M23 yaiteka miji miwili muhimu katika wilaya ya Lubero – DW – 01.07.2024

Kwa sasa mapigano makali yanaripotiwa katika kijiji cha Bingi ambako waasi hao wanadhamiria kuyateka makao makuu ya wilaya ya Lubero. 

Ni miji midogo na muhimu ya Kanyabayonga pamoja na Kirumba ilioanguka mikononi mwa waasi wa M23 wikendi iliyopita. 

Waasi hao walisonga mbele na kuteka kijiji cha Kaseghe duru kutoka eneo hilo zimeeleza.

Kwa mjibu wa mashirika ya kiraia katika wilaya ya Lubero, mapigano makali yalizuka asubuhi ya leo jumatatu katika kijiji cha Bingi, kaskazini magharibi ya mji mdogo wa kibiashara wa Kirumba. 

Bingi ni kijiji muhimu kutokana na madini ya  dhahabu inayopatikana chini ya ardhi yake. 

Soma pia: Mapigano yaongezeka mashariki ya Kongo 

Na akizungumza na wanahabari katika mji wa Lubero makao makuu ya wilaya hiyo, mkuu wa wilaya hiyo kanali Kiwewa Mitela Alain, alianza kuwapa pole wakaazi wa wilaya yake waliokimbia mapambano yanayoendelea kusini mwa wilaya yake.

“Nawapongeza raia na kuwakumbusha kwamba jeshi letu liko nasi na wawe na imani na jeshi hilo kwani tutamshinda adui huyo. Tunavyozungumza hapa kunayo mapigano kati ya majeshi yetu na hao magaidi wa jeshi la rwanda pamoja na vibaraka vyao.”

Rais Tshisekedi awapa pole wakaazi wa Kanyabayonga

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Félix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Félix TshisekediPicha: DW

Akiwahutubia wananchi kupitia siku kuu ya uhuru wa Congo, Rais Félix Antoine Tshisekedi aliwapa pole wakaazi wa Kanyabayonga na Kayna, baada ya M23 kuteka miji hiyo.

Aliwasifu pia wanajeshi wanao mwaga damu yao kwaajili ya kulinda mipaka ya nchi. 

“Heshima na bidii kwa vigogo wanajeshi ambao wanalinda nchi katika uhaki na kumwaga damu yao. Taifa litawakumbuka daima. Katika kipindi hiki ambacho nchi yetu inakabiliwa na change moto nyingi za kiusalama, naomba jamii zote kuungana pamoja katika umoja na mshikamano ili kutusanye nguvu zetu pamoja katika heshima yote ili tuwezekuimarisha mabadiliko ya nchi yetu kijamii na kiuchumi,” ameeleza Tshisekedi.

Mapigano baina ya waasi wa M23 na jeshi la serikali katika wilaya ya Lubero yakiwa yanashika kasi, hali ni ya wasiwasi katika miji ya Beni na Butembo, wakaazi wa miji hiyo wakiwa hawajui ni wapi watakimbilia ikiwa M23 itaamua kuteka miji yao. 

Hali hiyo imewapelekea vijana wengi kupiga doria usiku katika baadhi ya barabara, kuwatafuta waasi ambao wanawezakujipenyeza katika mji wa Butembo. 

Soma pia: Waasi wa M23 wauteka mji wa Kanyabayonga   

Usiku wa kuamkia leo, vijana hao wanaojiita kuwa vijana waangalifu, walichoma moto magari tano ya mashirika yasiokuwa ya serikali, pale wafanyakazi wa mashirika hayo walipokuwa wanaelekea Butembo kukimbia mapigano eneo la Kanyabayonga na Kirumba. 

Duru nyingine zasema kwamba, kuna wafanyakazi kumi na nne wa masharika hayo waliotekwa nyara na vijana waangali jana, na 12 kati yao ndio wameonekana na isijulikane waliko wengine wawili. 

 

Related Posts