Kilichowaponza vigogo wawili kusimamishwa kazi Dawasa

Dar es Salaam. Uamuzi wa kusimamishwa kazi kwa watendaji wawili wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), akiwemo Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Kiula Kingu umechochewa na sababu mbalimbali, ikiwemo ufuatiliaji duni wa miundombinu ya maji.

Kiula amesimamishwa jana Jumapili, Juni 30, 2024 pamoja na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji wa Dawasa, Shaban Mkwanywe kwa maelekezo ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kupisha uchunguzi wa utendaji usioridhisha na kusababisha kutopatikana kwa huduma ya maji katika eneo wanalolisimamia.

Mzizi wa kusimamishwa kwao ni ripoti iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mwajuma Waziri aliyoitoa mbele ya Waziri Aweso, wajumbe wa bodi, menejimenti na kamati ya siasa ya mkoa.

Ripoti hiyo ilitokana na ziara ya Mhandisi Mwajuma aliyoifanya katika maeneo mbalimbali ya mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu, Ruvu chini pamoja na bomba kuu linalosafirisha maji kutoka kwenye vyanzo hadi kwenye matenki.

Mhandisi Mwajuma alifanya ziara hiyo kwa siku mbili, ikiwa ni takribani wiki moja imepita tangu Mwananchi Digital iripoti hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam.

Habari hiyo ya uchunguzi iliangazia jinsi baadhi ya wakazi za jiji hilo wanavyopata adha ya upatikanaji wa huduma hiyo. Mathalani eneo la Msumi, Kata ya Mbezi ambako wananchi wanalazimika kutumia saruji kuyasafisha, ili kuweze kuyatumia.

Kadhia hiyo ilimfanya Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew kufanya ziara Machi 20, 2024 maeneo mbalimbali kujionea hali halisi ya upatikanaji wa maji akieleza ameagizwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Jana Jumapili, Waziri Aweso naye alifanya ziara Dawasa. Kabla ya kutoa ripoti hiyo, Aweso alitembelea maeneo ya tenki la Chuo Kikuu cha Ardhi, Luguruni, Mshikamano na Tegeta A. Timu nyingine ikiongozwa na wajumbe wa bodi walikwenda maeneo ya Kigamboni.

Baada ya kurejea, kilifanyika kikao cha ndani, kisha baadaye wakaingia ukumbini na Mhandisi Mwajuma akawasilisha ripoti ya kile alichokibaini kwenye ziara yake.

“Nilianza Ruvu Juu sehemu ambayo kwa siku inapaswa kuzalisha lita miloni 180, nilikuta baadhi ya pampu hazifanyi kazi na maji mengi yakimwagika chini na nilijiuliza tunapataje lita milioni 180,” amesema.

Amesema pia alikagua bomba kuu linalotoa maji kusafirisha hadi kwenye matenki, akabaini kuna sehemu kulipaswa kufungwa ‘flow mitter’ zinazoonyesha kiwango cha maji, lakini zimetolewa na baadhi ya watu wameanzisha makazi.

“Inaonekana hakuna anayechukua hatua ya kufuatilia maeneo hayo na baadhi ya chemba maji mengi yanapotea, hali hiyo si kwenye bomba kuu hata huku mijini chemba hizo watu wamegeuza visima,” amesema.

Katibu mkuu huyo amesema walifika baadhi ya maeneo watu wameanzisha mashamba ya umwagiliaji wakitumia maji ya taasisi hiyo na baada ya kuwaona wakifanya shughuli hizo, walikimbia.

“Eneo la Sinza Mugabe kuna chemba watu hadi wamegeuza kisima, sehemu ya kuchota maji kwa matumizi yao binafsi na hakuna hatua zilizochulia,” amesema

Uwekezaji wa Serikali na hali ya mitambo, amesema ilivyo katika mtambo wa Ruvu Chini wanatakiwa kuzalisha lita milioni 260 kwa siku, lakini pampu zake nyingine hazifanyi kazi.

“Serikali imefanya uwekezaji unaotakiwa kuzalisha lita milioni 590, kwa siku lakini ukiangalia taarifa ya miezi sita ya vyanzo vyotem, ikiwemo Kigamboni kwa siku tunazalisha lita milioni 320 manake tunadaiwa lita milioni 270 kufikia 590,” amesema.

Amesema katika lita hizo milioni 320 wanazozalisha kwa siku wanauza lita milioni 210 kulingana na taarifa waliyoingiza miezi sita iliyopita manake wanapoteza lita milioni 110.

“Tukipiga mahesabu kiwango cha lita milioni 279 wanachodaiwa na kuongeza lita milioni 110 wanazopoteza kama zingekuwa zinapatikana tungeweza kuhudumia idadi ya wananchi milioni sita,” amesema.

Katibu huyo amesema baada ya kutembelea hitimisho lao wamebaini tatizo lililopo ni uzalishaji si sahihi kutokana na ubovu wa mitambo.

“Pili tumejifundisha na kuona usimamizi na hapa kuna kutokuwajibika kwa watendaji kuona wanajionea, lakini shida katika kufanya uamuzi,” amesema.

Tatu, alichokibaini kuna shida katika kuwaunganishia wateja huduma, huku akieleza kuna maombi mengi na mengine wameshapokea fedha, lakini huduma walengwa haijawafikia.

“Kulingana na taarifa yao, mwaka mzima walioomba kuunganishiwa huduma wapo 55,547 na walilipia na wanaosubiri kuunganishiwa wapo 6,891,” amesema.

Amesema kingine walichokibaini watumishi wa taasisi hiyo wamejiachia kiasi kwamba hawajui namna ya kutekeleza majukumu yao.

“Watendaji wamekuwa wakiongea uongo kila mtumishi unayemuliza kitu anakupa majibu tofauti, wakati mwingine hadi waliopewa kusimamia nafasi fulani,” amesema.

Baada ya katibu kkuu huyo kuwasilisha taarifa yake, Waziri Aweso aliyeonekana kukerwa, alianza kwa kumuuliza Mhandisi Shaban kwamba katibu mkuu alifanya ziara siku mbili katika kituo chako cha kazi alikuwa wapi.

Mhandisi Shaban: Sikwepo mkuu

Waziri Aweso: Anayesimamia kitengo cha shughuli za matengenezo ya mitambo ni nani?

Mhandisi Shaban: Ni mimi mheshimiwa

Waziri Aweso: Inakuwaje katibu mkuu anafanya ziara ya siku mbili katika eneo lako la kazi na hujashiriki.

Mhandisi Shaban: Mheshimiwa tulipewa maelekezo na mkuu kwamba katibu mkuu anataka watu wa operesheni, tu.

Waziri Aweso: Mtendaji mkuu wa operesheni ni nani?

Mwandisi Shaban: Ni mimi na anapokuja kiongozi wangu mkuu katika ukaguzi natakiwa kuwepo.

Waziri Aweso: Ofisa Mtendaji Mkuu (Kiula Kingu) ulikuwepo?

Waziri Aweso: Mhandisi Shaban tumeenda wote Chuo cha Ardhi kuangalia ujazo wa maji kwenye tanki la kuhifadhi lita milioni 40 yalikwepo?

Mwandishi Shaban: Hayakuwepo.

Waziri Aweso: Tulienda kwenye flow mitter zinafanya kazi?

Mhandisi Shaban: Hazifanyi kazi.

Waziri Aweso: Unapokuja mtu ameandika kwenye daftari kiwango cha maji yanayozalishwa anakuwa ametoa wapi kama flow mitter hazisomi?

Mwandisi Shaban: Sielewi anakuwa ametoa wapi.

Waziri Aweso: Tumeenda Kibamba kuangalia tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10 tumeyaona?

Mhandisi Shaban: Hakuna maji kabisa, hayasomi.

Waziri Aweso: Hivi kama maji hakuna malalamiko hayatakuwepo?

Mhandisi Shaban: Yatakuwepo.

Waziri Aweso: Ili tupate maji kuna mambo ya msingi lazima yawepo je maji yapo?

Mhandisi Shabani: Maji yapo.

Waziri Aweso: Je umeme upo?

Mhandisi Shaban: Umeme upo.

Baada ya hapo, Waziri Aweso alimwomba mwenyekiti wa bodi hiyo, Jenerali mstaafu, Davis Mamunyange kuzungumza, naye amesema katika ziara waliyofanya maeneo machache waliyotembelea imewatupa picha sahihi ya halisi ya huduma ya maji.

“Hali ya utoaji huduma ya maji kwa kweli ni mbaya na ziara aliyofanya katibu mkuu ilikuwa ya kushtukiza, zinafaa zaidi kuliko zile rasmi kwa kuwa watendaji wanakuwa wamejiandaa,” amesema.

“Mimi sikutarajia na wajumbe wenzangu wa bodi tutakuta hali hiyo, imetustua. Ni jambo ambalo hatukulitarajia na hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa,” amesema Jenerali Mwamunyange.

Amesema kama bodi watakaa kikao na kufanyia kazi maagizo yaliyotolewa na waziri huyo kwa kuzingatia utaratibu wa bodi hiyo.

Baada ya Jenerali Mwamunyage kumaliza kuzungumza, Waziri Aweso amemshukuru na kusema: “Lazima uamuzi nichukue kwa sababu napokea malalamiko mengi kutoka Dar es Salaam na kama mnavyojua Dar es Salaam kama haina maji hatupati pa kuhemea.”

Waziri Aweso akaiomba bodi ya Dawasa wakubali kumsimamisha Kaimu Ofisi Mtendaji Mkuu, Kingu pamoja na Mhandisi Shaban kupisha uchunguzi na wanapaswa kutoa maelezo kwa bodi kwa nini maji kwenye matenki hakuna, ilihali kwenye vyanzo yapo, umeme upo na pampu zinafanya kazi.

Amesema katika kipindi ambacho wamesimamishwa viongozi hao, Dawasa itakuwa chini ya Wizara ya Maji.

Related Posts