Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewateua makada wake 10 kuwania nafasi za uenyekiti wa mikoa na wilaya mbalimbali.
Nafasi hizo ni zile zilizoachwa wazi baada ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Nafasi zilizokuwa wazi ni ya uenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Shinyanga, kadhalika uenyekiti wa Jumuiya hiyo ya vijana Wilaya ya Misungwi.
Uteuzi wa majina ya makada hao, umefanyika leo Jumapili Juni 30, 2024 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).
Akizungumza na wanahabari baada ya kikao cha NEC, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema makada watatu wameteuliwa kuwania uenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora.
Amewataja walioteuliwa kuwania nafasi hiyo mkoani Tabora ni Saada Malunde, Said Mkumba na Athumani Mfutakamba.
Kwa upande wa uenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga, amesema walioteuliwa ni Irene Masakilija, Benard Werema, Makamba Lameck na Severine Mbullu.
Katika nafasi ya uenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Misungwi, amewataja walioteuliwa ni Emmanuel Masangwa, Anthony Masele na Medard Mwijage.
Sambamba na uteuzi wa majina ya makada hao, Makalla amesema kikao hicho kimemteua Rajab Abdallah kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Amesema Abdallah anarithi nafasi iliyoachwa wazi na Hassan Wakasuvi aliyefariki dunia.
Kwa mujibu wa Makalla, chama hicho kimeridhishwa na utendaji wa Rais Samia Suluhu Hassan, kadhalika Dk Hussein Ali Mwinyi visiwani Zanzibar.
“NEC imewapongeza Rais Samia na Dk Mwinyi kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/25 kwa mafanikio makubwa,” amesema.