Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Mwenyekiti na Mfadhili wa Yanga, Yusuf Manji ambaye alifariki juzi Jumamosi anatarajiwa kuzikwa leo nchini Marekani.
Manji alifariki akiwa hospitalini Florida Marekani ikiwa ni miezi miwili tangu alipofanya mahojiano marefu na Mwananchi Dijital akiwa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo mtoto wa marehemu Mehbub Manji amelitumia Mwananchi inasema wao kama familia wanashukuru kwa jinsi ambavyo Watanzania wameendelea kuombeleza kifo cha baba yao na jinsi ambavyo wameendelea kumuombea huko alipo.
“Kama familia tunapenda kushukuru jinsi ambavyo watu wengi wakiwemo Watanzania wameendelea kuomboleza kifo cha baba yetu, tunashukuru sana kwa maombi yenu.
“Tunawaomba muendelee kumuombea baba yetu awe na safari njema huko aendapo. Alikuwa anaipenda Tanzania na Watanzania wanampenda sana, lakini tunaomba kuwaambia kuwa Manji atazikwa leo saa tisa alasiri Orlando, Florida Marekani, karibu na sehemu aliyozikwa baba yake. Baba tulikupenda lakini Allah amekupenda zaidi. Yusuf Manji: Ni baba, rafiki, kiongozi,” ilimalizia taarifa hiyo.
Manji ambaye aliingia madarakani siku chacha baada ya Yanga kuchapwa mabao 5-0 na Simba alikuwa mwenyekiti wa timu hiyo kwa kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2012 hadi 2017 na kufanikiwa kutwaa makombe manne ya Ligi Kuu Bara, Kombe moja la FA, Ngao ya Jamii na Kombe la Kagame huku akifanya usajili mkubwa wa mastaa kama Kelvin Yondan, Mbuyu Twite na Juma Kaseja.