Mchungaji Msigwa, ambaye ni mbunge wa zamani wa jimbo la Iringa mjini kwa tiketi ya chama cha CHADEMA, na mwenyekiti wa chama hicho kanda ya Nyasa, alijiunga rasmi na CCM siku ya Jumapili, wakati chama hicho tawala kikiendesha kikao chake cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Kumekuwepo na minon’gono juu ya Msigwa kujiunga na chama hicho tangu aliposhindwa katika uchaguzi wa ndani ya CHADEMA huku akimshtumu mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, kwa kutumia mamlaka yake kuingilia mchakato wa demokrasia ndani ya chama kulazimisha watu anaowataka yeye.
Soma pia: Edward Lowassa: Mwanasiasa hodari au mwoga?
Wakati huo, DW ilijaribu kuzungumza na Mchungaji Msigwa kufuatia uvumi huo lakini alikataa kuzungumza au hakupokea simu. Na baadae CCM ilimkaribisha chamani mchungaji huyo ambaye alikuwa mmoja wa nguzo za CHADEMA na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama.
Katibu Mkuu wa CCM Dk. Emmanuel Nchimbi alimshika mkono Mchungaji Msigwa na kuingia naye ndani ya ukumbi ulikokuwa mkutano wa CCM, wakati wajumbe wa mkutano huo wakiimbia wimbo wa: ” Tuna imani na Samia…” huku wakiongeza vionjo vya kumkaribisha Msigwa.
“Mleeteee Msiigwa..mleete Msiiigwa..,” ndivyo alivyochagiza Rais Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa kikao hicho cha Halmashauri Kuu, ambacho kilihudhuriwa pia na viongozi wa juu wa chama, akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ally Mwinyi, na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdul-Rahman Kinana.
Ni aumuzi sahihi au ulafi na uroho?
Mchungaji Msigwa alishindwa kutetea nafasi yake ya mwenyekiti wa chama kanda ya Nyasa baada ya kushindwa na Joseph Mbilinyi, maarufuku kama Sugu kwa tofauti ya kura mbili tu, katika uchaguzi wa ndani uliofanyika Mei 29, 2024.
Pamoja na kushindwa, Msigwa aliahidi kuendelea kukitumikia chama cha CHADEMA, akisema hakuingia chamani kwa ajili ya nafasi za uongozi.
Msigwa amekuwa akitiliwa mashaka na wenzake ndani ya CHADEMA tangu wakati huo, wakimshuku kupanga kukiacha chama na kumpa majina ya kejeli kama vile “Yuda Eskarioti.”
Soma pia:Je, ndio machweo ya chama kikongwe Tanzania?
Kwenye mitandao ya kijamii ya DW, watumiaji wamekuwa na maoni tofauti kuhusu hatua ya Msigwa kujiunga na chama cha CCM, baadhi wakimpongeza huku wengine wakikosoa kile walichokiita ulafi na uroho wa wanasiasa.
“Kweli wanasiasa lao moja na ndio maana nasema kila siku Watanzania nchi hii ni yetu, hawa watu wanatafuta kula zao tu ni wahuni tu, tutaamue tuipiganie nchi yetu au tubakie na taabu zetu,” aliandika Melkizedeck Dismas Kimario, kwenye ukurasa wa Facebook wa DW.
Amanyisye Mbogoso Mchungaji alisema “Dunia inapitia changamoto kubwa ya kuwa na watu wadhaifu na wanafiki na wasioweza kusimamia wanachokiamini.”
“Tunaomba viondolewe vyama vingine vyote havina maana yoyote vinalitia tu hasara taifa, tunaandaa bajeti kubwa kwenye uchaguzi ili hali tunajua hatuna mfumo wa vyama vingi,” alisema mtumiaji mwingine wa Facebook aliejitambulisha kwa jina la Rwanda Magere.
Kinachowavutia wapinzani CCM
Vyama vya upinzani nchini Tanzania vimekuwa vikipambana kurejesha makali yake tangu kukumbwa na rungu la aliekuwa rais wa taifa hilo kati ya 2015 na 2020, John Pombe Magufuli, ambaye alipiga marufuku mikutano wa hadhara kabla ya uchaguzi na hasa baada ya uchaguzi wa 2020, ambapo vyama hivyo vilipoteza karibu katika majimbo yote na hivyo kukifanya Chama Cha Mapinduzi kuwa chenye uwakilishi mkubwa zaidi bungeni.
Soma pia: Lissu asema hatambui matokeo ya udanganyifu
Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani alianzisha mchakato wa maridhiano na vyama vya upinzani, ambapo aliruhusu tena kufanyika kwa mikutano ya hadhara kutekeleza hatua kadhaa za kuimarisha demokrasia ndani ya taifa hilo la Afrika Mashariki.
Lakini mpaka sasa bado imekuwa vigumu kwa vyama vya upinzani kuweka sawa nguvu yao kufuatia hali ngumu ya kifedha kutokana na kukosa kiasi kikubwa cha ruzuku baada ya kukosa uwakilishi wa kutosha bungeni, lakini pia malumbano ndani ya vyama hivyo yanayopelekea baadhi ya wanachama kuamua kujiondoa na kujiunga na vyama vingine, hasa chama tawala, CCM.