Banda asikilizia Qatar, Sauzi na Tanzania

BEKI Mtanzania aliyekuwa akikipiga katika klabu ya Richards Bay ya Afrika Kusini, Abdi Banda amesema kwa sasa anahitaji kusaka changamoto mpya ya ushindani katika timu nyingine.

Banda amesema tayari ana ofa tatu mezani japokuwa hakutaja majina ya timu, ila Mwanaspoti linafahamu anazungumza na Singida Black Stars, timu kutoka Qatar na Afrika Kusini.

“Mkataba wangu uliisha mwishoni mwa mwezi uliopita, lakini nahitaji kwenda kucheza timu nyingine. Mazungumzo yanakwenda vizuri ya ofa nilizo nazo hadi sasa, hivyo lolote linaweza likatokea kikubwa naangalia maslahi,” amesema Banda, mchezaji wa timu ya Stars.

Alipoulizwa na Mwanaspoti kama anahitaji kurudi kucheza Ligi Kuu Bara? Nyota huyo amejibu: “Ningependa kucheza nje kwanza, ingawa huwa napenda kujipanga upya pindi nikiona mambo hayaendi sawa. Niliwahi kufanya hivyo msimu wa 2012/2022 nikasaini Mtibwa Sugar nilipoona nimekaa sawa nilikwenda kusaini Chippa United.”

Amesema kucheza kwake Afrika Kusini kwa muda mrefu  kummejenga kukabiliana na kila aina changamoto za nje na pia jinsi ya kuishi maisha ya huko.
  
Timu alizocheza Banda ni Coastal Union (2012–2014), Simba (2014–2017), Baroka (2017–2019), Highlands Park (2019/2020), TS Galaxy (2020), Mtibwa Sugar (2021/2022),  Chippa United (2022/2023) na Richards Bay (2023/24).

Related Posts