Watoto 53 wa Arusha kufanyiwa upasuaji wa moyo JKCI, Rais Samia kugharamia

Arusha. Wagonjwa wa moyo 236 wamepewa rufaa kwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa ajili ya matibabu ya moyo ikiwemo upasuaji.

Kati ya hao wamo watoto 53 ambao watafanyiwa upasuaji mkubwa na kuwekewa valvu za bandia.

Aidha, asilimia 40 ya wagonjwa zaidi ya 1,500 wa moyo waliofanyiwa uchunguzi, wamebainika kukutwa na matatizo ya umeme wa moyo.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Juni 30, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge alipozungumza na waandishi wa habari katika kambi ya matibabu ya madaktari bingwa, iliyodumu kwa siku saba katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Akitoa tathimini ya kambi hiyo katika kitengo cha moyo, Dk Kisenge amesema kuanzia Juni 24 hadi 30, mwaka huu , wamefanikiwa kutibu wagonjwa zaidi ya 1,500 na kati ya hao, asilimia 40 wamekutwa na matatizo ya umeme wa moyo.

“Kuna mgonjwa nimemkuta hakuwa anajijua kama ana tatizo, tulivyompima tumekuta mapigo yake ya  moyo yako  chini ya 39 na mwanadamu ili aweze kuishi anahitaji mapigo yaendelee kuanzia 60, huyu tumemkimbiza JKCI na kesho Jumatatu atawekewa mfumo wa umeme wa moyo,” amesema.

Dk Kisenge amesema kusingekuwa na kambi hiyo, mgonjwa huyo angekosa fursa ya matibabu na matokeo yake angefariki dunia ghafla.

Amesema watu wengi hupoteza maisha ghafla kutokana na tatizo hilo na wengi hufia usingizini.

Kuhusu waliopewa rufaa, Mkurugenzi huyo amesema kati ya wagonjwa 236, 183 ni watu wazima na wote wanaenda kutibiwa JKCI na gharama zote zitalipwa na Rais, Samia Suluhu Hassan.

“Pale kwenye Taasisi yetu kuna mtambo mkubwa wa kutibu umeme wa moyo na wagonjwa wote 183, Rais (Samia) amesema atawalipia gharama na tumeshaanza kutengeneza utaratibu ili wakifika wapate matibabu na kurejea,”amesema Dk Kisenge.

Kuhusu watoto, amesema wamewaona 150 ambao walikuwa na matatizo mbalimbali ya moyo na kati yao 53 wafanyiwa upasuaji mkubwa kwa sababu wana matatizo ya valvu za moyo.

“Valvu zao zilipata matatizo, hivyo hazifanyi kazi vizuri na damu inarudi, kama hawatafanyiwa upasuaji, hawatakua vizuri lakini pia ni rahisi kupoteza maisha mapema,” amesema daktari huyo.

Amesema kila upasuaji wa mtoto utagharimu Sh12 milioni.

“Watoto hao wote wanapelekwa JKCI na Rais Samia atalipia gharama hizo, upasuaji wa valvu unagharimu Sh12 milioni ni Watanzania wachache sana wanaoweza kumudu gharama hii, ila kutokana na kambi hii watapata matibabu bure. Nimpongeze sana Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa wazo hili la kuja na kambi hii,” amesema Dk Kisenge.

Amesema takwimu zinaonyesha duniani kote, karibu watu milioni 17 hupoteza maisha kutokana na magonjwa ya moyo.

Amewataka wananchi kubadili mfumo wa maisha ili kujiepusha na maradhi yasiyoambukiza kwa kufanya mazoezi, kuzingatia lishe bora, kupunguza matumizi ya tumbaku na unywaji wa pombe uliopitiliza.

Katika hatua nyingine Dk Kisenge amesema kuwa wapo katika mchakato wa kufungua tawi la JKCI mkoani Arusha  kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC).

Amesema mchakato huo unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu na kitatoa huduma kwa wananchi wa mikoa yote ya Kanda ya Kaskazini.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema tawi hilo litasaidia kupunguza gharama kwa wananchi wa mikoa hiyo ikiwamo ya gharama za kusafiri.

Makonda amesema wameongeza muda wa siku moja, awali kambi hiyo ilipangwa kukamilika leo Jumapili Juni 30, 2024 sasa itakamilika kesho Julai Mosi.

Makonda amesema wamefanya hivyo kwa sababu kuna baadhi ya sampuni za vipimo vya wagonjwa zilipelekwa nje ya Mkoa wa Arusha kwa uchunguzi.

“Itakuwa haina maana mwananchi amekuja tangu Alhamisi hadi leo halafu akose matibabu, na matibabu siyo suala la dakika moja kwamba umeingia pale na kutoka umetibiwa,” amesema.

Mmoja wa wanufaika wa kambi hiyo, Khamisi Iddy amesema huduma hiyo imesaidia watu wengi.

“Ila tunaomba kama itawezekana muda uongezwe au waje tena ili kila mwananchi anufaike na huduma hii muhimu ya afya,” amesema Iddy.

Ongezeko la magonjwa ya moyo nchini

Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani, yaliyofanyika Septemba 29, 2023 katika viwanja vya JKCI Hospitali ya Dar Group iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kumekuwapo na ongezeko la magonjwa ya moyo nchini.

Alisema takwimu za wizara hiyo kupitia Mtuha (DHIS-2) zinaonyesha kumekuwapo na ongezeko la asilimia 9.4 kwa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu pekee, kutoka wagonjwa milioni 2.5 mwaka 2017 hadi wagonjwa milioni 3.4 mwaka 2022.

Related Posts