Nairobi. Frank Okoth, mmoja wa vijana waliokuwa wakiandamana nchini Kenya maarufu ‘Gen Z’, amesimulia namna alivyokwepa umauti baada ya kudaiwa kupigwa risasi sita na Polisi.
Awali, Jumanne ya wiki iliyopita katika maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha wa Mwaka 2024, zilisambaa video za Okoth zikimuonyesha akiwa hoi, huku mwili wake ukiwa na matundu ya risasi kifuani na tumboni.
Akifanya mahojiano na kituo cha Citizen Tv cha Kenya, Okoth amesema alipopigwa risasi, wenzake walifahamu amefariki, hivyo walimuweka katika orodha ya vijana waliopoteza maisha katika tukio hilo.
Amesema baada ya tukio hilo alikimbizwa hospitali jijini Nairobi na jana Jumapili, Juni 30, 2024 alipotembelewa na Citizen ameshukuru Mungu kwamba hajapoteza maisha.
“Maisha yangu nimelelewa na bibi, sina wazazi na nimekuwa nikitafuta kazi bila mafanikio. Siku ya maandamano nilikuwa mbele na nilikuwa nime-focus na waliokuwa wakitupiga mabomu ya machozi mbele yetu, lakini walionitandika risasi walikuwa pembeni.
“Baada ya tukio hilo alikuja rafiki yangu akaniambia watu huko mitandaoni wameshakuandikia upumzike kwa amani maana umeshakufa, nikamwambia mimi sijafa niko mzima,” amesema.
Amesema mahali alipo sasa hakuna huduma anazopata na anashindwa hata kugeuka, huku akiiomba Serikali kuyatatua yale wanayoyalalamikia ili wapate haki yao.
“Kuhusu maandamano lazima tutaendelea hadi pale tutakapopata haki yetu,” amesema Okoth.
Baada ya maandamano makubwa ya Gen Z yalisababisha Serikali kupitia Rais wa nchi hiyo William Ruto kukataa kusaini Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2024 uliokuwa ukipingwa vikali.
Rais Ruto aliitoa kauli hiyo Juni 26, 2024, ikiwa ni siku moja tangu vijana nchini humo wafanye maandamano yaliyochangia kuwapo kwa uharibifu mkubwa, hasa katika eneo la Bunge nchini humo na kusababisha vifo na majeruhi.
“Sitosaini Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2024 kutokana na shinikizo la umma,” alisema Rais Ruto.
“Kwa sababu tumeuondosha muswada huo, inabidi tufanye mazungumzo kama Taifa jinsi tutaweza kuiendesha nchi pamoja na deni tulilonalo kwa pamoja, nitapanga kufanya mazungumzo na nitawasikiliza vijana wa nchi yetu na watoto wetu,” alisema.