Magamba ya samaki kaa kuzalisha nyuzi, nguo, ‘tishu’

Dar es Salaam. Katika kusaidia mapambano ya uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na utupaji taka holela, mwanafunzi wa shahada ya uzamili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amebuni namna magamba ya samaki aina ya kaa yanavyozalisha nyuzi na nguo.

Magamba hayo ya kaa ambayo kwa sasa huishia madampo katika maeneo mbalimbali, yanapochanganywa na mwani, huweza kutengeneza nyuzi kwa ajili ya kushonea vidonda kwa wagonjwa hospitalini, aina tofauti za nguo na hata karatasi nyeupe za kufutia mikono (tissue).

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Julai mosi, 2024 katika maonyesho ya 48 ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba), Cosmas Kindole, mhadhiri msaidizi chuoni hapo amesema kuzagaa kwa taka hizo ndiyo kulimfanya kufirikia namna inayoweza kuzifanya zirudi katika matumizi kwa namna tofauti.

Amesema moja ya bidhaa zinazozalishwa ni nyuzi zinazotumika kutengeneza nguo na kushonea vidonda hospitalini.

“Sisi tumeweza kutumia uchafu unatupwa mtaani kuuridisha katika matumizi kwa aina nyingine, kwa takwimu tulizonazo mpaka sasa Afrika Mashariki inazalisha tani kati ya milioni 6 hadi 8 kwa mwaka za magamba haya na yote yanatupwa kama uchafu,” amesema Cosmas.

Mbali na magamba hayo, pia aina ya malighafi wanayoitafuta katika magamba ya kaa huweza kupatikana kwenye senene na ngisi.

Pia kupitia mwani na magamba hayo wamezalisha plastiki inayooza, inayoweza kutumika kama vifungashio vya chakula.

Amesema ikiwa kifungashio hicho kutawekwa katika keki, huku akieleza kuwa plastiki hiyo pia mtu huweza kuila kama sehemu ya chakula.

Cosmas amesema gram 500 pekee za magamba ya kaa yanatosha kuzalisha kimiminika (gel) lita moja kilicho na uwezo wa kuzalisha nyuzi nyingi na ikiwa nyuzi hizo zitatumika kutengeneza nguo, basi itakuwa fulana moja na jeans mbili.

“Hii ni sehemu ya kazi yangu katika masomo ya shahada ya uzamili ninayosoma, tayari tumeshafanya majaribio ya nyuzi hizi katika kushona nguo, ikawa na ubora wa kiwango kikubwa. Kwa upande wa binadamu bado hatujafanya majaribio kwa sababu ni ngumu kutumia mwili wa binadamu kwa majaribio,” amesema Cosmas.

Kwa sasa utafiti wake uko katika hatua mbalimbali za kukamilisha utafiti wake ambao anaamini baadaye ukitumika ipasavyo utasaidia kupambana na uchafuzi wa mazingira na kuzalisha ajira kupitia uzalishaji bidhaa mbalimbali.

Akizungumza mmoja wa watembeleaji wa mabanda hayo, Ezekiel Kaswagula amesema endapo wazo hilo litafanyiwa kazi kilamilifu ni vyema itakuwa na faida kubwa.

“Kinachotakiwa kufanyika huko mbeleni ni kutoa elimu ya kutenganisha hizo taka, kama ni hoteli zinazouza vyakula vya aina hii basi wajue namna ya kuweka kile kinachohitajika pembeni na si kuchanganywa na taka nyingine, ili kuweka urahisi katika urejelezeshaji,” amesema Kaswagula.

Hilo linaweza kusaidia shughuli kufanyika kwa urahisi badala ya kulazimisha watu kuanza kufanya kazi ya kutafuta malighafi wanazohitaji katikati ya taka nyingi.

Related Posts