Mwanza. Wadau mbalimbali jiji hapa wamependekeza suala la upatikanaji wa Katiba mpya lirejeshwe bungeni likajadiliwe upya ili kuruhusu mchakato uendelee.
Mapendekezo mengine ni kuitishwa kwa mkutano maalumu wa kitaifa wa kujadili Katiba mpya, kuunda timu ya wataalamu wa kuchukua maoni na mapendekezo yatakayotolewa katika mkutano huo, lakini pia kuandika rasimu mpya itakayotokana na maoni na mapendekezo ya wananchi yatakayotolewa katika mkutano huo, kisha kurejesha kwa wananchi kwa ajili ya kuupigia kura.
Mapendekezo hayo yalitolewa jana Juni 29, 2024 kwenye kongamano la Katiba lililofanyika katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza. Wamesema mapendekezo hayo yakizingatiwa yatasaidia kufanikisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya.
“Kwa kuwa mchakato umesimama mimi napendekeza hatua za kuufufua kwanza kwa muswada wa sheria inayoongoza mchakato wa Katiba mpya upelekwe tena bungeni ukarekebishwe,” amesema Deus Kibamba, Mjumbe wa Jukwaa la Katiba Tanzania.
Amesema hiyo itasaidia kuchora upya ramani ya kukamilisha mchakato huo na pili, kuitishwe mkutano mkuu wa kitaifa wa kujadili katiba na sharti liwe wabunge wasiwepo ila wawepo wawakilishi wa makundi mbalimbali kutoka kila mkoa nchini,” amesema Kibamba.
Amesema hatua ya tatu iundwe tume itakayokusanya na kuandika maoni na mapendekezo kwenye mkutano huo na hatua ya mwisho, tume hiyo iandike rasimu mpya itakayorudishwa tena kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura.
Akiunga mkono mapendekezo hayo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Dk Ananilea Nkya amesema ili katiba iwe nzuri, lazima izingatie mambo makubwa matatu ambayo ni demokrasia, namna bora ya usimamizi na uangalizi wa rasilimali za Taifa na ionyeshe mpango halisi, mazingira yanayofaa na utaratibu unaoweza kutoa vipaumbele katika huduma za jamii.
“Suala la demokrasia inayowezesha wananchi kujiamulia mambo yao wenyewe na pia kiongozi kuwajibika kwa wananchi haipo,” amesema Dk Nkya.
Naye mfanyakazi kutoka Shirika la Wavuvi katika Ziwa Victoria, Demai John amesema wanapendekeza Katiba mpya ionyeshe wajibu wa umma katika kuhifadhi ikolojia ya uvuvi ikiwemo mazalia ya samaki.
Wakiwakilisha kundi la watu wenye ulemavu, Hidaya Masoud na Jones George wamesema Katiba iliyopo bado haijatambua lugha ya alama, kitu ambacho kinasababisha kukosekana kwa huduma za muhimu kama za afya, elimu na ajira.
“Katiba yetu bado inatambua lugha mbili Kiingereza na Kiswahili kwamba ni rasmi, lakini lugha ya alama haitambuliki na haitumiki kwa ufasaha katika Serikali yetu, Katiba ya sasa haijasema wazi kwamba lugha ya alama itatumika wapi,” amesema Masoud.
Naye George ametolea mfano mtu mwenye ulemavu wa kusikia akienda hospitali na anakwama kupata huduma kwa sababu hakuna mtafasiri wa lugha ya alama.
“Lakini kundi hili wapo wanaosoma shule mpaka vyuo lakini wakifika kwenye ajira wanakwama kwa sababu ofisini hawatumii lugha ya alama,” amefafanua zaidi Hidaya.
Dk Nkya amesema Katiba iliyopo imempa mamlaka na madaraka makubwa ya Rais hali ambayo inasababisha Taifa kupata athari mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.
“Ibara ya 37 (1) ya katiba yetu inasema ‘Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote, isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu au mamlaka yoyote.”
Hata hivyo, amesema nchi inapaswa kuwa na katiba mpya ili kupunguza upotevu wa fedha na rasilimali ikiwamo Bunge kuwa na wabunge wengi wa viti maalumu ambao husababisha kutumia bajeti kubwa ilihali wananchi wanakosa huduma za msingi.
Sababu mchakato wa katiba mpya kukwama
Kibamba akizungumzia sababu ya mchakato wa katiba mpya kukwama tangu 2014 ni Bunge la katiba kuundwa vibaya hali iliyosabahisha kushindwa kupitisha katiba inayogusa masilahi yao.
“Mfano wabunge wasiwe wengi mno bungeni kwa sasa wapo 395 wakati rasimu hii inasema wabunge wachaguliwe kwenye majimbo 70 peke yake, kwa sasa yapo 264, mzee Joseph Warioba alitaka yapungue na kuwa 70 tu halafu kila jimbo wananchi wachague mwanamke na mwanaume ili kuleta usawa wa jinsia bungeni na viti maalumu vitafutika,” amesema Kibamba.