuwa klabu inazuia uhuru wa kuuza nguvu kazi utakako na akasikilizwa na kushinda.
Kwa hiyo ni wakati sasa mamlaka husika za soka zianze kutengeneza kanuni za kuongoza uwekaji vipengele kwenye mikataba kwa lengo la kuulinda mpira na kulinda ushindani ambao ndio huvuta mashabiki, wawekezaji na wadhamini. Kanuni hizo hazitakiwi zitofautiane na za Fifa, bali ziakisi mazingira yetu na zinufaishe klabu na wachezaji.
Ndio maana pamoja na kwamba nchi za Ulaya ziko katika Jumuiya ya Ulaya na hivyo kutumia sheria moja kama ilivyokuwa wakati Jean Marc Bosman aliposhinda kesi ya kupinga kuzuiwa kuondoka baada ya kumaliza mkataba na ushindi wake, kuwa neema kwa wachezaji wote barani Ulaya tu, bado zinatofautiana katika kanuni za ndani ya nchi.
Ndio maana leo hii England wanafikiria kuanzisha kiwango cha juu cha mishahara kwa wachezaji, wakati nchi nyingine zinafanya hilohilo kwa kutumia kanuni tofauti za fedha.
Tunahitaji kuongoza haya mambo ya maslahi ya wachezaji na malipo ya ada ili kuwe na hoja za kuweza kuthibitisha kiwango kinachowekwa kama sharti la mchezaji kuondoka. Yaani klabu ilikokotoaje hadi kuweka sharti la malipo ya Sh1 bilioni katika mkataba wa mchezaji ili aweze kuondoka.
Tunahitaji kiwango cha kufikiri cha aina hiyo ili tuulinde mpira wetu dhidi ya uwezekano wa kupoteza mvuto na kuwa ligi ya timu mbili kama ile ya Scotland, ambako kuna Celtic na Rangers miaka yote.