Tunaanza upya 2024/25, mipango mikakati kambini

ILE siku iliyokuwa inasubiriwa na mashabiki wa soka hususan wale wa klabu zilizomaliza Nne Bora ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Yanga, Simba, Azam na Coastal Union imefika.

Klabu hizo zote zilitangaza kwamba leo, Jumatatu, ikiwa ni Julai Mosi ndio zinaanza rasmi mipango ya msimu ujao wa Ligi Kuu ikiwamo kuanza kukutana kambi za awali kabla ya kusafiri nje ya nchi kwa kambi za muda mrefu za maandalizi ya msimu wa 2024-2025.

Msimu mpya unatarajiwa kuanza Agosti 8-11 timu hizo zitakapocheza mechi za Ngao ya Jamii kabla ya ligi yenyewe kuamshwa rasmi kati ya Agosti 16-18 na leo kila kitu kinaanza upya kwa klabu hizo zitakazowakilisha nchi katika michuano ya kimataifa msimu ujao.

Ikumbukwe Yanga pamoja na Azam zilizomaliza nafasi mbili za juu zitaiwakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Simba na Coastal zilizomaliza nafasi ya tatu na nne mtawalia zitacheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Timu hizo tangu kumalizika kwa ligi ya msimu uliopita ziliweka bayana kwamba Julai Mosi ndipo zitaanza msimu mpya kwa maana ya kutangaza majina ya wachezaji kuacha na kushusha vifaa vipya sambamba na kuitisha kambi za awali zitakazoenda sambamba na upimaji wa afya za wachezaji wa vikosi hivyo.

Mabingwa hao wa msimu wa tatu mfululizo wa Ligi Kuu Bara kuanzia  leo wataanza kuingia kambini Avic Town, huku wakisikilizia tarehe rasmi ya kwenda nje ya nchi kuweka kambi maalumu ya msimu ujao.

Russia na Afrika Kusini ndiyo mataifa ambayo Yanga ipo nayo mezani ikisubiri kuamua tu wapi ikajichimbie kwa msimu ujao.

Tayari timu hiyo imeanza usajili kimya kimya lakini kuanzia  leo itaanza kutambulisha wachezaji wapya na kutoa ‘thank you’ kwa wale itakaoachana nao.

Inaelezwa kuwa Yanga ipo kwenye nafasi nzuri ya kuwasajili Clatous Chama aliyemaliza mkataba na Simba, Prince Dube aliyevunja mkataba na Azam, Chedrack Boka kutoka FC Lupopo na kipa Abubakar Khomeni kutoka Singida Black Stars.

Hata hivyo kina Skudu Makudubela, Zawadi Mauya na Augustine Okrah ni miongoni mwa wachezaji watakaopewa ‘thank you’.

Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kila kitu kitaanza leo, Julai Mosi.

“Ni muda wetu kufanya yetu. Kuanzia kesho (leo), kila kitu kuhusu maandalizi ya msimu mpya tutakiweka wazi. Usajili, kambi na maandalizi kwa ujumla vyote mtavipata kuanzia Jumatatu,” alisema Ahmed.

Wiki hii pia Azam inaingia kambini. Leo hadi Alhamisi utakuwa ni muda wa wachezaji kuwasili kambini na kufanyiwa vipimo sambamba na mambo mengine ya kiutawala, kisha Ijumaa itasafiri hadi Zanzibar kwa kambi fupi ya siku nane kabla ya Julai 14 kusafiri hadi Morocco kumalizia kambi.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Yusouph Dabo alisema ni maandalizi ambayo yatatoa picha kamili ya msimu ujao.

“Tunakwenda kuandaa timu itakayotupa tunachokitaka kwa msimu ujao. Lengo ni kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita na naamini itakuwa hivyo,” alisema Dabo.

Tayari Azam imesajili na kutangaza wachezaji wapya sita ambao ni Jhonier Blanco, Ever Meza, Yoro Mamadou Diaby, Franck Tiesse, Adam Adam na Saadun Nassoro.

Pia imeachana na Ayoub Lyanga, Daniel Amoah, Edward Manyama, Malickou Ndoye, Issa Ndala, Prince Dube huku ikimuuza Kipre Jr kwenda MC Alger ya Algeria na malengo kwa msimu ujao ni kutwaa ubingwa wa ligi na kuvuka makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wekundu wa Msimbazi nao hawajalala. Wanaendelea kujenga timu mpya, huku upepo kwa ishu ya makocha ukibadilika mara kwa mara, japo wachezaji wanaanza kukutana leo kambini kujiandaa na safari ya Misri watakakokita kambi katika mji wa Ismailia.

Hadi tunaingia mitamboni Simba ilikuwa ikifanya mazungumzo na makocha wawili kutoka Afrika Kusini, Steve Komphela na Davids Fadlu aliyekuwa kocha msaidizi wa Raja Casablanca, ili mmoja awahi kambi huko Misri.

Taarifa nyingine zinasema makocha hao wanaweza kuja wote mmoja akawa mkuu na mwingine msaidizi.

Mazungumzo hayo yanaendelea na huenda mmoja akatangazwa kuwa kocha mkuu ilhali mwingine akiwa msaidizi kutokana na mwafaka utakaofikiwa. Pia Juma Mgunda anadaiwa kuwa huenda akaendelea kuwepo kikosini.

Kwa upande wa wachezaji Simba imewasajili Lameck Lawi kutoka Coastal Union, Omary Omary aliyekuwa Mashujaa, Joshua Mutale kutoka Power Dyanamos na Steven Mukwala kutoka Asante Kotoko na wanatarajia kutambulishwa muda wowote huku ikiendelea na mazungumzo ya karibu na Debora Fernandez, Fasika Idumba na Augastine Okejepha.

Klabu hiyo imetangaza kuachana na nyota sita ambao ni Saidi Ntibazonkiza, John Bocco, Henock Inonga, Shaaban Chilunda, Kennedy Juma na Luis Miquissone, ilhali kipa Aisha Manula akitajwa kutolewa Azam kwa mkopo.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally aliwataka mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu kwani wanakwenda kuanza mwanzo mpya kwa kishindo.

“Mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi. Tunaenda kutengeneza Simba imara zaidi. Tutatangaza usajili, benchi la ufundi na kila kitu kinafanyiwa maboresho kwenye timu, lengo ikiwa ni kurejea kwenye ufalme wetu,” alisema Ahmed.

Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika sambamba na Simba nao wako bize jijini Tanga wakisuka mipango ya msimu ujao na leo wataanza kuweka wazi mipango waliyo nayo.

Tayari Coastal imewapa ‘thank you’ Roland Beakou, Ababakar Abbas, Omar Mbaruku, Felly Mulumba na kocha Fikirini Elias aliyetimkia Ken Gold na leo itaanza kutangaza jeshi lake jipya kwa ajili ya msimu ujao chini ya kocha Mkenya David Ouma.

“Tutafanya maboresho ya kikosi ili kuhakikisha tunafanya vizuri katika msimu ujao. Kuna wachezaji wataondoka ila tutasajili pia,” alisema Ouma.

Miongoni mwa timu ambazo Mwanaspoti limethibitisha kambi zao za msimu ujao zitakuwa wapi ni Singida BS, KMC na Mashujaa FC.

Timu hizo leo zitaingia kambini, KMC ikianzia Dar es Salaam na Mashujaa ikiwa Kigoma kisha kwa nyakati tofauti kila moja itavuka maji kwenda Zanzibar kwa maandalizi kamili ya msimu ujao, huku Singida itasalia mjini humo kabla ya Tanzania Prisons nayo kuanza Julai 7.

Ken Gold bado haijafahamika, japo inaelezwa ina mpango wa kujichimbia Mwakaleli, Tukuyu na kambi rasmi inatarajiwa kuanza Jumamosi wiki hii kwani kwa sasa zinashughulikiwa itifaki za kiuongozi ikiwemo kutambulisha kocha mpya.

Pamba Jiji imepanga kusalia Mwanza kama ilivyo Dodoma Jiji, huku Tabora Utd ikiwataka wachezaji kuanza kuripoti kambini leo japo haijataja kambi ilipo.

JKT Tanzania ina maeneo manne katika mipango ikiwa ni Dodoma, Dar es Salaam, Arusha na Zambia, lakini kila kitu kitaamuliwa kuanzia wiki hii hali kadhalika kwa Kagera Sugar yenye mipango ya kwenda Uganda, Rwanda au kusalia Bukoba.

Kwa Namungo na Fountain Gate mipango kamili ya msimu mpya itaanza rasmi kufanyika leo katika vikao ambavyo vitatoa uamuzi wa mambo yote kwa ujumla.

Related Posts