Msimu wa 4 wa mashindano ya mpira wa Kikapu ya CRDB Bank Taifa Cup umehitimishwa siku ya Jumamosi jijini Dodoma katika viwanja vya Chinangali na ambapo mikoa ya Kigoma na Mara imeibuka kidedea kwa upande wa wanaume na wanawake.
Mgeni Rasmi katika fainali hizo alikua ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ambae amewashukuru ushirikiano wa Benki ya CRDB, TBF na Azam Media kwa kuchagua mashindano hayo yafanyike jijini Dodoma na kuchangia katika kukuza hamasa ya mchezo wa mpira wa kikapu jijini Dodoma.
Mbali na hilo, Mkuu wa Mkoa huyo ameshukuru mashindano hayo kuchangia uchumi wa Dodoma kwani zaidi ya vijana 500 wameshiriki michuano hiyo kwa siku 10.
Mashindano hayo yaliyoanza Juni 19 yakihusisha timu za mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani yalishuhudia timu ya Kigoma ya wanaume ikiibuka kidedea mbele ya wenyeji Dodoma.
Kwa upande wa wanawake timu ya Mara iliibuka kidedea dhidi ya Unguja ambao wamepoteza fainali mbili mfululizo ambapo mara ya mwisho walikutana na Dar es Salaam katika fainali zilizofanyika jijini Tanga.
Mashindano ya CRDB Bank Taifa Cup yanaratibiwa na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) huku Azam TV wakiwa pia wadhamini wenza ambao wameonyesha LIVE mashindano hayo kwa siku.
Mbali na zawadi za zaidi ya Shilingi Milioni 24 zilizotolewa kwa timu na wachezaji binafsi, mashindano ya CRDB Bank Taifa Cup yanatarajiwa kuendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa vijana takribani 20 wenye vipaji maalum katika mchezo wa mpira wa kikapu.
#CRDBBankTaifaCup2024
##NiZaidiYaGameNiMaisha