JIWE LA SIKU: Kwa usajili huu, Yanga 4-0 Simba

UHAMISHO na usajili wa wachezaji unaendelea tangu dirisha la usajili lilipofunguliwa Juni 15, mwaka huu. Katika Ligi Kuu Bara kila timu inasajili inavyojua huku timu pendwa zaidi za Simba na Yanga zikiendelea kutambiana kama ilivyo kawaida ya watani hao wa jadi.

Yanga inasajili lakini bado haijatambulisha mchezaji yeyote hadi sasa vivyo hivyo kwa Simba iliyosajili ambayo hadi sasa imemtambulisha beki wa kati Lameck Lawi ambaye uhamisho wake ulileta sintofahamu kubwa baada ya Coastal Union kudai haiutambui.

Leo mambo yanaweza kubadilika. Yanga itaanza kutambulisha wachezaji wake wapya kwa msimu ujao na Simba itaendelea ilipoishia kwa Lawi.

Hata hivyo, Mwanaspoti kupitia vyanzo vyake mbalimbali linajua klabu hizo zipo kwenye mazungumzo na wachezaji gani na zimefikia hatua gani.

Tayari Simba imewasajili winga Mzambia, Joshua Mutale kutoka Power Dynamos ya Zambia, straika Mganda, Steven Mukwala kutoka Asante Kotoko, Mburkina Faso, Valentino Nouma kutokea Lupopo, Yusuph Kagoma kutoka Singida na Omary Omary kutoka Mashujaa huku Augustine Okejepha, Debora Fernandez na Fasika Idumba wakiwa kwenye hatua za mwisho za kutua Msimbazi.

Yanga imemnasa mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube kutoka Azam, beki Mkongomani, Chadrack Boka kutoka Lupopo na kipa Khomeiny Abubakar kutoka Singida lakini ipo kwenye hatua nzuri pia ya kumpata Clatous Chama kutoka Simba na straika Mghana, Jonathan Sowah kutoka Al Nasr Benghaz ya Libya.

Hapo ndipo unapata picha kamili ya andiko hili lenye kichwa cha habari ‘Kwa usajili huu, Yanga 4-0 Simba’ kwa nini?

Ni wazi Simba na Yanga ni watani wa jadi ndani na nje ya uwanja na kinachochochea utani huo zaidi ni pale wanapokutana kwenye mechi ‘derby’.

Mfano msimu uliopita katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara Simba ilifungwa 5-1, na mchezo wa marudiano ikachapwa tena 2-1 jambo lililoipa Yanga nafasi ya kutamba na kuwatania zaidi watani wao hao kwani ilinyakua pia ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo.

Msimu mpya unaenda kuanza na wachezaji wapya watakuwa na timu hizo. Ukiangalia vita ya usajili inayotajwa kwa sasa utaona Yanga inaongoza kwa mabao manne mbele ya Simba licha ya kwamba mechi haijachezwa bado.

Katika wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba hadi sasa, hakuna hata mmoja amewahi kuifunga Yanga katika michuano yoyote ilhali wale wa Yanga, kuna Dube aliyeifunga Simba mara nne.

Hapo ndipo matokeo ya 4-0, yanakuja. Dube akiwa na Azam alikuwa mwiba mchungu kwa Simba. Amewafunga wekundu wa Msimbazi hao mara nne kwenye mashindano tofauti tangu amesajiliwa na matajiri hao wa Chamazi mwaka 2020 akitokea Highlanders ya kwao Zimbambwe.

Straika huyo alianza kuifunga Simba kwenye mechi ya Ligi Kuu msimu wa 2022/2023 katika mechi zote mbili akianza kwenye mchezo wa duru ya kwanza ambapo Azam ilishinda bao 1-0, lililopachikwa na Dube dakika ya 35 ya mechi hiyo iliyopigwa Oktoba 27, 2022.

Mzimbabwe huyo aliifunga Simba tena kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa msimu huo iliyopigwa Februari 21, 2023 akipachika bao dakika ya pili kabla ya Kibu Denis kuisawazishia Simba dakika ya 90 na mechi kumalizika kwa sare ya mabao 1-1.

Dube hakupoa mbele ya wekundu kwani Mei 7, mwaka jana timu hizo zilikutana kwenye nusu fainali ya FA na Dube kuifungia Azam bao la ushindi dakika ya 75 katika mchezo ambao Azam ilianza kwa kufunga katika dakika ya 22 kupitia kwa Lusajo Mwaikenda kisha Sadio Kanoute kuisawazishia Simba katika dakika ya 28 kisha Dube kufunga la pili na mchezo kuisha 2-1.

Wakati Simba ikijaribu kumsahau Dube, msimu uliopita katika mechi ya mzunguko wa kwanza aliwakumbusha tena uwepo wake kwa kuifungia Azam bao la kuongoza dakika ya 14 kabla ya Simba kusawazisha dakika ya 90 kupitia kwa Clatous Chama na mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Februari 9, mwaka huu na kumalizika kwa sare ya 1-1.

Pamoja na kuwa hivyo, lakini usajili siku zote umekuwa kama michezo ya kubahatisha. Matokeo ya usajili ni baada ya msimu kuanza hivyo kila timu ina nafasi ya kujipanga na kufanya vyema dhidi ya mwenzake pale ambapo miamba hiyo itakutana. Kutokuifunga timu hapo kabla hakumaanishi kwamba hauwezi kuifunga ukikutana nayo kwa mara ya kwanza. Hata Freddy Koublan licha ya kusajiliwa akiwa hajawahi kucheza dhidi ya Yanga hapo kabla, alipokutana nayo kwa mara ya kwanza akaifunga katika zile 2-1 za mechi ya marudiano ya Derby ya Kariakoo msimu ulioisha. Na vivyo hivyo kwa Joseph Guede ambaye aliifunga Simba katika mechi hiyo ambayo pia ilkuwa ndio yake ya kwanza dhidi yao Wekundu.

Kwa mara ya kwanza wakati Dube anatua nchini, msimu wa 2020/2021 alifunga jumla ya mabao 14 ya Ligi Kuu Bara katika michezo 23 aliyocheza huku msimu uliofuata wa 2021/2022 alifunga bao moja tu kwenye mechi 14 baada ya kuandamwa vibaya na majeraha.

Msimu wa 2022/2023, alicheza jumla ya michezo 26 ya Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi cha Azam FC ambapo alifunga mabao 14 huku msimu uliopita wa 2023/2024, alicheza mechi 12 na kufunga mabao saba kisha kuanza mgogoro wa kimkataba na waajiri wake.

Related Posts