Kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa na wizara ya mambo ya ndani mapema leo asubuhi, chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia cha National Rally kinachoongozwa na mwanasiasa maarufu nchini Ufaransa Marine Le Pen, kimepata asilimia 33 ya kura, kikifuatiwa na kundi la vyama vya mrengo wa kushoto lililojipatia asilimia 28 huku vyama vya siasa za wastani ikiwemo kile cha Rais Emmanuel Macron cha Muungano wa pamoja kikipata asilimia 20 tu ya kura.
Waziri Mkuu wa Ufaransa Gabriel Attal, ambaye ni mshirika wa Macron amesema:
” Somo tulilolipata usiku wa leo ni kwamba chama cha mrengo wa kulia kinakaribia kwenye madaraka. Kamwe katika demokrasia yetu, Bunge halijawahi kuwa hatarini kutawaliwa na watu wenye siasa kali za mrengo wa kulia. Kwa hivyo lengo letu liko wazi: Kukizuia chama cha National Rally kisiwe na wingi wa viti bungeni katika duru ya pili ya uchaguzi, kisiweze kulitawala Bunge na kuitawala nchi kwa sera yao mbaya.”
Soma pia: Chama cha Le Pen chashinda duru ya kwanza ya uchaguzi Ufaransa
Ukizingatia sheria ya uchaguzi nchini Ufaransa, kwa kuwa hakuna chama kilichotimiza asilimia 50 ya kura katika duru ya kwanza, vyama vikuu viwili vilivyoshinda duru ya kwanza, huchuana moja kwa moja katika duru ya pili ya uchaguzi ambayo mara hii itakafanyika Julai 7. Wagombea wote waliofaulu katika duru ya kwanza wanatakiwa kufikia kesho Jumanne jioni wathibitishe iwapo watagombea tena katika duru ya pili.
Vyama vya siasa za wastani kukizuia chama cha RN
Vyama vya siasa za wastani na vile vya mrengo wa kushoto vimeapa kuungana ili kukizuia chama cha Marine Le Pen kinachopinga wahamiaji na taasisi ya Umoja wa Ulaya kuwa na wingi wa viti Bungeni.
Wanasiasa wa chama cha Le Pen wameanza pia mchakato wa kutafuta washirika kutoka vyama vidogo vya siasa za mrengo wa kulia kama kile cha Republican (LR), ambacho kilijipatia chini ya asilimia 7 ya kura. Lakini wataalam wa siasa za Ufaransa wanabaini kuwa katika duru ya pili ya uchaguzi, kura za vijana zitakuwa na nafasi kubwa ya kuamua mshindi.
Makadirio ya kura za maoni yanaonyesha kuwa chama cha RN cha Marine Le Pen kinatazamiwa kuwa na wingi wa viti katika Bunge lijalo, lakini hadi sasa haijulikani ikiwa chama hicho kitapata udhibiti kamili wa bunge kwa kujikusanyia jumla ya viti 289 kati ya 577.
Rais Emmanuel Macron ambaye umaarufu wake umepungua kutokana na sera zake kupingwa na wananchi, aliitisha uchaguzi wa mapema baada ya chama chake kuangushwa na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia katika uchaguzi wa bunge la Ulaya uliomalizika mapema mwezi uliopita.
(Vyanzo: Mashirika)