SAA chache tangu Azam FC itangaze kuridhia kumuachia Prince Dube baada ya Mzimbabwe huyo kuomba kuvunja mkataba ili awe huru, nyota huyo amefanya mahojiano mafupi na Mwanaspoti na kufunguka kuwa uamuzi aliouchukua kuiacha timu hiyo ni sahihi na kuwataka mashabiki wasubiri waone mambo msimu ujao.
Klabu ya Azam, ilitoa taarifa Ijumaa usiku kuwa imeridhia ombi la mchezaji huyo la kuvunja mkataba aliokuwa nao na klabu hiyo alilowasilisha kwa uongozi tangu Machi 2024.
Awali, nyota huyo alisusa kuitumikia timu hiyo mwanzoni mwa mwaka huu kwa alichodai amemaliza mkataba na klabu hiyo, lakini Azam ikamkomalia kwa madai ina mkataba naye hadi 2026 na kufikia pande hizo kufikishana katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kushtakiana katika Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ambayo ilikutana Aprili 18 na hukumu yake haikutangazwa rasmi hadi pande hizo ziliporidhiana.
Katika taarifa ya klabu hiyo, Azam imeweka wazi kwamba mshambuliaji huyo ametimiza matakwa ya kimkataba kama ambavyo imeanishwa kwenye vipengele vinavyoruhusu upande mmoja kuvunja mkataba, ikiwa na maana Mzimbabwe huyo kulipa fedha alizotakiwa ndio maana imemuachia aende atakako.
Sasa saa, chache baada ya Azam kutangaza imeachana na Dube, mshambuliaji hiyo aliyeifungia timu hiyo jumla ya mabao 33 ya Ligu Kuu Bara katika misimu minne aliyoitumikia, amesema alichokifanya ni sahihi na sasa anaenda kujifua ili kurudi na moto mpya kuthibitisha kuwa hakukosea kusepa Chamazi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Dube alisema amefurahishwa na waajiri wake wa zamani kumkubalia ombi lake la kusitisha mkataba, huku akikiri kuwa sasa ana hamu ya kurudi kucheza soka la ushindani.
Dube alisema ni muda wa kufanya kazi baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu tangu sakata hilo lilipoibuka miezi minne iliyopita.
“Kwanza namshukuru Mungu sana kwa jambo hili kumalizika salama, nilikuwa nasubiri kwa muda mrefu na kwa hamu uamuzi huu. Nawashukuru Azam kwa kukubaliana na ombi langu,” alisema Dube na kuongeza;
“Ni miezi minne sasa niko nje ya uwanja, ukweli ni kwamba nina hamu sana ya kurudi kucheza soka la ushindani, unapozoea kucheza soka na ikawa tofauti ukiwa huna matatizo yoyote ya afya ilikuwa inaniumiza sana, lakini kwa sasa mambo yamekwisha. Kinachofuata ni kujipanga tu, nataka kujiandaa vizuri ili nitakaporudi nithibitishe uwezo wangu.”
Dube alisema licha ya kuondoka Azam, lakini msimu ujao atacheza tena Ligi Kuu Bara ila suala la timu gani mashabiki wasubiri, kwani mpira ni mchezo wa wazi hawezi kujificha.
“Lilikuwa ni suala la muda, lakini nilikuwa katika wakati mgumu sana kusubiri uamuzi uliotolewa sasa nipo huru na tayari kwa kucheza, suala la mimi kuvunja mkataba sijashinikizwa na yeyote nimefanya nikiwa timamu na naamini kwangu ni uamuzi sahihi,” alisema Dube na kuongeza;
“Nimeishi vizuri Azam FC kwa misimu minne niliyoitumikia na kuamua kwangu kuondoka ni jambo ambalo nimelifanya kama ambavyo niliamua kusaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo.”
Japo, Dube hakutaka kuweka wazi timu gani ataitumikia kwa msimu ujao, lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa mshambuliaji huyo atajiunga na mabingwa wa soka nchini, Yanga ambao ameshasaini mkataba wa kuwatumikia.
Akizungumzia juu ya Ligi Kuu Bara alisema anatarajia ushindani mkubwa, kwani kabla ya kukaa nje ya uwanja kwa muda akipisha sakata lake limalizike tayari aliona ushindani kutokana na timu nyingi kufanya usajili mzuri.
“Msimu ulioisha ulikuwa bora na wa ushindani, timu nyingi zilikuwa bora na naamini msimu ujao mambo yatakuwa mazuri zaidi kulingana na sajili zinazoendelea, naamini timu itakayomalizana na mimi itakuwa bora pia,” alisema Dube aliyemaliza na mabao saba msimu uliopita na kuongeza kuwa, kwa vile kazi yake ni kufunga, basi anaamini ataendelea kufunga hata katika timu atakayojiunga nayo kulingana na nafasi atakazozipata.
Dube alianza kuzinguana na Azam mapema Februari mwaka huu alipogoma kwenda na timu mikoani kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu Bara, mechi ya kwanza kufanya hivyo ikiwa ni dhidi ya Tanzania Prisons iliyoisha kwa sare ya 1-1. Mechi hiyo ilipigwa Februari 25 kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Hata hivyo, ilipofika Machi aliwaaga Azam FC na kufuta kila kitu kuhusu klabu hiyo, ikielezwa pia alirudisha vitu vyote alivyokuwa akitumia kambini na kuhama jumla, ikielezwa alienda kufichwa na vigogo wanaotajwa kuwa wa Yanga ambayo ni klabu inayoelezwa anaipenda.
Staa huyo aliyekuwa akihusishwa na klabu kadhaa ikiwemo Al Hilal na Simba, alijulishwa na mabosi wa Azam kwamba kama anataka kuondoka, wao hawana tatizo ila ni lazima awalipe Dola 300,000 (zaidi ya Sh700 milioni), huku yeye akisema yu tayari kulipa Dola 200,000 (zaidi ya Sh500 Milioni) kabla ya kupelekana TFF.
Dube alikuwa akisisitiza kwamba mkataba wake ulikuwa ukimalizika mwishoni mwa msimu uliomalizika na sio 2026 kama Azam ilivyokuwa ikidai kwa maelezo ilimuongeza mpya na ilishaanza kumlipa mshahara wa mkataba huo, ndipo mambo yakaenda kumalizwa TFF na ikaelezwa Dube alichemka na kutakiwa kuilipa Azam kama alivyokuwa ameomba kuvunja mkataba aondoke klabuni hapo.
Ikaelezwa watu wa karibu na Yanga wamemhifadhi nyota huyo jijini Dar es Salaam na wameshampa ofa ya miaka miwili, wakimnunulia pia samani za ndani za Sh30 milioni na ulinzi mkali wa saa 24.
Kwenye taarifa yao waliyoitoa kuhusu Dube kuomba kuvunja mkataba, Azam walisema mkataba na mchezaji huyo utaisha 2026 na Mwanaspoti liliambiwa wanamuuza kwa Sh700 milioni. Yeye akawaomba awarudishie Sh500 milioni walizompa wakati wa usajili na wiki iliyopita kama tulivyoripoti jamaa akaingiza fedha na mara muamala uliposoma katika akaunti za Azam FC, wakamalizana kiroho safi.
Dube alijiunga na Azam, Agosti 2020, akitokea Highlanders ya Zimbabwe kwa kusaini mkataba wa miaka miwili hadi 2022. Mwaka mmoja baadaye, 2021, anasaini nyongeza ya mkataba hadi 2024.
Huu ndio mkataba ambao Dube alikuwa anadai kuutambua kabla mambo hayajabadilika. Lakini Azam walikuwa wanasisitiza mwaka jana nyota huyo wa kimataifa wa Zimbabwe alisaini tena mkataba hadi 2026. Huu ndiyo mkataba ambao Dube aliukana lakini mambo yakamuelemea kwenye ‘mahakama’ ya TFF.
Wakala wa Prince Dube, George Deda kutoka Zimbabwe awali alikuwa akikwepa kufafanua sakata la mteja wake hadi mambo yalipoisha na sasa Dube anajiandaa kuonekana tena Bara huku Yanga ikitajwa.
Kutua kwake Yanga inayoelezwa inajiandaa kumtambulisha muda wowote kunaenda kuiongezea makali safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ambayo msimu uliopita ilifunga jumla ya mabao 71 katika mechi 30 za Ligi Kuu na kutetea taji kwa msimu wa tatu mfululizo.
Safu ya mauaji ya Yanga iliongozwa na viungo Stephane Aziz KI aliyemaliza na mabao 21, Maxi Nzengeli aliyefunga mabao 11, Mudathir Yahya aliyefunga mabao tisa na Pacome Zouzoua aliyemaliza na mabao saba, huku Joseph Guede na Clement Mzize ambao ni washambuliaji kiasilia wakifunga mabao sita kila mmoja wakati straika Kennedy Musonda naye akifunga matano. Musonda na Guede wanatajwa kuwa kwenye mchakato ya mmoja wao kutemwa.